Sunday May 26, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Yanga kupata kibonde robo-fainali

21st July 2012
Print
Comments
Saidi Bahanuz akipongeezwa na wachezaji wanzake baada ya kuipatia Yanga goli la kwanza dhidi ya APR katika mechi ya kombe la Kagame uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Mabingwa watetezi Yanga jana walifanya kazi kama watumwa kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi C la Kombe la Kagame la klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati na kuifunga timu ngumu ya APR mabao 2-0, na sasa inatarajiwa kuishi kifalme kwenye robo-fainali kwa kuikabili timu dhaifu ya Mafunzo, keshokutwa.

Kwa ushindi huo wa mabao yaliyofungwa moja kila kipindi na mshambuliaji mpya, hatari, Said Bahanuzi Yanga ina nafasi kubwa ya kukutana na wawakilishi hao wa Zanzibar wenye pointi mbili na ambao wanatarajiwa kufuzu kama washindi wa pili endapo mchezo kati ya Azam na Tusker ya Kenya zenye ponti moja kila moja, utatoa mshindi kwa mara ya kwanza katika Kundi B baada ya mechi tatu.

Mafunzo ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam katika mchezo wa kwanza kabla ya juzi kutoka suluhu na Tusker, huku ikionyesha kiwango kidogo uwanjani.

Itakuwa ni mechi rahisi kulinganisha na kazi ambayo APR italazimika kufanya sasa dhidi ya washindi wa Kundi A URA ya Uganda iliyoshinda mechi zote tatu za awali, ikiwemo kuifunga Simba 2-0.

Iliichukua Yanga dakika 22 kuwainua mashabiki wake wakati krosi safi ya Hamis Kiiza ilipounganishwa vizuri na Bahanuzi.

Makosa ya beki wa kati wa Rwanda yalimpa nafasi Bahanuzi kuongeza goli la pili katika dakika ya 67  baada ya kuunasa mpira ndani ya eneo la hatari na kuachia shuti la mguu wa kushoto lilojaa wavuni.

Kuingia kwa goli hilo kulibadilisha mchezo ambapo Yanga walirudi nyuma na kulinda lango lao huku wakifanya mashambulizi kwa mipira mirefu kuelekea kwa Kiiza, na baadaye Jerry Tegete aliyetokea benchini, aliyekuwa amebaki mbele peke yake.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Kocha wa Yanga, Sam Saintfiet alisema kuwa timu yake ilicheza vizuri tofauti na michezo miwili iliyopita.

"Nimeridhika na matokeo na mchezo uliochezwa na timu Yangu... hatukucheza vizuri dhidi ya Atletico lakini tumefanya marekebisho na mmeona tulichokifanya leo (jana)," alisema Saintfiet.
Kikosi cha Yanga kilikuwa:

Yaw Berko, Juma Abdul, Stephano Mwasika, Nadir Haroub 'Canavaro', Kelvin Yondan, Chuji, Niyonzima/ Gumbo, Nizar/ Juma Seif, Oscar Joshua, Kiiza, Bahanuzi/Tegete.


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment