Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Matatizo ya kisheria katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

18th May 2012
Print
Comments

Ifuatayo ni sehemu ya tafsiri ya Makala iliyoandikwa na Dk. Sengondo Mvungi ,chini ya kichwa  kisemacho “Legal Problems of the Union Between Tanganyika and Zanzibar” (East Africa Law Review, jarida la Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu, 2003) kwa Kiswahili ikiwa ni “Matatizo ya Kisheria katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar” kama iliyotafsiriwa na, Denis Maringo. 

Dk. Mvungi ni mjumbe wa Tume ya Kukusanya na kuratibu maoni ya Katiba mpya ya Tanzania na aliandika makala haya wakati alipokuwa Mhadhiri na pia Mkuu wa Kitivo Cha Sheria Mlimani . Makosa yoyote katika tafsiri ni ya yule aliyetafsiri na si mwandishi wa makala kama ilivyokuwa katika uhalisia wake kimombo. 

Utangulizi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muungano wa zolizokuwa dola mbili huru atika Afrika, zikiitwa, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Jamhuri hizi mbili zilisaini mkataba wa muungano mnamo Aprili 22, 1964 na kuzaa Jamhuri moja kuanzia Aprili 26, 1964.

Muungano huu unajumuisha serikali mbili, moja ikibeba mamlaka ya ki-utawala katikamambo yote ya muungano huku, wakati ule ule, ikiwa na mamlaka ya ki-utawala ndani na kwa ajili ya (sehemu iliyokuwepo) Tanganyika. 

Serikali yenye mamlaka inayojitegemea ijulikanyo kama Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina nguvu za ki-mamlaka katika masuala yasiyo ya muungano ndani na kwa ajili ya Zanzibar. 

Tanganyika ilikuwa sehemu ya Deutsch-Ostafrika, koloni lililokuwa linamilikiwa kibeberu na Ujerumani likihusisha pia Rwanda na Burundi kuanzia Februari 17, 1885 hadi Juni 28, 1919 (rejea kitabu kilichoandikwa mwaka 1973 na E.A. Seaton na S.T. Maliti kiitwacho Tanzania Treaty Practice kuhusu uzoefu wa Tanzania kwenye mikataba ya kimataifa ; rejea pia mkataba wa Versailles wa Juni 28, 1919).

Ilipofikia Januari 10, 1920 Tanganyika, pasipo  kuhusisha Rwanda na Burundi, ikawa dola la kikoloni chini ya Uingereza  (British mandate territory) chini ya Jumuiya ya Mataifa (League of Nations). 

Mwaka 1947 Tanganyika ikawa dola la kikoloni lilikokuwa chini ya Uingereza kwa Dhamana (Trusteeship Territory) ya Umoja wa Mataifa, ambapo kwa wakati huu Umoja wa Mataifa ndio ulikuwa umezaliwa kuchukua nafasi ya iliyokuwa Jumuiya ya Mataifa. 

Desemba 9, 1961 Tanganyika ikapata uhuru na kuanza kujitawala yenyewe kama sehemu huru katika himaya ya Falme wa Uingereza na ikawa Jamhuri inayojitegemea Desemba 9, 1962. 

Zanzibar, ile sehemu nyingine yaTanzania ni eneo la kijiografia na dola inayohusisha visiwa viwili, viiitwavyo Unguja na Pemba. Zanzibar iko umbali wa kilometa 36 tu kutoka mwambao wa pwani ya Tanganyika na  ina uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria kati yake na Tanganyika. Zanzibar iliangukia chini ya utawala wa kiloni wa waarabu wa Oman mwishoni mwa karne ya 17.

Sultani wa Omani aliitwaa Zanzibar na kuifanya sehemu ya himaya yake mwaka 1832 katika mwaka ambao, Sultan Seyyid Said ibin Sultan .alipohamishia makazi yake kwa kujenga hekalu jipya la kifalme Zanzibar. Mwaka 1886 Zanzibar ikasaini mkataba wa kulindwa chini ya Uingereza.

Sultani wa Zanzibar kwa kufanya hivi akawa amejivua mamlaka ya kuamua mambo katika masuala ya ya nje ya Zanzibar na hivyo basi hakuhusishwa na mazungumzo kati ya Uingereza na Ujerumani kuhusiana na mustakabali (hatma) wa baadaye wa Zanzibar.

Mnamo Julai 1, 1890 Ujerumani na Uingereza zilihitimisha mazungumzo na kuingia mkataba ambapo Uingereza ilipewa mamlaka ya kuitawala Zanzibar na eneo la Wituland na hasa katika masuala yote ya nje na kimataifa na huku utawala wa Sultani ukiachiwa uwezo wa kujiamulia mambo katika masuala fulani fulani ya ndani pekee (suzerainty) .

Ujerumani yenyewe ikapewa mamlaka haya haya kulitawala eneo la Heligoland ambalo kabla ya hapo lilikuwa chini ya Waingereza  (Rejea Martens, N.R.G. 2Bd. 16 ukurasa wa 894). 

Kufuatia maendeleo haya, Uingereza ikajitwalia mamlaka kamili juu ya Zanzibar na punde tu ikaichukulia Zanzibar kama milki yake mpya katika himaya yake ya kikoloni. Mwaka 1914 masuala ya husianayo na Zanzibar yakahamishiwa kutoka Ofisi ya Masuala ya Nje ya Uingereza na kupelekwa katika Ofisi iliyohusika na Makoloni ya London. 

Zanzibar iliendelea kuwa himaya chini ya Uingereza hadi Desemba 10, 1963 pale ilipohitimisha mkataba wa ki-ulinzi kufuatia makubaliano ya Lancaster ambayo yalipelekea kuundwa kwa Katiba mpya ya Zanzibar chini ya Ufalme wa Uingereza.

Katiba hii haikupokelewa kwa mikono miwili wakati huu ambapo waafrika walio wengi walaikuwa katika mapambano ya kujikomboa. Waafrika hawakukubali kuona wanakuwa chini ya Sultani wa Arabia na aliyekuwa na mamlaka ya kuwatawala wao.

Kwa Waafrika, Sultani Seyyid Said alikuwa ni mkoloni ambaye asingeweza kubadilishwa na kuwa mtawala wa dola la wazawa.  Kama ilivyopangwa, utawala wa Wingereza ukala njama kwa kushirikiana na Sultani na kufanya hujuma kwenye chaguzi za kuelekea uhuru wa Zanzibar ili kuwezesha vyama vya kihifadhina, yaani Zanzibar Nationalist party (ZNP) na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) zishinde chaguzi katika hali ya kuunda serikali ya mseto yenye wingi kidogo tu wa ziada wa viti, bila kujali wingi zaidi wa kura ambazo chama cha ASP ndicho kilichopata.

Kutoridhika huku miongoni mwa Waafrika walio wengi kukasababisha mapinduzi yenye umwagaji damu miezi miwili baadaye.  Mnamo Januari 12, 1964 Chama cha Afro Shirazi Party kikaupindua utawala wa Sultani na kutangaza Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. 

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar zilihitimisha mazungumzo kwa kusaini mkataba wa Muungano Aprili 1964 zikunda Jamhuri moja huru (rejea Ibara (i) ya mkataba wa Muungano). 

Ukweli wa mambo katika jambo hili ni kuwa viongozi wa nchi hizi mbili walikutana kwanza kwa siri Zanzibar na kukubaliana kuziunganisha nchi zao kabla ya umma haujaelezwa kuhusu muungano huu. 

Mkataba wa Muungano ulisainiwa na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Zanzibar ,sheikh Abeid Amani Karume, Aprili 22, 1964 huko Zanzibar. 

Mkataba wa muungano baada ya hapo ukawasilishwa katika vyombo vya Kutunga Sheria katika nchi hizi mbili ili kuridhiwa (ratification). Uridhiaji wa Mkataba ulifanywa na vyombo vyote viwiliv ya Kutunga Sheria Aprili 26, 1964. (Angalia Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iitwayo Union of Tanganyika and Zanzibar Act,  ambayo ni sheria namba 22 ya mwaka 1964 (iliyotungwa na Bunge la Tanganyika kwa wakati ule) na pia Sheria ya Muungano wa Zanzibar na Tanganyika, iitwayo, Union of Zanzibar and Tanganyika Law, ambayo  ni Tangazo la Serikali Namba 243 (G.N. 243) la Mei 1, 1964, iliyotungwa na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar). 

Baadhi ya waandishi wamehoji kama kweli mkataba huu uliingiwa kwa uhuru usiotokana na shinikizo baina ya nchi hizi mbili (Rejea Issa G. Shivji, “Legal Foundations of the Union” , Dar es Salaam University Press (DUP), 1990); Wolfgang Dourado, The Consolidation of the Union na; Aboud Jumbe, The Partnership: Tanganyika-Zanzibar Union: 30 Turbulent Years, 1994).   Hoja inayotolewa na wale wenye msimamo kuwa mkataba huu haukufanywa kwa uhuru usiotokana na shinikizo ni kuwa Zanzibar haikuuridhia mkataba wa Muungano (Rejea Wolfgang Dourado, The Consolidation of the Union).

Dourado ambaye wakati wa kusaini mkataba wa muungano alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, ndiye aliyeibua  hoja ya jambo hili. Kulingana na maelezo ya Dourado, hakuna sheria yoyote iliyowahi kutungwa na mamlaka za Zanzibar kuridhia mkataba wa Muungano.

Shivji katika kupekua pekua kwake ndani ya Sheria za Zanzibar alibahatika kuliona Tangazo la Serikali namba 243 (G.N. 243) la Mei 1, 1964 lililochapishwa ndani ya gazeti la Serikali la Tanganyika (Tanganyika Gazette) na ambalo lilitolewa na Mwanasheria Mkuu. (Rejea Issa Shivji, “The Legal Foundations of the Union”). 

Ni kweli kwamba mkataba wowote wa kimataifa,  uwe katika maandishi ama ukiwa katika mdomo, ni lazima uwe umeingiwa katika hali ya uhuru usio na shinikizo na kwa nia njema.

Idhini isiyotokana na shiniko kwa pande zote mbili katika makubaliano ya kimataifa ni jambo lenye kuhitaji uhakika na msisitizo wa kiupekee. 

Uwepo wa lolote katika mambo yafuatayo utabatilisha mkataba: ulazimishanaji katika kufanya jambo (coercion), udanganyifu unaotokana na hila (fraud) au udanganyifu unaotokana na upotoshaji wa jambo ama kutokuweka jambo husika bayana (misrepresentation). 

Denis Maringo, aliyetafsiri makala haya ni Mwanasheria na alifundishwa sheria na Dk. Mvungi katika Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.  Anapatikana kwa simu: 0719270067. Barua-pepe: HYPERLINK "mailto:[email protected]"[email protected]

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles