


.jpg)
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Erica Mussika, na Mkurugenzi Mtndaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Xavier Tilweselekwa, hawajakamtwa, kinyume na agizo la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Pinda aliagiza wasimamishwe kazi na kukamatwa kisha wafikishwe mahakamani kutokana na halmashauri zao kubainika kufuja fedha za umma.
Habari za uhakika zinadai kuwa wakurugenzi hao wanaendelea kufanya kazi kama kawaida. “Bado Mkurugenzi Mtendaji wa hapa kwetu Sengerema anaendelea na kazi; na mpaka sasa yuko Dodoma kikazi,” kilidai chanzo chetu cha habari katika wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.
Habari zinasema kuwa Mkurugenzi huyo anaendelea kufanya kazi kwa vile hajatumiwa barua rasmi inayomuamuru akabidhi ofisi.
“Mkurugenzi wetu bado yuko kazini kama kawaida, hata jana (juzi) alikuwa kazini kama kawaida,” kilidai chanzo kingine cha habari kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Inadaiwa kwamba Tilweselekwa anaendelea na kazi na kwamba bado hajakamatwa wala kuhojiwa kama alivyoagiza Waziri Mkuu Pinda.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, hakupatikana kuzungumzia suala hilo.
Mei 9, mwaka huu, Pinda aliagiza wakurugenzi wa halmashauri za wilaya za Sengerema na Misungwi wakamatwe na kufikishwa kortini kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha za umma.