Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kwa nini serikali inashindwa kufufua ICU Zanzibar?

18th March 2012
Print
Comments

Kitengo cha huduma za dharura kwa wagonjwa Mahututi (ICU) ni muhimu katika hospitali yoyote hasa ya rufaa, ili kuokoa maisha ya mgonjwa anayehitaji msaada apumue ipasavyo.

Moja ya hospitali zilizo katika hitaji kuu la ICU ni ile ya rufaa ya Mnazi mmoja kisiwani Zanzibar, ambao kwa takribani miaka miwili sasa, huduma za kitengo hicho zimezorota na kuathiri hali za wagonjwa.

Tatizo hilo limetokana na mashine tano zilizopo hospitalini hapo zinazotumika kuwasadia wagonjwa waliyopoteza fahamu kuharibika.

Hospitali hiyo ni mfano wa mkombozi kwa wananchi wa Zanzibar hasa masikini wasiyokuwa na uwezo wa kusafirishwa nje ya nchi au kumudu gharama za matibabu katika hospitali za binafsi zilizo ndani na nje ya visiwa hivyo.

Wagonjwa wanaolazwa katika hospitali hiyo wanatoka katika hospitali za mikoa mitano ya Zanzibar kwa vile hospitali hiyo ni kituo kikuu cha madaktari bingwa wa maladhi ya aina mbali mbali.

Kutotengenezwa mashine hizo kumeibua mjadala mkubwa kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ambao kwa zaidi ya mwaka mmoja wamekuwa wakipigia kelele tatizo hilo wakati wa mijadala ndani ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar (BLW). Bila shaka hakuna mafanikio.

Wawakilishi hao wakiongozwa na Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub, wanasema kukosekana kwa huduma hizo, kunawaathiri zaidi wananchi wanyonge ambao hawana nguvu za kiuchumi za kumudu gharama za matibabu nje ya nchi au hospitali za binafsi.

Hata hivyo, Wizara ya Afya Zanzibar katika mwaka wa fedha 2011/2012 haikutenga fedha za kufanyia matengenezo wala kununua mashine mpya kutokana na umuhimu wake.

Waziri wa Afya wa Zanzibar, Juma Duni Haji, anasema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ipo mbioni kuondoa tatizo hilo kwa kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambayo imeonyesha nia ya kusaidia kujenga ICU mpya katika hospitali hiyo.

Hatua ya China kuisadia SMZ kuondoa tatizo hilo inastahili kuungwa mkono na kupongezwa hasa kwa kuzingatia (China) imekuwa mstari wa mbele kusadia Zanzibar katika kuimarisha huduma za afya.

Duni anasema Shilingi milioni 800 zinahitajika kuondoa tatizo hilo kama gharama za kununua mashine mpya za kusadia wagonjwa mahututi katika kitengo hicho, lakini serikali inakabiliwa na ufinyu wa fedha kwenye bajeti yake.

Baada ya tatizo hilo kuripotiwa na vyombo vya habari mwaka jana, kampuni mbili kutoka mikoa ya Arusha na Dar es Salaam, ikiwemo ‘Gillya Electronics and General Supply LTD’ zilijitokeza na kueleza kuwa zina uwezo wa kutengeneza mashine hizo, huku kampuni hiyo ikitaja jumla ya Sh Shilingi milioni 45 za kugharamia shughuli hiyo.

Lakini wizara imeshindwa kutumia fursa hiyo kuondoa tatizo hilo. Kutokana na tatizo hilo wagonjwa waliyopoteza fahamu wamekuwa wakilazwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi katika wodi hiyo kama kuwapa mazingira ya utulivu bila ya kuwepo huduma muhimu za kuokoa maisha yao.

Wodi ya ICU imekuwa kama gereji ya magari kutokana na madaktari bingwa kulazimika kutumia mitungi ya gesi kusadia wagonjwa kupumua tangu kuharibika kwa mashine hizo.

Machi 14 mwaka huu aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Bububu, Salum Amour Mtondoo, alilazimika kuhamishiwa katika wodi hiyo baada ya kulazwa siku tano na kusumbuliwa na maladhi ya shinikizo la damu, sukari na malaria kabla ya kufariki Machi 15 mwaka huu.

Madaktari bingwa katika hospitali hiyo wanasema shinikizo la damu lilikuwa limepanda kwa asilimia 180 na kulazimika kuwekewa mtungi wa gesi ya Oksijeni kujaribu kumsadia kupumua kutokana na tatizo hilo.

Wajumbe watatu wa Baraza la Wawakilishi walilazimika kufanya kazi usiku ya kupandisha ghorofani mitungi ya gesi baada hali ya mwenzao kuwa mbaya na kulazimika kulazwa katika wodi hiyo.

Pamoja na serikali ya China kutoa ahadi ya kujenga ICU mpya, bado SMZ inawajibika kuchukua hatua za haraka kuhakikisha mashine hizo zinafufuliwa ili kuokoa maisha ya wananchi wake.

Aidha wakati umefika kwa wataalam wa mipango Zanzibar kutoa vipaumbele kwa kuangalia umuhimu wake kwa jamii, ili kuondoa matatizo kama hayo kujitokeza na kuathiri maisha wananchi wake.

Serikali makini haiwezekani ikashindwa kupata Shilingi milioni 800 kwa zaidi ya miaka miwili za kununua mashine mpya au Shilingi milioni 45 za kufufua mashine zilizoharibika kwa manufaa ya wananchi Zanzibar.

Tatizo la wataalam wa mipango kutokuwa na vipaumbele ndiyo maana tunashuhudia serikali, kwa mfano ikinunua magari ya kifahari kama Toyota Prando wakati wanafunzi wakikaa kwenye sakafu darasani ama mashine za ICU zikiwa zimeharibika kwa zaidi ya miaka miwili.

Kama serikali inaweza kutumia zaidi ya Shilingi bilioni moja kila mwaka kuadhimisha sherehe za Mapinduzi inashindwa vipi kufufua mashine za ICU kwa manufaa ya wananchi wake?

Wakati umefika kwa wataalam wa mipango Zanzibar kuangalia vipaumbele wanapopanga mipango ya maendeleo katika kila mwaka wa bajeti pamoja na kuthibiti vitendo vya wafanyabiashara wakubwa kukwepa kodi Zanzibar, ili fedha inayopatikana itumike katika kuimarisha huduma za afya na elimu kwa wananchi wa Zanzibar.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles