Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Msekwa ang’aka

2nd June 2012
Print
Comments
  Baadhi ya viongozi CCM hawana maadili
  Akerwa na wanaolipuana ovyo nje ya vikao
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara),Pius Msekwa

Chama Cha Mapinduzi kimekiri kwamba baadhi ya viongozi wake wamekosa maadili hali inayochangia kukosekana kwa nidhamu ndani ya chama hicho.

Hali hiyo imeelezwa kwamba imesababisha miparaganyiko ndani ya CCM na kuleta mtikisiko ndani ya chama hicho.
Kauli hiyo ilitolewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa, wakati akizungumza kwenye kipindi cha Nipashe kinachorushwa na Redio One jana asubuhi.

Msekwa alisema kuwa maadili yametoweka ndani ya chama kutokana na utaratibu wa zamani wa mafunzo kwa makada kutokuwepo sasa.

Alisema awali kulikuwa na vyuo vya kuandaa makada na viongozi kwa ujumla, lakini vyuo hivyo kwa sasa havipo na ndiyo matokeo yanayoonekana ya kuporomoka kwa maadili na utu.

Kwa mujibu wa Msekwa, awali mwanachama ili ajiunge na chama, lazima anapitia mafunzo maalumu kwanza.
“Kulikuwa na semina za miezi mitatu kuhusu maadili. Semina hizi zilikuwa zinamuandaa mwanachama mchanga kujifunza mambo mbalimbali yakiwemo ya uadilifu…” alisema.

Makamu Mwenyekiti huyo alielezea kusikitishwa kwake kwa hali ya mambo inavyokwenda ndani ya chama hasa ya viongozi na makada wake kurushiana maneno nje ya vikao halali vya chama.

Alisema CCM inao utaratibu mzuri wa kukosoa na kukosolewa, utaratibu aliosema unafanyika ndani ya vikao halila.
Ndani ya CCM kumekuwa na mitafaruku ya mara kwa mara kwa viongozi wake kulaumiana na kudhalilishana hadharani.

Moja ya matukio ya aina hiyo ni la hivi karibuni ambapo aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige, alimtuhumu hadharani Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kuwa ni gamba namba moja linalotakiwa kuvuliwa.

Maige alidai kuwa Nape amekuwa akitoa matamshi mengi yanayosababisha kukisambaratisha, kukivunjia heshima na kukidhoofisha chama huku akishindwa  kubuni mbinu na mikakati ya kuingiza wanachama lakini pia kuzuia wanachama kukihama chama hicho.

Hata hivyo, Nape kwa upande wake alisema Mbunge huyo si saizi yake kwani yeye (Nape) ana majukumu ya kitaifa zaidi wakati Maige yuko ngazi ya kata na matawi.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment