Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Afrika iko tayari kwa biashara?

20th May 2012
Print
Comments

Wiki iliyopita imekuwa ya neema kwa Rais Jakaya Kikwete, kana kwamba ilipangwa apate afueni baada ya dhoruba kubwa bungeni iliyofikia kusukwa upya kwa Baraza la Mawaziri.

Rais Kikwete maarufu kama JK alikaribishwa katika mkutano maalum wa masuala ya kilimo ulioandaliwa na taasisi inayofungamana na asasi ya kimataifa ya masuala ya uchumi, World Economic Forum, na bila kungoja, akaombwa tena ahudhurie mkutano wa nchi kubwa kwa viwanda duniani, Group of Eight. Ilikuwa ni suala hilo hilo la jinsi ya kuendeleza kilimo barani Afrika, hali inayoashiria kuwa Tanzania ina sifa kiwango cha kuridhisha katika eneo hilo.

Ikikumbukwa kuwa Rais Kikwete alikuwa kiongozi wa kwanza kutoka nchi za Afrika kupata mwaliko Ikulu ya Marekani baada ya Rais Barack Obama kuingia madarakani, ni wazi kuwa hakuna jambo lolote ambalo limepunguza sifa ya Tanzania hadi sasa.

Siyo tofauti na alivyoalikwa Mwalimu Nyerere katika mkutano muhimu wa Cancun nchini Mexico mwaka 1983, ambako Rais Ronald Reagan wa Marekani alikataa rasmi wazo la ‘hali mpya ya uchumi duniani,’ambako mfumo wa biashara kati ya nchi changa na zile zilizoendelea ungefanyiwa mabadiliko makubwa.Ni sifa ya nchi, si kiongozi tu binafsi.

Mialiko hii miwili, ule wa Mwalimu Nyerere mapema miaka ya 80 na mialiko ya hivi karibuni ya JK inaonyesha kuwa hakuna uhusiano wa karibu kati ya mialiko na hali ya uchumi katika nchi, na tofauti yake ni uthabiti wa kisiasa wa kiongozi husika, na hasa mwelekeo wake kidemokrasia.

Licha ya kuwa Mwalimu hakuwa anasimamia mfumo wa vyama vingi, alikuwa na sifa ya kutetea haki na kuwa msikivu wa mahitaji ya watu, na kuwazuia wapinzani wasivuruge utawala wake, bila kuonyesha ‘makali ya dola,’ yaani ukaliti wa kunuia.Hata wale aliowaweka kuzuizini mwaka 1968 walipopinga ‘chama kushika hatamu’ bungeni, aliwapa viwanja na mikopo ya benki walipotoka, wajiendeleze.

Pamoja na sifa zinazotokana na mwelekeo wa kisiasa ambao hasa unalinda demokrasia, bado kuna suala la msingi kuhusu kiwango ambacho JK atakuwa amezisaidia nchi za G 8 kupambanua nini cha kufanya kuinua kilimo katika nchi za Afrika.

Suala hilo ni moja ya yale yanayohitaji ufumbuzi wa haraka, kwani nchi nyingi za Afrika zinatishiwa na baa la njaa, na kupatikana misaada kutoka Ulaya na Marekani inazidi kuwa vigumu, kwani kila mahali matatizo ya uchumi yamepamba moto. Suala ni kama tunachofanya hivi sasa katika kilimo ni ‘mwarobaini’ wa njaa, na kama sera hiyo inafaa kuigwa Afrika.

Labda tuanze na takwimu kadhaa, ya kwanza ikiwa ni kupanda kwa bei ya mahindi mkoa wa Rukwa mara mbili ndani ya mwezi mmoja, kutokana na wanunuzi kusambaa eneo hilo na kuchukua mahindi kutoka kwa wakulima kwani yanahitajiwa mikoa ya jirani, kama Tabora, Shinyanga na kwingineko.

Isitoshe, maeneo mengi ambako wawekezaji ambao baadhi wana shauku kubwa ya mazao ya biashara ya aina tofauti wamepewa ardhi kuna migogoro isiyoisha na wanannchi.Si rahisi kutaka G8 waridhike kabisa na hali hiyo.

Cha msingi zaidi ni kuwa katika kipindi cha miaka mitano kabla ya Azimio la Arusha, yaani kuanzia mapema 1962 hadi mwisho wa 1966, maendeleo katika sekta ya kilimo yalikuwa asilimia 13.5 kwa mwaka.

Ilishuka hadi kufikia asimilia 3.0 kwa mwaka, hali ambayo inaonyesha Azimio la Arusha lilivuruga kabisa sekta ya kilimo, na suala hilo bado halijaanza kujadiliwa na wataalamu wa uchumi,au hata kilimo, nchini. Suala la msingi ni kufafanua jinsi ya kurudi katika ukuaji wa kilimo kwa asilimia 13.5 kama katika kipindi cha awali, kwa kuangalia nyanja zote za ufanisi huo, na si kutunga vigezo.

Suala ambalo haielekei kuwa JK aliliwasilisha mbele ya wakuu hao wa G8, au katika mazungumzo binafsi na Rais Obama, ni lile la mzunguko wa fedha katika sekta ya kilimo.

Hii ndiyo tofauti kubwa kati ya kipindi cha awali baada ya uhuru ambacho Azimio la Arusha liliweka tamati yake, na ina maana pia kuwa kiburi cha kizalendo ambacho kimejengwa na Azimio la Arusha ni tatizo, kwani mradi kipo, haiwezekani kurudisha kasi ya kukua kwa kilimo kupitia mzunguko chanya wa fedha. Msingi wake ni mali binafsi, kuwa wakati ule mtu akiwa na shamba ni lake, serikali haiwezi kulichukua bila malipo kwa bei ya soko, na watu binafsi waliweza kubadilishana mali bila vizuizi.

Ukilinganisha idadi ya mabenki iliyopo leo na wakati ule, licha ya kuwa idadi ya watu imeongezeka kwa kasi, na ukiongeza pia uwezekano wa fedha kutoka nje kuingia katika mzunguko hapa nchini, ni wazi kuwa mazingira ya mzunguko wa kifedha yangekuwa bora zaidi wakati huu kuliko uliopita.

Lakini hali siyo hiyo, kwa mfano nchini Kenya maofisa wa benki wanatoka nje ya ofisi kutafuta watu wa kuwapatia mikopo –licha ya kuwa mpangilio huo unaweza kuleta mkasa kama ule wa ukopeshaji nyumba kwa ‘walalahoi’nchini Marekani, ambako kulilipuka na kusomba mabenki kadhaa, kuweka mfumo mzima wa fedha hatarini. Ni hali ambayo bado haipo hapa nchini, inasuasua tu.

Hapa nchini mabenki kwa kawaida yanarudisha watu wanaotaka mikopo, isipokuwa ya mambo madogo kama ununuzi wa magari, au kumalizia nyumba (iko mikopo ya kuweka umeme baada ya kukamilisha ujenzi), na kwa jumla mikopo kwa wafanyabiashara kuendesha shughuli, hasa za mauzo nje, n.k. Msingi wa mali binafsi unapokuwepo, kule kuaminiana katika mikopo kunarudi, kwani kunakuwa hakuna kizuizi cha kuchukua rehani iliyowekwa katika benki moja au nyingine, kama ilivyo Kenya.Hapa kwetu rehani ikichukuliwa ya watu kadhaa wenye sifa, Bunge lazima lilipuke, ‘makaburu wanatawala.’

Mradi nchi za G 8 zinafanya juhudi kujua ni kwa njia gani kilimo Afrika kinaweza kukuzwa, watalinganisha maoni na mwishowe kufikia tamati chanya. Suala la sera hapa ni kuwa serikali iondoe imani yake katika hisia kuwa ardhi ni mali ya pamoja kijijini, kwani ‘bomu linalongoja kulipuka’ la vijana kukosa kazi kwa mamia ya maelfu, hata wangekuwa na vyeti au shahada za elimu ya juu, halitaweza kutatuliwa na kubakiza ardhi mikono ya vijiji, ila kupanua uwekezaji kimsingi, viwanda na huduma nyingine zihitaji nguvu kazi yao, na pia waanze kuwa sehemu ya soko linalokua.

Ina maana kuwa inahitaji wananchi wapewe ardhi wanayoishi iwe mali binafsi, waweze kuiuza na kuanzisha miradi waajiri watu wengine, na waliobaki waweze kupata mikopo kwa rehani ya ardhi. Kuendeleza uzalendo wa kutotaka mali binafsi ni kosa – pesa ni baba, ardhi ni mama, ndipo uzalishaji utaongezeka na kukua kwa kasi; serikali haitachukua nafasi ya mabenki.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles