Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wafanyakazi watambue haki na wajibu wao

1st May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Leo Watanzania wanaungana na wafanyakazi wote duniani kuadhimisha siku ya Wafanyakazi Dunia maarufu kwa jina la Mei Mosi. Ni siku muhimu kwa wafanyakazi duniani kote kukutana na kutafakari hatma yao katika kuuza jasho lao kwa wenye mitaji.

Ni siku ambayo husherehekewa kote duniani kufurahia hatua ambayo imepigwa na wafanyakazi katika kutimiza wajibu wao, lakini pia wakitazama wanavyonufaika na jasho lao katika harakati za uzalishaji mali.

Miaka ya nyuma katika nchi zilizokuwa zinafuata siasa za kijamaa kama Tanzania mbazo njia kuu za uchumi zilikuwa mikononi mwa dola, siku ya leo mbali ya kutumiwa kuwatunukia wafanyakazi bora pia ilitumiwa na viongozi wakuu wa serikali, aghalab Rais, kutangaza nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma, leo hii hali ni tofauti kidogo kutokana na mfumo wa uchumi ndani ya serikali na taasisi zake.

Hata hivyo, bado wafanyakazi bora wanaendelea kukumbukwa na kutunukiwa kwa uwajibikaji wao, ambao kimsingi umejidhihirisha kuwa wa kipekee miongoni mwa wafanyakazi wengine mahali pa kazi.

Mfumo huu pamoja na udhaifu wowote unaweza kufungamanishwa nao, bado umeendelea kutumika kuamsha hamasa ya kutambua michango ya wafanyakazi na kuweka ushindani miongoni mwao na hivyo kutuzwa kuwa sehemu ya utamaduni unaoendelea kudumishwa hadi sasa.

Kwetu Tanzania leo wafanyakazi wanaikumbuka sikukuu yao kwa hali ya mchanganyiko zaidi; wanajitazama katika kioo kinachoakisi walikotoka katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita tangu waliposherehekea tena siku kama ya leo, wanajiuliza maswali kama changamoto zilizokuwa zinawakabili mwaka jana siku kama ya leo bado ziko? Je, zimepunguzwa makali au yameongezeka? Wanajiuliza tena kama kumekuwa na juhudi za makusudi za kisera na kisheria za kukabiliana na changamoto hizo?

Itakumbukwa kwamba mwaka juzi kulikuwa na mvutano mkali baina ya Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (Tucta) na serikali juu ya haki za wafanyakazi.

Eneo moja lililokuwa linapigiwa kelele sana ni viwango vya mishahara serikalini. Wakati Tucta walikuwa wakipiga kampeni kima cha chini kiongezeke hadi Sh. 350,000 kwa mwezi, mapendekezo hayo yalizua mzozo mkubwa baina ya wafanyakazi na serikali, kila mmoja ukiutuhumu mwingine kwa kutokujali hali halisi ya uchumi.

Kimsingi hali ya uchumi mwaka huu ni mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka jana siku kama ya leo, mfumuko wa bei umeongezeka sana, gharama za maisha zimekwenda juu zaidi, idadi ya wafanyakazi ambao wanapoteza kazi kutokana na kuyumba kwa uchumi duniani ni wengi; hali hii kwa ujumla wake inaathiri sana wafanyakazi na familia zao, lakini pia inapunguza uwezo wa serikali kutimiza majukumu yake makubwa, kama kujenga mfumo wa miundombinu kwa taifa hili.

Madhara ya mdororo wa uchumi ulioikumba duniani miaka ya hivi karibuni bado umeendelea kuwa na madhara kwa taifa hili, uwekezaji kutoka nje umeathirika. Pamoja na madhara haya, bado wafanyakazi wameendelea kutaabika kwa ujira ambao hautoshelezi mahitaji yao ya lazima ya kila siku. Hali inazidi kuwa mbaya mwaka baada ya mwaka.

Ndiyo kusema kuwa wakati wafanyakazi wakiadhimisha sikukuu yao leo, hakika wanaendelea kuvumilia machungu mengi, wanaendelea kusononeka.

Ni kwa hali hii tungependa kuwaasa waichukulie sikukuu hii kama jukwaa muhimu la kutafakari mustakabali wao na nini kifanyike kujikwamua katika mkwamo huu mbaya wa kiuchumi ili kufufua uzalishaji zaidi na kuongeza tija ili kuchochea faida katika uzalishaji na kwa maana hiyo kujihakikishia ujira mno zaidi.

 

Kila la heri Tume ya Katiba

LEO ndiyo siku iliyotangazwa rasmi kwamba Tume ya Katiba inaanza kazi yake rasmi. Tume hii inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba kama Mwenyekiti ikiwa na wajumbe 30, itakuwa na kazi kubwa ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya kuandika katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tunatambua na kuwaheshimu kwa kiwango cha juu wajumbe walioteuliwa kuunda Tume hii, ni watu waadilifu katika jamii, wanatazamwa kwa macho ya matarajio makubwa kwamba wataongoza kazi hii ya kutafuta maoni ya wananchi kwa uadilifu uliotukuka.

Wananchi wana imani na Tume hii, wanaamini kwamba chini ya Tume hii kazi ya kukusanya maoni itaendeshwa kwa umakini mkubwa, uaminifu na kuzingatia kwa kiwango cha juu kabisa kila kauli itakayotolewa na wananchi. Tume hii inatarajiwa kuwa itatenda haki kwa wananchi. Kazi yake ni kuwasikiliza wananchi, na si kuibua maoni yake peke yake.

Umma wa Tanzania unafahamu Jaji Warioba vilivyo, pia unamtambua Makamu wake, Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani, unatambua uadilifu wao wa miaka yote ya utumishi wao, unawaelewa kama viongozi ambao hawajawahi kuyumba katika misimamo ya kimaadili, ni kwa hali hii tuna imani kwamba leo Tume inaaza kazi ngumu na ndefu ya kuwaongoza Watanzania kufanya jambo la kihitoria, kuandika katiba yao mpya. Kila la kheri Tume ya Katiba.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles