



Operesheni ‘Okoa Kusini’ inayoendeshwa na Chadema, imewastua mawaziri wanaotokea kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara, kurejea majimboni mwao.
Taarifa za ndani kutoka vyanzo tofauti ikiwamo ndani ya jeshi la polisi, zimeeleza kuwasili kwa mawaziri hao kutokana na kile kinachoaminika kuwa ‘kuweka mambo sawa’ baada ya operesheni ya Chadema kupita kwenye majimbo yao.
Mawaziri wanaotajwa kurejea majimboni kwa nyakati tofauti ni pamoja na Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Tamisemi), George Mkuchika wa Newala (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utawala Bora), Bernard Membe wa Mtama (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa) na Mathias Chikawe wa Nachingwea (Katiba na Sheria).
Jana, Chadema iliingia kwenye siku ya 13 ya ziara yake katika mikoa hiyo, ambapo Jumanne iliyopita ilikamilisha mikutano, kufungua matawi na kusimika viongozi wa ngazi za msingi mkoani Mtwara na (juzi) ilianza mkoani Lindi.
Katika ziara hiyo, Chadema ilifika kwenye majimbo ya mawaziri hao, akiwamo Membe, ambapo watakuwa jimboni kwake leo.
Ingawa hakuna taarifa rasmi iliyohusu ziara ya mawaziri hao wakati huu wakijiandaa na Mkutano wa wa Bunge utakaoanza wiki ijayo, imeelezwa kuwa mawaziri hao hawakufanya mikutano ya hadhara, badala yake walikutana na wanachama na viongozi wa CCM kwenye vikao vya ndani.