Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

TFF ibaki na waamuzi maalumu

5th May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Ligi kuu ya Bara iliyokuwa imalizike leo, sasa itafikia kilele cha msimu wa 2011-12 kesho baada ya shirikisho la soka, TFF, kusogeza mbele kwa siku moja mechi za mwisho.

TFF ilisogeza mbele kwa siku moja mechi za mwisho ili kuzipa Azam na Mtibwa Sugar muda wa chini kabisa kikanuni, wa kutosha, wa mapumziko kufuatia kurudiwa kwa pambano baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Taifa jana.

Azam na Mtibwa Sugar zilirudiana jana kufuatia uamuzi wa kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF ambayo ilibatilisha maamuzi ya Kamati ya Ligi ya kuipa Azam ushindi wa mabao matatu na pointi tatu wa pambano lililovunjika wiki iliyopita baina yao.

Wakati wapenzi wa soka wa Bara wakisubiri kwa hamu kukamilika kwa msimu mwingine wa ligi kuu ya Bara, ni vizuri kujikumbusha kwamba kwa mara nyingine utamu wa ligi kuu nchini uliathiriwa na maamuzi mengine mabovu mwaka huu.

Kwamba kwa mara nyingine utamu wa ligi kuu uliathiriwa na maamuzi mengine mabovu mwaka huu kuko wazi kiasi kwamba hatuna hata haja, Nipashe, ya kuorodhesha michezo ambayo ilikumbwa na malalamiko kutoka kwa makocha wa timu shiriki, mechi ambazo dakika 90 zake hazikwisha salama viwanjani au faini za jumla ya makumi ya mamilioni ambazo walitozwa wachezaji wa klabu mbalimbali ambao waliwafanyia vurugu waamuzi baada ya kukasirishwa na utendaji wao.

Lakini kielelezo cha kiwango cha hali duni ya mwisho ya maamuzi mabovu ni mchezo wa pili kati ya mitatu msimu huu baina ya Azam na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex uliomalizwa na muamuzi katika dakika ya 88 kwa maelezo kuwa wageni waligoma kuendelea na mechi.

Ni mchezo ambao umetufanya Nipashe tuone kuwa ingawa ligi kuu yetu na vyombo vinavyoisimamia bado ni vya ridhaa, upo umuhimu mkubwa kwa TFF kudokoa moja kutoka katika ligi kuu za kulipwa kwa ajili ya kunusuru soka la Bara.

Waamuzi wanaochezesha ligi kuu yetu ni wa ridhaa na hapajakuwa na dalili za kuanzishwa kwa fani ya uamuzi wa soka wa kulipwa, hilo linafahamika.

Lakini hali hiyo, Nipashe tunaona, bado haizuii TFF kupata waamuzi wenye uwezo wa kutosha kuchezesha mechi za ligi kuu ya Bara kwa kuiga mzingira yaliyo katika ligi kuu za kisasa.

Tungeishauri TFF kwamba badala ya kuendelea na mtindo wa kupokea na kutumia orodha yenye jina la kila muamuzi mwenye HADHI ya kuchezesha mechi za ligi kuu ya Bara, shirikisho hilo sasa lichekeche utitiri huo kwa lengo la kupata majina machache ya waamuzi wenye UWEZO wa kuchezesha ligi hiyo.

Hawa wenye uwezo, tunaamini, watapatikana tu kwa kuangalia ripoti za waamuzi, makamisaa na wakuu wa vituo vya ligi kwa miaka miwili-mitatu iliyopita ili kuwabaini.

Haiwezekani pakawa na waamuzi wapya kila msimu na bado TFF ikataraji kiwango cha uchezeshaji wa mechi za ligi kiwe juu.

Na haiwezekani kiwango cha uamuzi nchini kikaendelea kudidimia msimu hata msimu na bado TFF ikataraji mashabiki waendelee kufurika viwanjani kutazama mechi ambazo zinaharibiwa na maamuzi mabovu hayo.

Imeonywa na matukio, TFF, tunaamini: kwamba ni wakati wa kubadili mfumo wa kupata waamuzi wa mechi za ligi kuu ili si tu kiwango cha uchezeshaji kiendane na matarajio ya viongozi wa timu, makocha, wachezaji na mashabiki wa mchezo wenyewe bali pia matokeo ya uwanjani yaendane na kiwango ambacho watazamaji wanakishuhudia katika mechi kwenye msimu husika wa ligi kuu ya Bara.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles