Sunday May 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Hali ngumu kwa Wastaafu isigeuzwe Siasa!

22nd July 2012
Print
Comments

Kuna baadhi ya kauli ambazo zikisemwa katika mtazamo wa kisiasa hazileti athari yoyote kwa jamii, tofauti na linapoongelewa suala la nyongeza za maslahi ya mfanyakazi aliyestaafu kazi serikalini na hatimaye ahadi hizo kuwa kama siasa na zikawa vigumu kuzitekeleza.

Wastaafu wasiwekwe kama kigezo cha kutolea mifano ya hali ngumu ya maisha na kwamba zipo jitihada za kuongeza mafao yao tofauti na utekelezwaji wa ahadi kama hizo ambazo zimekuwa zikitolewa katika kila bajeti ya kila mwaka.

Wakati mwingine unaweza kushindwa kupata uhalisia wa namna mamlaka inayohusika na wastaafu wa serikali inavyofanya kazi bila kuonyesha uadilifu! Yapo maeneo yanayodhihirisha kuwa wastaafu wanaonekana kuwa kama kero na mzigo kwa serikali, na hasa inapojitokeza kudai nyongeza ya mafao au haki nyinginezo.

Wahusika wakuu, ambao ni Wizara ya Fedha huunda majibu mazuri kwa nia ya kutaka kama kuwatoa barabarani wastaafu, wanachoambiwa wastaafu ni kufanya subira wakati serikali inajipanga kukusanya mapato zaidi, kwamba hali ya uchumi haijaruhusu kutoa nyongeza kwa kipindi hicho. Wakati wakijua kuwa hizo ni sawa na porojo tu au siasa.

Serikali inafahamu kuwa nguvu kazi kubwa ya wastaafu iliyoko huko mitaani ni kioo cha tafsiri ya namna serikali ilivyo, kama hali ngumu ya wastaafu itokanayo na mafao madogo wayapatayo ambayo hayakidhi hata nusu ya mahitaji ya lazima kwao, basi hiyo ni tafsiri ya namna serikali isivyowajali wastaafu wake ambao kwa hakika ndiyo nguvu kazi ya akiba katika nyanja mbalimbali za maendeleo ya taifa.

Ni dhahiri kuwa serikali bado inawahitaji wastaafu wake, na ndio maana wakati wa hali za dharura zinapojitokeza kitaifa, dharura kama za migomo ya madaktari, walimu, wahandisi nk. serikali huwaita wastaafu kuziba mapengo hayo na kuendelea kutoa huduma inayostahiki, ni wakati huo tu ambapo wastaafu huonekana kupewa heshima, ni wakati huo wanapopewa majukumu mengine muhimu bila kujali kama wapo katika hali ngumu ya maisha baada ya kustaafu.

Serikali inalo kundi la wastaafu wa taaluma mbalimbali, wapo walimu, wahandisi, wanasheria, madaktari, wanajeshi nk. makundi hayo yote yana umuhimu sawa kwa mwajiri wao ambaye ni serikali, na wanastahili kuhudumiwa ipasavyo na serikali. Huduma hiyo ni kwa njia ya malipo ya pensheni ambaypo kwa sasa hutolewa kila baada ya miezi mitatu. Fedha hizo za pensheni ni kidogo sana, hazikidhi haja ya matumizi muhimu kwa familia za wastaafu hao.

Katika kikao cha Bunge kinachoendelea sasa, Naibu Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mji Mkongwe, Muhammad Ibrahim Sanya (CUF) aliyetaka kujua kama serikali inafahamu kuwa wastaafu wengi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania wanaishi katika hali ngumu ya maisha, Mheshimiwa Waziri Saada alikiri kwa dhati kuwa wastaafu wengi wa Jeshi hilo wana hali ngumu ya maisha.

Aidha Mbunge huyo alitaka kujua kama ni kitu gani kinachozuia serikali kupandisha pensheni za wastaafu hao kila mara wanapopandisha vima vya chini vya mishahara ya wafanyakazi wake.

Waziri alikiri kuwa kiwango cha chini cha pensheni cha Sh. 50,114/- kwa kila mwezi kwa mstaafu kinacholipwa na serikali ni kidogo kulingana na hali halisi ya maisha yalivyo sasa. Akaongeza kuwa kutokana na serikali kulitambua tatizo hilo, itaendelea kuongeza kiwango cha pensheni kwa wastaafu wote kwa kadri ya mapato ya nchi yatakavyoruhusu. Kwa uzoefu wa suala la mapato 'kuruhusu', hiyo ni siasa tu kwani haitatokea serikali kuwa na mapato yatakayoruhusu kwa mfumo huo.

Ipo siasa ndani yake katika ahadi kama hizo, kwani ni mara ngapi serikali imeongeza mishahara ya wafanyakazi walioko serikalini bila kuwaangalia wastaafu? Mara ya mwisho nyongeza ya mafao kufanyiwa marekebisho madogo ilikuwa mwaka 1998, ni miaka minne sasa. Naibu Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum anasema serikali itaendelea kuongeza kiwango cha pensheni....maana yake ni kuwa serikali imekuwa ikitoa nyongeza ya pensheni hiyo kwa wastaafu kila inapopandisha mishahara kwa wafanyakazi wake, hali ambayo si kweli, hizo ni siasa tu.

Wastaafu wengi wanangojea kupokea mafao yao ya kila baada ya miezi mitatu ifikapo mwishoni mwa mwezi huu, na kwa baadhi ya wastaafu wanaofuatilia hotuba za waheshimiwa huko Bungeni, wameshajua nyongeza ya mishahara ilivyopangwa kutolewa na serikali kuanzia mwaka huu wa fedha, na kwa kadri Naibu Waziri wa Fedha alivyojibu swali la Mbunge wa Mji Mkongwe Muhammad Ibrahim Sanya, wastaafu sasa wanasubiri kuona nyongeza ambayo itaongezwa sambamba na nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma.

Wastaafu wanajua kwa dhati kuwa wakikosa nyongeza ya pensheni katika Bajeti inayoendelea safari hii, basi majaliwa yao labda mwaka mwingine ujao wa fedha wa 2013/14.

Wastaafu wanafahamu majukumu mazito yanayoikabili serikali kiuchumi, na hasa kutokana na madai mbalimbali ya nyongeza za malipo kutoka taasisi nyingine za watumishi wa umma ambayo baadhi yanatishiwa kwa migomo pamoja na maandamano.

Wastaafu wengi pia wanafahamu hali halisi ya uchumi wa nchi, lakini bado wastaafu ni moja ya kundi linalowajibika kwa serikali yao, wastaafu hawana pa kukimbilia, na wastaafu wengi ni wastaarabu, wanaelewa ukomo wao katika kufuatilia haki zao za msingi. Wanaomba masuala ya nyongeza katika pensheni zao yasiongelewe kama siasa, yawekewe mikakati mahsusi na kuyatekeleza.

Maoni: 0715-047304 na

0762-233116

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment