Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Udhamini Kilimanjaro waweka rekodi Stars

11th May 2012
Print
Comments
Rais wa TFF, Leodegar Tenga

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) juzi usiku iliweka historia mpya katika michezo nchini kwa kusaini mkataba wa kuidhamini timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, wenye thamani ya Sh. bilioni 23 ambapo wadau wa soka nchini wamesema kwamba haijawahi kutokea kitu kama hicho na kampuni hiyo imefungua ukurasa mpya.

Udhamini huo mpya wa TBL na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni wa miaka mitano (Sh. bilioni 2 kwa mwaka) na umeupiku kwa takriban mara tatu udhamini uliopita wa kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) walioanza kuidhamini Stars mwaka 2006 kwa Sh. milioni 700 kwa mwaka.

Akitangaza udhamini huo, Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe, alisema kuwa udhamini wao utazingatia mambo yote muhimu kuanzia kuiweka timu kwenye kambi yenye hadhi (hoteli ya nyota tatu), kuboresha mara mbili posho za wachezaji, kuitafutia mechi za kirafiki dhidi ya timu bora na kuwapatia vifaa vyenye ubora unaolingana na heshima ya nchi.

Kavishe alisema pia Stars itanunuliwa basi la kisasa lenye uwezo wa kubeba watu 40 na kusisitiza kuwa ili matokeo mazuri yapatikane ni lazima ushirikiano wa wadau uwepo kwa kujitokeza kuishangilia timu hiyo wakati wowote inapokuwa inacheza.

"TFF na TBL peke yao hawatoshi kuifikisha Stars katika kilele cha mafanikio, wote tushirikiane kuhakikisha timu inashinda," alisema Kavishe.

Alisema pia katika udhamini huo watahakikisha mafunzo mbalimbali ya kiufundi ya soka yanaendeshwa, semina za utawala bora zinafanyika pamoja na kuwafanya Watanzania waione timu hiyo ni yao na si ya TFF au wadhamini.

Rais wa TFF, Leodegar Tenga, aliishukuru TBL kwa kusaini mkataba huo na kusema kwamba ni wa kihistoria kwenye soka la Tanzania.

Tenga alisema kuwa udhamini huo utasaidia kukuza na kuendeleza kiwango cha soka nchini jambo ambalo ndio malengo yao.

Alisema kuwa ili soka lifanikiwe ni lazima kuwepo na uwekezaji imara na kueleza kwamba hicho ndicho kilichofanywa na kampuni hiyo mwaka huu.

"Tunasonga mbele, tunafahamu kuwa changamoto huja kutokana na uwajibikaji," alisema rais huyo.
Aliongeza kwa kusema kuwa Taifa Stars ni ya wote na si ya mtu mmoja mmoja au kiongozi.

Mdau wa soka, Jamhuri Kihwelu 'Julio', ambaye ni beki wa zamani wa Simba na kocha wa timu ya soka ya vijana wa umri chini ya miaka 23, alisema kuwa huu ndio wakati wa wachezaji wa Tanzania kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali watakayoshiriki na kuhakikisha heshima ya timu hiyo inarejea kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Julio ambaye alionekana akipiga makofi kwa furaha na kushangilia wakati alimposikia Kavishe akisema kuwa udhamini huo utahusisha basi la kisasa kwa timu ya taifa, alisema kuwa udhamini huo wa TBL

unaonyesha wazi kwamba kila kinachohitajika katika kambi kuanzia vifaa bora vitapatikana ikiwemo kuongezeka kwa posho ambao ilikuwa ni moja ya kilio cha wachezaji wa Taifa Stars.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Simba, Kassim Dewji, alisema kwamba udhamini huo ni mkubwa na ni deni kwa wachezaji watakaochaguliwa kupeperusha bendera ya nchi.

Kassim alisema kwamba hiyo itawafanya kila mchezaji aone kuwa ana jukumu la kuipa timu matokeo bora na hapo pia wachezaji husika watakapofaidika.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment