Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tulinde, tusafishe  makazi ya wafu wetu

1st May 2012
Print
Comments

Kuna mambo mawili nilitamani kuongea leo kuhusu makaburi. Jambo la kwanza ni ongezeko la watu katika jiji la Dar es Salaam sambamba na ongezeko la vifo huku mahala pa kuzikia wafu wetu pakizidi kukosekana na suala la pili linahusu uchafu katika makaburi.

Hilo la ufinyu wa makaburi nitalizungumzia siku nyingine kama si wiki ijayo, lakini leo imenipendeza tukumbushane kuhusu usafi wa mahala hapa (makaburini) tunakozika baba zetu, mama zetu, kaka zetu, dada zetu watoto wetu na wadogo zetu.

Katika moja ya imani za kidini ni kwamba makaburi ni sawa na nyumba hizi tunazoishi na ndio maana mafundisho ya dini hiyo yanasema kwamba mtu ukipita makaburini inabidi kuwatolea salamu waliolala katika ‘nyumba’ hizo, ukiwaombea huruma ya Mwenyezi Mungu na kuwaambia kwamba wao wametangulia na Mungu akipenda siku moja, inshallah, na wewe utaungana nao.

Kwa mujibu wa imani hiyo, hata kama wewe ulio duniani kwa sasa husikii lakini wafu wanakusukia. Imani nyingine huyaita makaburi kuwa ni ‘Shamba la Bwana’.

Lakini shamba hili ama nyumba hizi, tumeshindwa kuzingalia ipasavyo. Hatuzitunzi na kuzifanyia usafi ipasavyo, yaani tumesahau kwamba hata sisi ambao leo tunajivuna na kujiona wajanja kwenye huu mgongo wa dunia, kesho tutapelekwa huko huko kwenye mashamba hayo ya Bwana.

Mashamba haya ama nyumba hizi tumezigeuza kuwa dampo, zimegeuka kuwa mahala pa vibaka kujificha na kuviziana kwa lengo la kuporana na wengine wamezigeuza mahala pa kufanyia mambo ya hovyo kama vile uchawi na hata uzinifu. Nimekuwa ninajiuliza kwa nini tumejisahau kiasi hiki?

Kwa wanaokumbuka, wiki kadhaa zilizopita niliandika hapa kuhusu habari ya ndugu zangu fulani kugombea maiti katika visa viwili vinavyofanana fanana. Nikasema kwamba mmoja wa marehemu hao kabla hajafariki dunia ni wachache waliofuatilia tiba zake hospitalini, wakajali kula kwake na mahitaji mengine muhimu kwa mgonjwa lakini alipofariki dunia akawa ‘dili’,  kila mmoja anamtaka!

Ambacho sikusema siku ile ni kwamba maiti huyo, tulikwenda kumzika katika makaburi ya Kinondoni. Ingawa, alhamdulillahi, siku hizi makaburi hayo yamezungushiwa ukuta, lakini tulikuta bonge la msitu, hususan upande wa makaburi ya Waislamu tulikomzika bibi huyo.

Baada ya kumaliza kuzika, mzee mmoja aliyepewa nafasi na wanandugu kutoa salamu, alilalamika sana kuhusu hali ile ya  kuacha makaburi yakageuka kuwa msitu hatari.

“Ni nani kati yetu anaweza kuapa kwamba ataishi milele na hatarajii kuzikwa mahala hapa ama pengine panapofanana na hapa. Kwa nini tunaacha makaburi yanakuwa katika hali hii? Makaburi yanageuka kuwa msitu ambamo simba, fisi ama chui wanaweza kuishi!”

Akawa analalamika yule mzee na kushauri vijana na wazee kujitokeza kwa ajili ya kuyafanyia usafi makaburi hayo.

Kwa vile sijatembelea hayo makaburi (mimi ninaishi Temeke), sina hakika kama wahusika walishakutana kama walivyoahidi na kuyafanyia usafi makaburi hayo.

Kabla ya hapo, ninakumbuka siku moja nilipita maeneo ya Mabibo Luhanga nikaona kikundi cha vijana wakisafisha makaburi yaliyo jirani na kituo kidogo cha polisi eneo hilo. Nadhani ilikuwa ni hatua nzuri na nilitamani kuingia pale nishirikiane nao kuonyesha ninavyowaunga mkono, lakini haraka niliyokuwa nayo ilinifanya nishindwe kuungana nao. Baadaye nilijilaumu pia kutowapiga hata picha na kuitoa kwenye gazeti pengine ikawa sababu ya kuwahamasisha watu wengine kufuata nyayo hizo.

Hivi karibuni pia nilipita karibu na makaburi ya Mwananyamala, pale jirani na hospitali nikashangaa kwa jinsi palivyobadilika. Kumbukumbu zangu wakati ninapita hapo siku za nyuma zilionyesha kwamba makaburi hayo yalikuwa yamgeuzwa kuwa dampo kubwa lililokuwa linatoa harufu mbaya, lakini haya yalikuwa masafi kweli kweli na niliona kama yanazungushiwa uzio. Nilipouliza nikaambiwa kwamba ni vijana fulani ambao waliamua kuyasafisha na ndio wanaweka huo uzio. Nilifurahi sana, nikawapongeza na ninawaombea dua.

Nimeandika makala haya ili kuhamasisha watu wengine; kuanza kujenga tabia ya kusafisha na kulinda makaburi. Nimegundua kwamba baadhi ya watu wanaoishi jirani na makaburi ndio wenye tabia hizi za kugeuza makaburi kuwa jalala la kutupa takataka zao. Ninawaomba tukome tabia hii kwa sababu hizi ni nyumba zetu sote. Hakuna kiumbe anayeweza kutamba kwamba siku moja hatakuwa ‘mpangaji’ katika nyumba hizo.

Kubwa zaidi ni watu kila mtaa, kila kijiji na kila mji kujikusanya na kutenga siku moja kwa wiki ama hata kwa mwezi kwa ajili ya kufanyia usafi makaburi na hata maeneo mengine kama vile mitaro na kadhalika.

Shime Watanzania wenzangu, tujenge tabia ya kuendekeza usafi huku tukiupiga vita uchafu na wachafu.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles