Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Banyana waja kuivaa Twiga Stars J`pili

16th May 2012
Print
Comments
Kocha wa Twiga Stars, Boniface Mkwasa

Baada ya kupokea kichapo cha magoli 4-1 kutoka kwa Zimbabwe wiki iliyopita, timu ya soka ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, inatarajia kucheza mechi nyingine ya kirafiki na wenzao wa Afrika Kusini, Banyana Banyana, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumapili.

Twiga Stars, Banyana Banyana na Zimbabwe zote zinajiandaa na mechi zao za kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Novemba nchini Equatorial Guinea.

Akizungumza jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa mechi hiyo ya pili itaisaidia Twiga kujiimarisha na kuingia katika mechi yao dhidi ya Ethiopia ikiwa kwenye hali nzuri ya kiushindani.

Wambura alisema kuwa Banyana Banyana ndio wameomba kucheza na Twiga ambapo mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika mechi ya ufunguzi ya fainali zilizopita za Afrika kwa wanawake mwaka juzi jijini Johannesburg, Afrika Kusini ambapo wageni hao walishinda magoli 2-1.

Alisema kuwa katika kuboresha kikosi hicho, kocha wa Twiga Stars, Boniface Mkwasa, amemuongeza mshambuliaji mkongwe, Esther Chabruma 'Lunyamila', kwenye kikosi chake.

Chabruma ameitwa kwenye kikosi hicho kutokana na uwezo alionao licha ya kuwa nje wakati timu hiyo inaikabili Namibia mapema mwezi Januari mwaka huu.

Wakati huo huo, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Rwanda kuchezesha mechi hiyo ya kati ya Ethiopia na Twiga Stars itakayochezwa jijini Addis.

Waamuzi hao ni Angelique Tuyishime atakayepuliza filimbi wakati waamuzi wasaidizi ni Sandrine Murangwa, Speciose Nyinawabari na Salma Mukansanga huku Kamishna wa mchezo huo wa kwanza ni Catherine Adipo kutoka Uganda.

Timu hizo mbili zitarudiana baada ya wiki mbili kwenye Uwanja wa Taifa jijini na mshindi atakuwa amefuzu tiketi ya kucheza fainali hizo zijazo za Afrika kwa wanawake.


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles