Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

`Big Brother Africa` ukiukwaji mtupu wa maadili 

20th May 2012
Print
Comments

Mtu wa kwanza kujitokeza hadharani na kutangaza kupinga shindano la kuishi katika jumba lililotengwa maalum, maarufu kama 'Big Brother Africa' (BBA), alikuwa ni aliyekuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi.

 Dk. Nchimbi, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alilipinga shindano hilo Agosti 12, mwaka jana, alipokuwa akihitimisha bungeni hoja ya bajeti ya wizara aliyokuwa akiiongoza wakati huo.

 Alisema kipindi kinachorusha hewani shindano hilo ni kero na serikali haikiungi mkono.

 Wakati tukiitafakari kauli hiyo ya Dk. Nchimbi, pengine hapa ningeelezea japo kwa uchache ‘Big Brother Afrika’ ni kitu gani. Hiyo ni kutokana na sehemu kubwa ya watu kutoifahamu.

 ‘Big Brother Africa’ ni jina lililopewa shindano ambalo washindani huishi katika jumba maalum na kujitahidi kukwepa kung’olewa na watu wanaofuatilia moja kwa moja shindano hilo kwenye televisheni kutokana na upungufu wanaouonyesha. 

Mtu wa mwisho kubaki katika jumba hilo, huzawadiwa fedha nyingi na kwa taarifa sahihi, zawadi inayoshindaniwa mwaka huu, imetangazwa kuwa ni Dola za Marekani 300,000 sawa na Sh. milioni 480 za Tanzania.

 Shindano hilo huonyeshwa moja kwa moja (Live) kwenye televisheni. Huonyesha hadi vitendo vinavyofanywa na washiriki wanaume kwa wanawake wanapokuwa katika vyumba vyao vya kulala ndani ya jumba hilo. Katika kila kona ya jumba hilo, kumefungwa kamera.  

Katika shindano la mwaka huu, imeelezwa kuwa kuna kamera 53. Nyingine zimefungwa hadi chooni, bafuni na na vipaza sauti 120 kwa ajili ya kutoa usikivu mzuri hata pale washiriki wanapoamua kunong’onezana. 

Shindanio hilo linaelezwa kuwa lilianzishwa kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini na kampuni ya kutengeneza na kuuza televisheni duniani ya Endemol yenye makao yake makuu, jijini Amsterdam, nchini Uholanzi.  

Inaelezwa kuwa shindano la kwanza lilianza Jumapili ya Mei 25, 2003 likijumuisha nchi 12 za Afrika, ikiwamo Tanzania liliporushwa kwa televisheni moja kwa moja katika nchi 42.

 Shindano hilo linafanyika kwa mara ya saba mwaka huu na Tanzania ikiwa mshiriki kwa miaka sita mfululizo.

Ndilo shindano pekee barani Afrika linaloonekana 'Live' kwenye televisheni kwa saa 24 ndani ya miezi mitatu na kutazamwa na watu katika nchi 47.

 Nikirejea kwenye kauli ya Dk. Nchimbi, nadhani sitakuwa nimetenda haki kama sitatumia fursa hii kumpongeza kwa dhati waziri huyo. 

Hiyo ni kutokana na ujasiri mkubwa aliouonyesha hadharani kwa kuthubutu angalau kutoa tu kauli ya kupinga shindano hilo. 

Kuthubutu kwa Dk. Nchimbi kunathibitisha namna waziri huyo anavyojali, kuthamini na kulinda maadili ya Kitanzania. Ana kila sababu za kupinga shindano hilo.

 Zipo sababu nyingi za shindano hilo kutokukubalika. Kubwa ni kuwa na mambo yanayokiuka maadili ya Kitanzania. 

Hapa nafasi haitoshi. Ningetoa mifano lukuki kuthibitisha dai hilo.

 Mfano wa haraka haraka, ni kile kitendo cha mshiriki wa BBA kukubali kupigwa picha na waandaaji wa shindano na kurushwa hewani akiwa uchi wa mnyama, iwe chooni, bafuni, kitandani au anapokuwa anafanya ngono. 

Maadili ya Kitanzania yanatokana na mila na desturi za makabila zaidi ya 120 ya Tanzania.

 Mila na desturi hizo, zinatoa mafunzo yanayotofautiana kwa kiasi kikubwa mno na mambo yanayostahili kufanywa na wanyama ambayo hutendeka katika jumba la BBA. 

Katika makabila mengi ya Kitanzania, masuala yanayohusiana na mambo ya faragha, yamewekewa utaratibu maalum, ambao hutenganisha makundi mbalimbali katika jamii kama vile watoto, wanawake na wanaume.

Si jambo la kawaida katika mila na desturi za Kitanzania kukuta wanaume na wanawake katika shughuli za unyago au jando wakiwa wamechanganyika.  

Shindano la BBA halizingatii utaratibu huo. Yaliyomo, kuanzia mchanganyiko hadi mavazi ya washiriki, vyote ni vya Kimagharibi. Havina haya, staha wala aibu! 

Vilevile, katika utazamaji wa hilo shindano kupitia televisheni, hakuna ilani inayotolewa kwa watazamaji, kama ilivyo kwa baadhi ya vipindi vinavyozingatia mila na maadili, ambavyo hutenganisha vipindi vinavyostahili kuangaliwa na watoto na wazima. 

Katika BBA watu wote bila kujali rika wanaruhusiwa kuangalia shindano wakati wowote!  

Uoneshaji hauzingatii mila na desturi za Kitanzania. Unalenga makundi yote katika jamii, wakiwamo watoto.

 Nina kila sababu ya kuungana na Waziri Nchimbi. Kusema shindano la BBA halifai. Limetawaliwa na ukiukwaji wa maadili ya Kitanzania. 

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles