Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mabosi wa serikali wasomewa mashitaka 120 mahakamani

9th May 2012
Print
Comments

Watumishi sita wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani humo, wakikabiliwa na makosa 120 ya kughushi nyaraka, kudanganya na kumuibia mwajiri ambaye ni serikali zaidi ya Sh. milioni 54.

Watumishi hao ni Mhasibu Msaidizi wa halmashauri hiyo, Pere Muganda (50); Mhasibu, Emmanuel Shija (40); Mhandisi, Felisian Msangi ( 49); Mkuu wa Shule ya Msingi Rongai, Mussa Mruma (54); Ofisa Usambazaji, Silivia Shirima (46) na Ofisa Usambazaji Msaidizi, Rachel Mshangila (48).

Washitakiwa wa kesi hiyo namba 04 ya mwaka 2012, walisomewa mashitaka jana mbele ya Hakimu Mfawidhi, Simon Kobelo, wakidaiwa kutenda makosa hayo kati ya kipindi cha mwaka 2007 na 2010.

Ilidaiwa kuwa mshitakiwa wa kwanza hadi wa nne ambao ni Msangi, Shija, Rachel na Shirima wana makosa 34, mshitakiwa wa tano Muganda ana makosa 18, mshitakiwa wa nne (Shirima) ana makosa mengine manane, mshitakiwa wa sita Mruma ana kosa moja, mshitakiwa wa pili Shija ana makosa mengine matatu, mshitakiwa wa tatu Rachel ana makosa mengine 33 na mshitakiwa wa nne ana mashitaka mwengine 15. 

Akiainisha makosa hayo kwa ujumla mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Patrick Mwita, alidai kuwa mshitakiwa wa kwanza na wanne kwa pamoja walighushi nyaraka kuonyesha kuwa lori tatu za mchanga zilipelekwa kwenye Kituo cha Afya cha Karume, jambo ambalo siyo la kweli.

Alidai kuwa mshtakiwa wa nne, ambaye ni Ofisa Usambazaji, Agosti mwaka 2009, alitengeneza nyaraka kuonyesha kuwa kuwa lori 16 za mchanga zilipelekwa kwenye kituo hicho, lakini aliiba mchanga huo wenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 1.4

Wakili Mwita alidai kuwa mshitakiwa huyo pia alitengeneza nyaraka kuonyesha kuwa lori kumi za kokoto na matofali 2,100 yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 3.4, yalipelekwa kwenye kituo hicho huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Alidai kuwa mshtakiwa huyo alighushi nyaraka kuonyesha kuwa mifuko 180 ya saruji yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 2.8 ilipelekwa kwenye kituo hicho.

Alidai kuwa Juni 4, mwaka 2009, mshitakiwa wa kwanza ambaye ni mhandisi na wanne, walitengeneza nyaraka kuonyesha kuwa lori nne za kokoto zenye thamani ya Sh. 480,000, zilipelekwa kwenye ujenzi wa mgahawa wa halmashauri hiyo, uitwao Bomani, jambo ambalo siyo la kweli.

Alidai kuwa Agosti 25, mwaka 2008, washitakiwa hao pia walitengeneza nyaraka na kufanikiwa kuiba kiasi cha Sh. 1,550,000 kwa kudai kuwa zilinunua mifuko 100 ya saruji na lori tano za mawe zilitumika kwenye ujenzi wa mgahawa huo, jambo ambalo siyo la kweli.

Mwita aliongeza kuwa katika kipindi hicho mshitakiwa wa nne, alitengeneza nyaraka kuonyesha kuwa mifuko 350 ya saruji yenye thamani ya Sh. 4,795,000 ilipelekwa katika shule za sekondari za
Tanya, Mbomai, Nduweni, Kahe Usseri, Ngereni, Booni na Mema kwa kila shule kupata mifuko 50 ya saruji, jambo ambalo siyo la kweli.

Alidai kuwa mshitakiwa Muganda ambaye ni Mhasibu Msaidizi wa halmashauri hiyo katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2009, alitengeneza nyaraka na kujipatia kiasi cha Sh. milioni 16 kutoka vyama vya msingi vya ushirika vya Mamsera, Mengwe, Keni, Makiidi, Mkuu, Msaseni na Essab na fedha nyingine ambazo zilitakiwa kupelekwa kwenye vituo vya afya vya Kirua, Ikuini na Keni.

Wakili huyo alidai kuwa mshitakiwa wa sita, Mussa Mruma, ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Rongai, anakabiliwa na kosa la kughushi nyaraka na kujipatia Sh. 18, 228, 847, makosa ambayo alitenda kati ya Mei 2009 hadi Februari 2010.

Mwita aliendelea kudai kuwa mshitakiwa Emmanuel Shija, alitengeneza nyaraka na kuonyesha kuwa gari lenye namba za usajili SM 4165 liliwekewa mafuta ya diesel yenye thamani ya zaidi ya Sh. 870,000 katika kituo cha mafuta cha Dodoma Gapco.

Alidai kuwa mshitakiwa Rachael Mshangila alitengenza vocha kumi za malipo mbalimbali kuonyesha imesainiwa na watu waitwao Andrew Malisa, John Kisela, Seleiman Mpanju, Goefrey Kabyemera na Prosista Mtenga, huku akijua kuwa siyo kweli na kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Mwita alidai kuwa mshitakiwa huyo akiwa ofisa usambazaji, aliiba karatasi za urudufishaji rimu 180 zenye thamani ya Sh. 1,260,000 na nyingine kuonyesha kuwa mtu aitwaye Kabyemera amelipwa vipande 30 vya wino.

Hata hivyo, washtakiwa hao walikana mashitaka hayo, ambapo upande wa mashataka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na hauna pingamizi na dhamana kwa washtakiwa hao alimradi watimize masharti.

Hakimu Kobelo aliyataja masharti ya dhamana kwa mshitakiwa wa kwanza hadi wa tano kuwa ni kuwa na wadhamini watatu, wawili kati yao wawe wafanyakazi wa serikali, ambapo wataweka dhamana ya mdomo ya Sh. milioni 15 kila mmoja.

Alisema mshtakiwa wa sita Mruma anakabiliwa na kosa la wizi wa zaidi ya Sh. milioni 18, hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu Uchumi, anatakiwa kuweka dhamana nusu ya fedha, ambazo ni Sh. milioni tisa au mali isiyohamishika yenye thamani ya fedha hizo.

Hadi NIPASHE inaondoka mahakamani humo, majira ya saa 8:30 mchana,washitakiwa wote walikuwa hawajafanikiwa kupata dhamana na hivyo kwenda rumande. Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa Mei 22, mwaka huu.

Kukamatwa kwa washitakiwa hao kumefuatia taarifa ya Mdhibiti na na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2007/2008, 2008/09 na 2009/10 iliyoonyesha kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Rombo inakabiliwa na ubadhilifu wa zaidi ya Shilingi bilioni moja.

Akizungumza na NIPASHE, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamana na Rushwa (Takukuru), wilayani Rombo Chuzela Shija, ambaye alikuwepo mahakamani, alisema huo ni mwanzo tu na kwamba watumishi zaidi wanadaiwa kuhusika katika ubadhilifu wa fedha na mali ya umma watafikishwa mahakamani hapo kadri upelelezi utakavyokamilika.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles