Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Waziri Nagu azitaka benki kupunguza riba

25th April 2012
Print
Comments
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk. Mary Nagu (kulia),akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Akiba Commercial Bank, John Lwande, baada ya kuzindua Huduma ya ACB Mobile katika hafla iliyofanyika tawi la Kijitonyama jijini Dar es Salaam jana. (PICHA:SELEMANI MPOCHI)

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwezeshaji na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu, amezitaka benki nchini kurahisisha masharti ya mikopo kwa wateja wake sambamba na kupunguza viwango vya riba kwa wakopaji.

Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua huduma ya Akiba Commercial Bank Mobile katika tawi la Kijitonyama inayotolewa na Akiba Commercial Bank (ACB).

Dk. Nagu alitoa wito kwa uongozi wa ACB kuhakikisha kuwa utoaji wa huduma ya Akiba Commercial Bank Mobile unakidhi matarajio ya watanzania kwa ujumla.

“Mteja anaponunua umeme (Luku) kupitia ACB Mobile, apate umeme kwa wakati alioutarajia na sio usumbufu wa kuambiwa kuwa hawezi kupata huduma hiyo kwa muda huo kutokana na visingizio mbalimbali, kama hitilafu ya mitambo,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Akiba Commercial Bank, John Lwande, alisema kupitia huduma hiyo ya simu ya mkononi, mteja wa ACB atapata huduma ya kujua taarifa za akaunti yake, kulipia DSTV, maombi ya hundi na marejesho ya mikopo.

Huduma nyingine ni kulipia ankara za maji (Dawasco), kujua taarifa ya akaunti yake, kuongeza muda wa maongezi wa simu yake ya mkononi, uhamishaji wa fedha kutoka akaunti moja kwenda nyingine,kupata taarifa mbalimbali za kibenki.

Alisema ACB tangu ianzishwe 1997  kama benki ya kibiashara ikiwa na dhumuni la kumuwezesha mwananchi wa kipato cha chini kupata huduma za kibenki, mpaka sasa inawateja 23,000 na akaunti 190,000 za wateja.

Lwande alisema ACB kwa sasa ina matawi 15 nchi nzima, matawi 13 Dar es Salaam, tawi moja Moshi na lingine Arusha, na hivi sasa wanatarajia kufungua tawi la 16 jijini Mwanza.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles