Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Yanga haijachukuliwa na wazee - Nchunga

30th April 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga

Uongozi wa Yanga umekanusha kauli iliyotolewa na Wazee wa Klabu hiyo kuwa wamekabidhiwa timu na badala yake imesema kuwa kikosi cha timu hiyo bado kiko mikononi mwao na kesho kitaingia kambini Kibaha mkoani Pwani kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya watani, Simba.

Juzi Wazee wa klabu hiyo wakiongozwa na Katibu wa kundi hilo, Ibrahim Akilimali walitangaza kukabidhiwa timu na uongozi kutokana na walichokiita kuwepo kwa hali ya hewa 'chafu' ndani ya klabu yao ambayo ndio imesababishwa kupoteza ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu.

Akizungumza jana kwenye makao makuu ya klabu hiyo, Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, alisema kuwa mazungumzo ya kuwakabidhi Wazee hao timu yalishindwa kufikia muafaka baada ya kundi hilo kushindwa kuweka wazi ni wapi litapata fedha za kuiendesha timu endapo watakabidhiwa.

Nchunga alisema pia uongozi wake ulikataa kuwakabidhi timu Wazee hao baada ya kushindwa kuweka wazi ni nani atawapa fedha za kuendesha timu na hivyo wakaona ni vyema kuendelea kuiongoza kwa sababu wao ndio wenye jukumu hilo kama walivyochaguliwa na wanachama kwenye uchaguzi.

"Timu bado iko chini yetu, hatujaikabidhi kwa Wazee kwa sababu wameshindwa kuweka wazi ni jinsi gani wataweza kuihudumia timu," alisisitiza Nchunga.

Mwenyekiti huyo alisema pia uongozi wake umeridhia maamuzi ya aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Seif Ahmed 'Magari' kujiuzulu nafasi hiyo lakini ikikataa maamuzi ya kujiuzulu yaliyofikishwa kwao na mjumbe mwingine, Abdallah Binblek.

Aliongeza kuwa kutokana na maamuzi hayo nafasi ya Seif na nyingine zilizowazi zitajazwa hapo baadaye na sasa akili yao inaelekezwa kwenye mechi yao dhidi ya Simba, usajili na katika mashindano ya Kombe la Kagame yanayotarajiwa kuanza kufanyika hapa nchini Juni 23 ambapo Yanga ni mabingwa watetezi.

Alisema pia huu ni wakati wa wanachama wa Yanga kutulia kwa sababu hakuna ambaye anapenda kuona timu inafanya vibaya.

Yanga inajipanga kuhakikisha inalinda heshima yake kwa kuifunga Simba iliyoko kwenye changamoto ya kutwaa ubingwa wa Bara msimu huu ambao pia unawaniwa na Azam.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles