Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

NECTA kupewa meno

5th May 2012
Print
Comments
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani Taifa (Necta)

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani Taifa (Necta), imesema kuwa itafanyia marekebisho baadhi ya sheria zinazolihusu baraza hilo ili kulipa  meno ya kuwawajibisha moja kwa moja watu wanaohusika na kughushi vyeti na udanganyifu wa mitihani.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Remigius Ntyama kwa niaba ya Naibu Waziri wa wizara hiyo, Philipo Mulugo, katika mahafali ya chuo cha ualimu cha Capital.

Alisema baadhi ya sheria zilizopo zimekuwa zikilifanya Baraza hilo kukosa meno ya kuwawajibisha watu wa aina hiyo.

Ntyama alisema, utaratibu wa hivi sasa wa baraza mara baada ya kubainika kwa vyeti vya namna hiyo, chuo husika ndicho kinachoachiwa kazi ya kuchukua hatua. Hata hivyo, alisema hali hiyo imekuwa ikitoa mwanya kwa wahusika kutoroka.

Alieleza kuwa suala la Baraza kuchukua hatua amelichukuwa na utaratibu utawekwa ili liwe ndiyo lenye uwezo wa kuchukua hatua mara linapogundua kuwa cheti kimeghushiwa.

Kwa upande wa Mkuu wa chuo hicho, Khan Nassor Charokiwa, alisema utaratibu wa uhakiki wa vyeti vya wanachuo unaofanywa na baraza hilo umekuwa ukiondoa dhana nzima ya zoezi hilo kwani lengo la kupeleka vyeti kwa uhakiki baraza ili kubaini vilivyohalali hurudisha kesi kwa vyuo kuwa hawafanyi kazi vizuri.

Alisema hali hiyo ni kuwaonea kwani vyeti vya taaluma ya sekondari anayeweza kuvichambua vema ni Baraza na sio mtu mwingine yeyote.

Mkuu huyo alisema changamoto hiyo inatokana na kutokuwa na ofisi za Baraza la mitihani kanda ambapo kungetoa nafasi kubwa kwa vyuo hivyo ambavyo vipo mikoani kusafirisha vyeti ni tatizo hasa ikitokea upotevu au ajali.

Pia alitoa ombi kwa serikali kusitisha badiliko la sifa za udahili kwa mwaka huu kutoka pointi 28 hadi 27 katika kozi ya ualimu.

Alisema  wao kama chuo wanaelewa umuhimu wa kuongeza sifa za kujiunga ili wapatikane walimu bora lakini kabla ya kupata waraka wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Machi 13, 2012 tayari walikuwa wameshatangaza na kupokea maombi ya wanafunzi mara baada ya matokeo ya kidato cha nne.

Alieleza kuwa mabadiliko hayo yamekuja ghafla wakati watanzania wengi ufaulu wao haukuwa mzuri hasa wale waliosoma shule za kata kutokana na mazingira ya shule hizo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles