Thursday Jun 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Werevu wa CCM unapoishia ujinga wa raia unapoanzia!

4th April 2012
Print
Comments

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbrod Slaa ‘kutungwa mimba’ ilikuwa sehemu ya kauli za wapiga debe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki mkoani Arusha.

Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, akawa kinara wa kutoa ‘matusi’ ya aina jukwaani, ambayo hata hivyo hayakukisaidia chama hicho tawala kuibuka na ushindi.

Si Lusinde peke yake, wapo waliokuwa wapiga debe wa CCM katika uchaguzi huo walikifanya chama hicho na mgombea wao, Sioi Sumari, kuwa mbali na wananchi.

Walishindwa kuwatambua raia za jimbo hilo na haki zao, walishindwa kuyatambua mahitaji ya jimbo na wananchi wake, walishindwa kufanya siasa zinazoistahili Arumeru Mashariki na watu wake.

Wapiga debe wa mgombea kupitia CCM walikuwa wanatembea njia isiyoifikia jamii pana ya wakazi wa Arumeru Mashariki, lakini hawakulibaini hilo!

Ninashawishika kuamini kwamba CCM hawakubaini namna walivyokuwa wakipotea njia, kwa maana walionywa kupitia vyombo habari, walionywa kupitia ishara za wananchi jimboni humo, walionywa na upinzani hususani Chadema, hawakusikia.

Ndio maana mbali na Lusinde ambaye siwezi kusita kumtaja kuwa mmoja wa waliochangia kushindwa kwa CCM, wapo wenginge waliotembea juu ya nyao zake.

Miongoni mwa mwao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Wassira akaibua hoja ya wizi wa michango ya Wakatoliki iliyotolewa kufanyikisha ziara ya aliyekuwa Kiongozi wa kanisa duniani, Baba Mtakatifu Yohane Paul II katika miaka ya mwanzoni mwa 1990.

Kwamba wizi huo ulifanywa na Dk Slaa wakati huo akiwa Padre wa Kanisa Katoliki na mtumishi wa Baraza la Maaskofu Wakatoliki (Tec).

Madai ya Wassira licha ya kutokuwa na uhusiano wowote na kampeni ama nafasi ya ubunge iliyokuwa ikishindaniwa, ilionekana kuwa ya kizushi, ikakanushwa na Kanisa Katoliki.

Rais wa Baraza la Maaskofu Wakatoliki (Tec), Mhashamu Yuda Thedeus Ruwai’chi ikamtaka Wassira atoe uthibitisho wa madai yake, ambapo hadi matokeo yalipotangazwa na CCM kubwagwa, haikuwa hivyo.

Mzee Mkapa naye akaingia kwenye mtego huo, akifungua kampeni hizo, akamuweka kando Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vicent Nyerere na ukoo wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Vicent na walio katika ukoo wa Mwalimu Nyerere, ‘wakamuumbua’ kwa uthibitisho kuwa aliyoyanena Mzee Mkapa hayakuwa kweli bali uongo mtupu.

Lakini kwa nini ilifikia hatua kwa wana-CCM, wakongwe na vijana kuibua kauli tata zisizokuwa na mashiko kwa umma? Kwamba zingekuwa kishawishi kwa wapiga kura wa Arumeru Mashariki?

Wakati kauli hizo zikitolewa, lengo lilikuwa kuiwezesha CCM ishinde, huo ndio werevu wa chama hicho na wapiga debe wake.

Werevu ni hali ya kutumia akili ili kupata jambo au kitu. Ni ujanja, akili, fahamu au bongo. Hapo ndipo hayo yote yalifanyika kwa CCM, tena kwa kiwango cha juu ili ipate ushindi.

Kwa wananchi haikuwa hivyo. Wananchi hawakuhitaji maisha binafsi ya Dk Slaa, hawakuhitaji matusi machafu yakiwemo kuhusu Katibu Mkuu huyo wa Chadema kupewa mimba na CCM.

Wananchi wa Arumeru Mashariki hawakuguswa na hekaya za wizi wa sadaka na michango ya Baba Mtakatifu, hawakuiona nafasi ya ukoo wa Mwalimu Nyerere katika maisha yao.

Kwa maana hayo yote yalikuwa mfano wa ubatili mbele zao, walichokihitaji ni namna bora ya kukabiliana na kero zinazowakabili, zikiwemo migogoro ya ardhi na ukosefu wa huduma muhimu za kijamii, basi.

Bila shaka wakati CCM wakipiga debe kwa hekaya hizo, walikuwa mithili ya walio katika ujinga. Wakawasikiliza, lakini hawakuwachagua.

Kampeni za uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki zilipohitimishwa, mgombea kupitia Chadema, Joshua Nassari, kuibuka mshindi, akimuangusha mshindani wake wa karibu, Sioi Sumari wa CCM.

Yapo mafunzo mengi kwa kadri ya tafsiri ya mchakato wa uchaguzi huo, lakini zaidi ni pale werevu wa CCM unapoonekana kuishia pale ujinga wa raia unapoanzia!

Ni kauli inaweza kutatiza. Lakini ukweli ni kwamba kufanya kampeni kunatakiwa chama shiriki kizishinde fikra za umma. Kiwe na werevu ulio juu ya ujinga wa umma.

Lakini kwa Arumeru Mashariki haikuwa hivyo, werevu wa CCM iliyokuwa ikitetea kiti hicho, ulipoishia, wananchi wakazitambua hila na nia ovu, wakakikataa.

Ikiwa ni hivyo, chama tawala kimeshindwa. Kimekiri kushindwa. Limekuwa jambo jema.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kwenye simu namba +255 754 691540, 0716635612 au barua pepe; mgeta2000@yahoo.com  

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment