


Timu za soka za wabunge mashabiki wa Simba na Yanga zimepanga kurudiana kwenye mchezo utakaofanyika Agosti 25 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Awali timu hizo zilipambana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Julai 7 na Simba kuibuka na ushindi wa 3-1 baada ya kupigiana penati kufuatia kushindwa kufungana kwenye dakika 90 za mchezo huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, mmoja wa waratibu wa tamasha la matumaini linalojumuisha mchezo huo wa wabunge, Abdallah Mrisho, alisema mchezo huo umepangwa baada ya wabunge wa Yanga kuomba kurudiana na Simba ili kulipiza kisasi.
"Kiujumla tamasha hili litafanyika tena Mwanza kwa lengo lile lile la kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wasichana katika shule za sekondari, lakini kubwa zaidi wabunge wa Yanga wameomba mchezo wa marudiano ambao tumepanga ufanyike kwenye tamasha hilo," alisema Mrisho.
Aidha, alisema kuwa mbali na mchezo huo wa soka wa wabunge, pia burudani mbalimbali zitafanyika wakati wa tamasha hilo.
Alizitaja burudani hizo kuwa ni pamoja na wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya 'Bongofleva' na wale wa muziki wa injili watatoa burudani kwa wakazi wa mkoa huo wa Mwanza.
Alisema kuwa baada ya tamasha hili la Mwanza pia watapeleka tamasha hilo katika mikoa mingine lengo likiwa kufanikisha ujenzi huo wa mabweni ya wasichana.
Katika tamasha lililofanyika jijini Dar es Salaam, waandaaji walikabidhi hundi ya sh. milioni 10 kwa Mamlaka ya Elimu (TEA) inayoratibu ujenzi wa mabweni hayo.