Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Lema abomoa kwa Magufuli

22nd May 2012
Print
Comments
Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbress Lema (Chadema)

Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbress Lema (Chadema), amezidi kuzisambaratisha ngome za Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, baada ya makada saba wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Chato katika mkoa mpya wa Geita kukihama chama hicho na kujinga na Chadema.

Wakati tukio hilo likitokea, Lema, alielezea kushangazwa na uwezo mkubwa wa waziri huyo katika kutambua wingi wa samaki walioko majini pamoja na mimba zao, lakini ameshindwa kutatua tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa jimbo lake.

Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Chato kwenye mkutano wa hadhara, Lema alimtupia lawama Dk. Magufuli kuwa ameshindwa kuwatumikia wananchi wake katika kutatua matatizo yanayowakabili ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama.

Alisema wananchi hao wamekuwa wakitumia maji yasiyofaa kwa matumizi ya binadamu kutokana na kutumiwa na mifugo na wengine kuchota maji machafu ya ziwa ambayo yamekuwa yakiwasababishia magonjwa ya kuhara.

“Ndugu zangu inasikitisha sana kuona Chato ndiyo hii…wakati nikipita njiani kuja huku nimeshuhudia ziwa likiwa karibu kabisa na makazi yenu kiasi kwamba mbunge wenu angekuwa na nia thabiti ya kuwatumikia, nina imani wananchi wa hapa msingelikuwa masikini wa kutupwa namna hii…mimi ni mara yangu ya kwanza kufika hapa, lakini kutokana na mbwembwe za Magufuli bungeni kuonyesha anafahamu aina, idadi na mimba za samaki waliomo ndani ya maji niliamini Chato inafanana na Arusha kumbe la,” alisema.

Kauli hiyo ilisababisha wananchama 27 wa CCM wakiwemo makada saba kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema, hatua iliyotofasiriwa kuwa ni kuendelea kuvunjwa ngome za Magufuli ambaye pia ni Mbunge wa Chato kutokana na nafasi nyingine za wenyeviti wa vijiji vinane kati ya 11 kutwaliwa na Chadema katika uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizokuwa zimeachwa wazi na viongozi waliokuwepo awali.

Baadhi ya makada wa CCM waliokihama chama hicho ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkuyuni Uhuru Selemani na aliyekuwa katibu wa vijana wa Kata ya Chato, Masumbuko Kaitila.

Masumbuko pia aliwahi kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM mkoa wa Kagera, mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji mkoa wa Kagera na Katibu wa Hamasa wa Chipukizi Wilaya ya Chato.  Makada wengine mashuhuri waliohamia Chadema ni Lusia Kahindi, Fikiri Makoye, Samwel Mkome, Emmanuel Kayila na Vigoro Lucas.

Huku akitumia kauli mbiu ya “vua gamba vaa gwanda” na “vua ukada vaa ukamanda”, Lema aliwataka watumishi wa serikali hususani Jeshi la Polisi kuacha kutumia nafasi zao vibaya kwa kuwanyanyasa wananchi wakiwemo viongozi wa Chadema.

Alisema baadhi ya askari polisi wamekuwa wakitumiwa vibaya na viongozi wa chama tawala kutokana na kushinikizwa kuwapiga kwa marungu, mabomu na kuwabambikiza kesi baadhi ya wananchi na wafuasi wa vyama vya upinzani wakiamini kuwa njia hiyo itasaidia kudidimiza kasi ya mageuzi kwa jamii, hatua ambayo imekuwa ikiongeza chuki kwa wananchi dhidi ya polisi na serikali yao.

Aidha, aliwataka wananchi kwa kushirikiana na viongozi wa Chadema kushirikiana kufanya maandamano ya amani kuishinikiza serikali kuwafukuza kazi watendaji wabovu na wabadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo ya wilaya ya Chato ambazo zimedaiwa kutafunwa ili serikali iwaburuze mahakamani.

 MBOWE, SLAA KUONGOZA OPERESHENI KUSINI

Awamu mpya ya operesheni ya Chadema inayolenga kuhamaisha umma kuleta mabadiliko na uwajibikaji serikalini iliyopangwa kufanyika katika mikoa ya Kanda ya Kusini, itaanza rasmi Mei 28, mwaka huu, katika Mkoa wa Mtwara.

Akizungumza na NIPASHE jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alisema operesheni hiyo itaongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe.

Alisema wengine watakaoongoza operesheni hiyo, ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa pamoja na wabunge wa chama hicho na kwamba, itahitimishwa katika mkoa wa Lindi.

Kwa mujibu wa Mnyika, operesheni hiyo imelenga kushughulikia mambo matatu; la kwanza likiwa ni kusimamia uwajibikaji katika ngazi zote za serikali, ili kuhakikisha changamoto zote zinazolikabili taifa zinashughulikiwa.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema jambo la pili litakaloshughulikiwa na operesheni hiyo, ni kutoa elimu ya kisiasa kwa umma kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema jambo la tatu, litakuwa ni kujenga organaizesheni ya chama mijini na vijijini katika mikoa hiyo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles