Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tanesco wahaha kujisafisha

8th May 2012
Print
Comments
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando

Hali ya mambo ndani ya Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), sio shwari baada ya uongozi wa shirika hilo kuanza kuhaha na kutaka kutoa baadhi ya taarifa za kujisafisha kwa umma.

Dalili za kutaka kijisafisha zilijitokeza jana mchana baada ya uongozi wa shirika hilo kuita ghafla waandishi wa habari ili kuzungumza nao makao makuu Ubungo jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando, ambaye alitaka kuzungumza na waandishi wa habari alifuta ghafla mkutano huo huku Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud,  akisema bosi wake amefikia hatua hiyo baada ya kuitwa na Waziri mpya wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye aliapishwa jana.

Profesa Muhongo jana aliapishwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini baada ya Rais Jakaya Kikwete kuvunja baraza la mawaziri wiki iliyopita na kumtupa nje aliyekuwa anashilikilia nafasi hiyo, William Ngeleja.

Sababu kubwa iliyomponza Ngeleja ni Tanesco kufanya mamunuzi makubwa ambayo yanafikia Sh. bilioni 600 kinyume na taratibu za manunuzi.

Tuhuma hizo pia zinamgusa Mhando kama mtendaji mkuu wa shirika hilo.

Habari za ndani kutoka ndani ya shirika hilo zilidai kuwa, Mhando alitaka kuzungumzia masuala mbalimbali yakiwemo ya hali ya  upatikanaji wa umeme, mita za Luki na hali ya kifedha.

Badra aliwaomba radhi waandishi waliofika kwa ajili ya mkutano huo na kuwaambia kuwa wataitwa siku nyingine kwa ajili ya mkutano huo.

Mpaka waandishi wa habari wanaondoka katika ofisi hizo, Mhando alikuwa bado wizarani ingawa haikujulikana walichokuwa wakizungumza na waziri wake.

Wiki iliyopita wakati Rais akitangaza baraza jipya alisema watu wote watakaobainika kuhusika na ufisadi katika wizara na taasisi za serikali watachukuliwa hatua na kwamba hakuna atakayebaki.

Alisema wakuu wa idara na wakurugenzi wote watakaobainika kuhusika katika ufisadi ambao ulitajwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo ilisomwa bungeni watachukuliwa hatua kali.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles