Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Simba yaondoka leo, Okwi atamba

9th May 2012
Print
Comments
Emmanuel Okwi

Wawakilishi pekee wa Tanzania waliobaki kwenye mashindano ya kimataifa, Simba, wanaondoka nchini leo na kuelekea jijini Khartoum, Sudan kwa ajili ya mechi yao ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya klabu ya Al Ahly Shandy itakaofanyika Jumapili usiku mjini Shandy huku mshambuliaji wake aliye kwenye kiwango cha juu, Emmanuel Okwi, akisema Simba iko kikazi zaidi.

"Tumedhamiria na tunakwenda Sudan kumalizia kazi, ila bado safari yetu ni ngumu," alisema Okwi.

Akizungumza na NIPASHE jana mchana, Okwi ambaye ni raia wa Uganda alisema kuwa wachezaji wote wa Simba wanataka kuona mafanikio na huu ndio mwaka wao wa kuieletea heshima klabu na nchi.

Okwi alisema kuwa uwezo wa kila mchezaji na mafunzo ya kocha wao, Mserbia Milovan Cirkovic ndio siri ya matokeo mazuri msimu huu na wanaamini kuwa watasonga mbele kwenye mashindano hayo ya Afrika.

"Tunajua jukumu letu, kila mmoja anataka kupata mafanikio zaidi, hatujaridhika bado, ila tunaomba dua zenu ili tukafanye vizuri huko Sudan," Okwi aliongeza.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu', aliliambia gazeti hili kuwa wachezaji 20 na viongozi nane wataondoka leo saa 9 Alasiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.

Kaburu alisema kuwa maandalizi ya safari hiyo yamekamilika na aliwataja wachezaji wanaoondoka kuwa ni pamoja na Juma Kaseja, Ally Mustapha 'Barthez', Amir Maftah, Shomary Kapombe, Obadia Mungusa, Kevin Yondani, Patrick Mafisango, Uhuru Suleiman, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Okwi, Haruna Moshi 'Boban' na Edward Christopher.

Aliwataja wachezaji wengine ni Salum Machaku, Jonas Mkude, Gervais Kago, Derick Walulya, Abdallah Seseme huku wanaobaki wakiwa ni Ulimboka Mwakingwe, Nassor Masoud 'Chollo', Juma Nyosso, Hassan Thabit, Frank Sekule na Ramadhan Singano 'Messi'.

Simba inaondoka ikiwa na faida ya magoli 3-0 waliyoifunga Al Alhy Shandy kwenye mechi ya kwanza iliyofanyika Aprili 29 jijini Dar es Salaam na kumbukumbu nzuri ya ushindi mnono wa magoli 5-0 ilioupata dhidi ya watani zao Yanga katika mechi ya funga dimba ya Ligi Kuu ya Bara Jumapili.

Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeitakia kila la kheri timu ya Simba kwenye mechi yake hiyo ya marudiano.

Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa mkuu wa msafara wa timu hiyo leo atakuwa ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo, Hussein Mwamba.

Wambura alisema kuwa Simba inatarajia kurejea nchini Jumanne ya Mei 15 na pia TFF imeipongeza Simba kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara msimu wa 2011/2012 ambayo ilimalizika Jumapili iliyopita.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles