Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kero zinapomtoa chozi Filikunjombe bungeni

16th May 2012
Print
Comments

NI dhahiri kwamba sasa taifa limefika mahali ambapo ‘siasa za kisasa’ zinapaswa kupewa nafasi ili kuchagiza kasi ya maendeleo nchini.

Siasa za kulindana hususani ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimekuwa kichochea cha kushuka kwa uwajibikaji, ulinzi na utetezi wa rasilimali za umma, huku kiwango cha rushwa na aina nyingine za ufisadi kikipanda kwa kasi ‘ya kutisha’.

Wanahusika katika uovu huo ni viongozi na wawakilishi wa umma, wale waliopewa dhamana ya kuhakikisha jamii inapata maendeleo na ustawi bora, lakini inakuwa kinyume chake.

Wanachota kila kinachoistahili jamii, wanajilimbikia kupita ukomo na kuwaacha wananchi wanaowaongoza wakilazama kwenye dimbwi la ‘umasikini wa kutupwa.’

Hali hiyo inawafanya wananchi kwa idadi iliyo kubwa kupunguza ama kukosa kabisa imani kwa serikali iliyopo madarakani. Kwa maana kuwepo kwa serikali iliyopewa dhamana ya kuliongoza taifa inakosa maana katika maisha yao ya kila siku. Wanapoteza matumaini na kuamua kumuachia Mungu!

Hata hivyo, inavyoonekana ni kwamba Mungu hamtupi mja wake. Umma wa Watanzania ni sehemu ya waja wa Mwenyezi Mungu, ndio maana katikati yao, anawaibua wachache miongoni mwa watawala na wawakilishi ili wausemee umma.

Kuusema umma wa Watanzania katika dhana ya maendeleo na ustawi wao inahitaji ujasiri, lakini hata ukiwa na nguvu kuliko Simba, uozo unaofanywa na baadhi ya viongozi wa serikali, wakilenga kuzihujumu rasilimali za umma, unasononesha na hata kufikia hatua yakumtoa mtu machozi.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe, ambaye kwa maneno yake wakati akiwahutubia wananchi wa jimbo hilo, anaweza wazi jinsi machozi yalivyomjaa bungeni.

Machozi ya Filikunjombe mmoja wa wanahabari mahiri nchini, hayakulenga kuwalilia wana familia wake, mali zake binafsi, ama kingine chochote kinachogusa matakwa ya nafsi yake.

Anasema yaliyotokana na mlingano wa ukubwa wa ‘mdudu’ anayeitwa umasikini kwa jinsi unavyoathiri jamii, na ukwasi waliojilimbikizia baadhi ya viongozi kwa njia za wizi wa mali za umma, rushwa na ufisadi.
******
Sehemu ya maneno ya Filikunjombe, akiuhutubia umma wa Ludewa anasema;_

Ndugu wananchi wenzangu, nikiwa mle bungeni, tukiwa tunaijadili ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, inayoonyesha ubadhirifu mkubwa katika fedha za umma; ghafla mawazo yangu yalihama kutoka bungeni yakaja katika vijiji vyetu vya Ludewa, Mavanga, Lusala, Lumbila, na kadhalika. Kitu kama mshale wenye ncha kali wa moto uliuchoma moyo wangu.

Nilikumbuka mateso makubwa mnayoyapata nyie wenzangu, nikaumia sana. Nilikumbuka namna mwananchi wa Ludewa anavyoishi katika mazingira duni na maisha ya dhiki.

Wakati baadhi ya Mawaziri, wanatumia nafasi zao kujineemesha, nilikumbuka jinsi mwananchi wa Ludewa anavyotaabika kwa miundombinu duni. Nilikumbuka jinsi tulivyo na bara bara mbovu. Nilikumbuka jinsi mwananchi wa Ludewa anavyocheleweshewa kuletewa Pembejeo za Kilimo.

Nilikumbuka jinsi mwananchi wa Ludewa anavyoletewa mbegu za kupandia mwezi wa pili wakati msimu wa kupanda mahindi ni mwezi Novemba.

Nilikumbuka Jinsi mawakala wa Pembejeo wanavyokopwa mbolea na serikali yetu, na hakuna kauli maalum inayotolewa.

Nikaumia sana. Nilikumbuka namna wanafunzi wa Ludewa wanavyosoma katika mazingira duni, wamekaa chini, walimu hawatoshi, madarasa hayatoshi, nyumba za walimu hazitoshi. Nilikumbuka namna sekondari zetu zinavyokosa maabara. Nilizidi kuumia moyoni mwangu.

Ripoti ile mbovu ya CAG inayonyesha wahe. Mawaziri wetu wametutelekeza, ilinikumbusha namna shule zote za Msingi na Sekondari zilivyo na upungufu mkubwa wa vifaa vya kufundishia.

Nilikumbuka jinsi vijiji vyetu havina zahanati na pale palipo na zahanati kuna upungufu mkubwa wa dawa, waganga pamoja na wauguzi.

Machozi yalizidi kujaa machoni. Nilizidi kushikwa na huzuni. Nilikumbuka jinsi wananchi wenzangu wa Ludewa mlivyokata tamaa kwa umaskini uliokithiri, wakati fedha zenu za Umma zinatafunwa na kikundi cha viongozi wachache tu, wanaojali matumbo yao. Machozi yalizidi kujaa machioni mwangu.

Nilipowatazama wabunge wenzangu niliona wengine wamevishika vitabu vya CAG na wengine walikuwa hawavisomi kabisa. Wabunge wengine walikuwa wakiendelea na mambo yao.

Nilikumbuka jinsi ambavyo kuna miezi mingine serikali yetu haileti hata senti tano Ludewa, huku Waziri wa Fedha akitumia Tshs. 1.3 trillioni kwa matumizi yake binafsi, bila idhini ya Bunge. Matatizo yetu Ludewa yalinipa nguvu za kuikemea serikali yetu. Nikapiga moyo konde, nikasema, na nitasema ukweli.

Ni kwa sababu hizo, kwa niaba yenu, niliitaka Serikali yetu ya CCM iwawajibishe Mawaziri wote walihusika katika vitendo vya ufisadi. Sikuishia hapo, mimi pia kwa niaba yenu, nilitia saini katika hoja ya kuunga mkono kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, na serikali yake endapo atakataa kumshauri Rais kuwawajibisha hao mawaziri.

Kwa hali hiyo, inawapasa viongozi na wawakilishi wa umma kuyatazama matatizo yanayowakabili wananchi, ili wayaelekee na kujitoa kwa namna iwayo yote, yapate ufumbuzi.

Kukemea uovu na uozo ndani ya taasisi yoyote ya kijamii kama vilivyo vyama vya siasa, haina maana ya kusababisha chuki na mafarakano, kuleta mabadiliko yenye matokeo chanya kwa jamii.

Filikunjombe ameainisha mlolongo wa kero zilizomfikisha katika kutoa machozi bungeni, lakini kero hizo zipo kwenye eneo kubwa la nchi ambalo hata hivyo, wapo baadhi ya wawakilishi kama yeye (Filikunjombe) wanaoliona na wapo walio wengi wasioliona.

Ndio maana wamejitokeza wanaombeza, wanaoshambulia Filikunjombe na wengine wa kariba yake, lakini wanapaswa kusimamia ukweli na kuamini katika kuishi siku chache ukiwa shujaa, kuliko kuwepo duniani miaka ‘nenda rudi’ ukiwa umefunikwa blanketi la woga!

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kwenye simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe: [email protected]

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles