Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Royal Mirage yamsaidia mama wa watoto wenye vichwa vikubwa

12th May 2012
Print
Comments
Mkurugenzi wa Hoteli Hoteli ya Royal Mirage Amir Esmail akimkabidhi msaada wa Shilingi 200,000 Sofia Rashid kwa ajili ya kuwahudumia watoto wake wawili wanaosumbuliwa na matatizo ywa vichwa vikubwa. Katikati ni Issa Mohamed Said Jumbe wa NEC ya CCm

Hatimaye kilio cha Sofia Rashidi (22) mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam kimesikika baada ya Uongozi wa Hoteli ya Royal Mirage kumpatia  msaada wa fedha na chakula kwa ajili ya watoto wake wawili wenye matatizo ya kuwa na vichwa vikubwa.

Msaada huo alikabidhiwa jana na Mkurugenzi wa Hoteli hiyo Amir Esmail ambapo alisema ameamua kutoa msaada wenye Shilingi 500,000 ikiwemo pesa taslimu 200,000 kutokana na kuguswa na matatizo ya watoto hao.

Wiki iliyopita Gazeti hili ilitoa habari ikielezea mkasa wa Sofia ambaye amelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) baada ya kuzaa watoto wawili Omar Mohamed (4) na maulidi Mohamed (miezi minne) wakiwa na matatizo ya vichwa vikubwa.

Esmail alisema mara baada ya kuona habari za kusikitisha zinazomhusu mwanamke huyo aliamua kutoa mchango wao huo kwa ajili ya kusukuma maisha ya watoto hao pamoja na mama yao.

"Kweli tumesikitishwa sana na tatizo lilomkuta Sofia, tumeamua kama wafanyakazi wa Royal Mirage kutoa msaada wetu ili angalau aweze kuwahudumia watoto hawa," alisema Esmail.

Alisema hoteli yake iliyopo eneo la Kariakoo makutano ya mtaa wa Jamhuri na Amani inamilikiwa na Watanzania na inawajibu mkubwa wa kusaidia jamii pale wanapohitaji msaada.

Esmail alisema pamoja na kutoa msaada huo wanaangalia uwezekano wa kuwanunulia watoto hao kiti maalum cha kutembelea ili kumuwezesha mama yao afanye kazi zingine mara atakaporuhusiwa wodini.

"Si jambo zuri wageni waje kutusaidia hata kwa matatizo yetu, tumeanza naomba na watu wengine wajitokeze kumsaidia mama huyu anayetaabika hapa Hospitalini," aliongeza kusema.

Hata hivyo, Sofia alimshukuru Mkurugenzi hayo kwa kumpatia msaada huo ambapo alisema atautumia kwa ajili ya kununua mahitaji muhimu ya watoto wake hao.

Kabla ya tukio hilo Afisa Uhusiano Msaidizi, Mary Ocheng alisema tayari watoto Omar na maulid wamefanyiwa upasuaji kwa ajili ya kutoa maji kwenye vichwa vyao na hali zao zinaendelea vizuri.

Alisema kabla ya kufanyiwa upasuaji watoto hao walikuwa wanashindwa kutazama lakini kwa sasa wameanza kufumbua macho baada ya upasuaji huo kuwa wa mafanikio.

Hata hivyo, alisema bado Sofia anakabiliwa na tatizo la sehemu ya kuishi mara atakapopewa ruhusa kutokana na mume wake kumfukuza akimtuhu anazaa watoto wa ajabu.

Alisema baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo wamepokea misaada ya fedha na vitu mbalimbali kutoka kwa watu waliotuma kupitia ofisini kwake na gazeti la Nipashe.

Awali alikaririwa Sofia akisema watoto wake wote walizaliwa wakiwa na maradhi hayo ambapo walipofikia miezi miwili walianza na tatizo la kichwa kukua kwa haraka na kusababbisha ashindwe kuwabeba.

Sofia alisema kwamba kutokana na matatizo ya watoto wake, mume wake aliyemtaja kwa jina la jina moja la Mohamed alimpa talaka kwa madai hawezi kuishi nae kwa sababu anazaa watoto wa ajabu.

Alieleza toka apewe talaka baba wa watoo hao hajakwenda kumjulia hali wala kumpatia huduma muhimu kwa ajili ya watoto hao.

"Inaniuma sana nikiona hali hii, mimi sikupenda kuzaa watoto hawa ila Mungu amepanga, lakini mwenzangu ananiona kama mimi ndiye mwenye tatizo na kuamua kuniacha," alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha wazazi wa watoto wenye vichwa vikubwa nchini, Abdul Hakim kugundulika kwa Sofia na watoto wake ni kazi iliyofanywa na viongozi wa chama hicho baada ya kusikia habari zake na watu wanaomfahamu.

Alisema kwa ujumla maisha ya mama huyo na watoto yake yalikuwa ya mateso kutokana na kuishi katika kibanda kimoja cha nyasi ambapo inaponyesha mvua hawakuwa na sehemu ya kukimbilia kujihifadhi.

"Maisha yake ni mabaya mno tumemtoa katika nyumba ya nyasi na ilimbidi kunyeshewa na mvua yeye na watoto wake baada ya nyumba aliyokuwa akiishi nyuma na mume wake kufukuzwa," alisema Hakimu
Kwa mtu yoyote anayetaka kumsaidia Sofia  anaombwa kufika katika Ofisi ya Uhusano wa MOI au awasiliane na mwandishi Moshi Lusonzo kwa simu No 0717336368 kwa taarifa zaidi.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles