


.jpg)
Wananchi kisiwani Pemba, wamezungumzia vurugu za Zanzibar huku wakiwa wamegawanyika kuhusu wazo la Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara (JUMIKI), la kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa mwaka 1964.
Wakizungumza katika mahojiano na NIPASHE kwa nyakati tofauti huko wilayani Wete, mkazi wa eneo la Mtemani, Mrisho Juma Mtwana, alisema kwamba haungi mkono wazo la Uamsho la kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano, kwa vile watakaoathirika ni wakazi wengi kutoka Pemba.
Alisema kwamba, idadi kubwa ya vijana pamoja na wafanyabiashara kutoka Pemba, wanategemea soko la Tanzania Bara, na wameweza kunufaika kiuchumi na kuzisaidia familia zao zinazoishi kisiwani Pemba.
Alisema kwamba iwapo Muungano utavunjika, itakuwa ndio mwanzo wa kuvigawa visiwa vya Unguja na Pemba kwa vile Waunguja wengi bado wanaunga mkono kuendelea kwa Muungano, jambo ambalo linaweza kuyumbisha umoja wa kitaifa miongoni mwa wananchi wa Zanzibar.
Suleiman Ali Haji, Mkazi wa Kizimbani Wete, alisema kwamba jambo la msingi kero za Muungano zijadiliwe badala ya kukaribisha mawazo ya kuuvunja Muungano kwa vile Wazanzibari wengi wataathirika hasa kutoka kisiwani pemba ambao tayari wamewekeza vitega uchumi vikubwa.
Alisema Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara, watalazimika kulipia vibali vya kuishi kila mwaka kabla ya kupewa uraia, na kulipia kodi ya ardhi, jambo ambalo litawaathiri Wazanzibari wanaofanya shughuli za kilimo katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na wafanyabiashara ndogo ndogo.
Hata hivyo, alisema jambo la msingi viongozi wa dini ni vyema wakabakia katika jukwaa la dini, ili kuepusha migongano isiyokuwa ya lazima na kupinga kutumika kisiasa ili kulinda umoja wa kitaifa uliodumu zaidi ya miaka 48 iliyopita.
Kwa upande wake, Mrisho Juma Mtwana, mkazi wa Jadida Wete, alisema kwamba fursa aliyoitoa Rais Kikwete ina umuhimu mkubwa, jambo la msingi kwa Wazanzibari kujipanga vizuri kudai haki za msingi za Zanzibar ndani ya Muungano badala ya kutaka kujitenga.
Alisema ni wakati muafaka kwa wananchi wa Zanzibar kutoa maoni yao wakati utakapofika, kupitia tume iliyoundwa ya kuratibu na kukusanya maoni kuhusu katiba mpya ya Muungano, ili Zanzibar iweze kunufaika na kupata haki zake ambazo hivi sasa zinaonekana kuwa ni kero.
Naye Mwalimu Faki Khatib Simba mkazi wa Micheweni, alisema tatizo watu wengi hawafahamu mambo ya Muungano, na wanasiasa badala ya kuwaelimisha wananchi wanapotosha kwa masilahi yao binafsi ya kisiasa.
Naye, Mohamed Abdallah Ngushi mkazi wa Micheweni alisema kwamba tatizo sio muungano, bali mabaya yaliyomo ndani ya Muungano, na ndio maana vijana wa sasa wamesoma na kuanza kugundua kasoro za Muungano katika nyanja ya kiuchumi na ushirikiano wa kimataifa, ambazo sasa wanataka zitatuliwe na sio kutengana.
Kwa upande wake, Rashid Jabu Dawa, mkazi wa Micheweni, alisema yeye binafsi anataka muungano uvunjike kwa sababu Serikali zote mbili kwa muda mrefu zimeshindwa kutatua kero za Muungano, na kuikosesha Zanzibar haki zake kama Nchi.
Faki Makame Kombo mkazi wa Micheweni, alisema Muungano uvunjwe, kwa vile viongozi wengi wamepita na kushindwa kutatua kero za Muungano tangu Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na sasa Jakaya Kikwete.
Alisema viongozi hao wameshindwa kutatua kero za Muungano, jambo ambalo limewakatisha tamaa wananchi hasa wa Zanzibar ambao hali zao zinazidi kuwa duni, umasikini unaongezeka, na wachache wanaonufaika.
Katibu wa wazee 12 waliokuwa wakitaka kisiwa cha Pemba kujitenga na Unguja, ili kijitawale chenyewe kutokana na mwamvuli wa Muungano, Hamad Ali Mussa mkazi wa chakechake, alisema kwamba Muungano umekuwa na dhuluma dhidi ya Zanzibar na ndio maana wamekuwa wakiupinga tangu 2008.
Alisema kwamba wao binafsi walifikia kupeleka malalamiko yao Umoja wa Mataifa kupitia ofisi ya UNDP Dar es Salaam, kutaka Pemba ijitenge baada ya kuona Serikali ya Uchunguzi wa NIPASHE kisiwani Pemba, umebaini wananchi wengi bado wanahitaji kuwepo kwa Muungano mbali na wanasiasa, lakini wanataka kero za Muungano zitatuliwe, ili pande zote mbili ziweze kunufaika, mawazo ambayo hayatofautiani na Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara.