


.jpg)
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania imecharuka na kueleza kuwa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limekuwa likifelisha wanafunzi wa imani ya dini hiyo.
Jumuiya na taasisi hizo zimemtuhumu Katibu Mtendaji wa Necta, Joyce Ndalichako na watendaji wengine wa baraza hilo kwa madai kuwa wamekuwa wakihujumu matokeo ya mitihani ya wanafunzi wa Kiislamu.
Aidha, wamelaani vikali uvunjaji wa heshima kwa kuchoma moto makanisa wakati wa vurugu zilizotokea visiwani Zanzibar ambapo zimeitaka serikali kuunda tume huru kutoka pande zote makanisa, serikali na kikundi cha Uamsho ili kuwapata waliohusika na uhalifu huo.
Kauli hiyo imetolewa jana kwenye mkutano wa kuzindua waraka wa maoni ya Waislamu katika mchakato wa katiba mpya uliowashirikisha Waislamu wa jiji la Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Baraza Kuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ramadhani Sanza, akizungumza katika mkutano huo alisema kila mwaka wanafunzi wa Kiislamu wamekuwa na matokeo mabaya hali inayotia mashaka kwamba yanachakachuliwa na Necta.
“Ufaulu mkubwa umekuwa ni kwa wanafunzi wa Kikristo huku wa Kiislamu wakionekana kufanya vibaya, tunajua huo ni mpango maalum unaofanywa na Necta wa kuwadidimiza kitaalum watoto wa Kiislamu na uislamu kwa ujumla,” alisema Sanza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Kiislamu Tanzania, Shabani Mapeyo, alisema Waislamu wanalaami vikali kuchoma moto makanisa wakati wa vurugu zilizotokea visiwani Zanzibar ambapo wameitaka serikali kuunda tume huru kutoka pande zote makanisa, serikali na kikundi cha Uamsho ili kuwapata waliohusika na uhalifu huo.
Mapeyo alisema kila upande uliohusika na kadhia hiyo kwa maana ya Wakristo, Waislamu na Serikali ushushe munkari na badala yake busara itumike ili kumpata muhusika wa uhalifu huo.
Mapeyo alisema atakayebainika kuhusika na jambo hilo achukuliwe hatua kali bila ya kujali wadhifa wake iwe katika chama, dini ama serikali.
“Fitina iliyopandikizwa baina ya Wakristo na Waislamu, Watanzania Bara na Wazanzibar zisipoangaliwa kwa umakini zinaweza kuvuka mipaka na kuenea nchi nzima na kuharibu hali ya nchi, hivyo ndugu zangu Waislamu tuwe makini tusije tukachokozwa na tukaingia katika vurugu hizo kirahisi,” alisema Mapeyo.
Naye Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, akizungumzia suala la sensa, alitaka iundwe tume huru ambayo inawashirikisha Waislamu na Wakristo kabla ya Juni 20 mwaka huu.
NIPASHE ilimtafuta Dk. Ndalichako juu ya madai hayo, alisema angezungumza na mwandishi wa habari hizi leo.