Sunday May 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Ufumbuzi matatizo ardhi, makazi haujapatikana pamoja na kumfukuza mbunge

15th July 2012
Print
Comments

Kila mtu nchini ni shahidi. Kwamba, ardhi ni katika rasilimali, ambayo imekuwa ikisababisha matatizo mengi na makubwa hapa nchini.

Vurugu, ambazo zimekuwa zikisababisha uvunjifu wa amani wa watu kujeruhiwa, mali za mamilioni kuharibiwa na wakati mwingine hata kusababisha vifo kutokana na migogoro ya ardhi, ni ushahidi tosha unaothibitisha ukweli huo.

Yapo mambo mengi yanayochangia kuwapo na migogoro ya ardhi. Nafasi hapa haitoshi kuweza kuyataja mambo yote. Nitataja machache.

Jambo mojawapo linalochangia migogoro ya ardhi, ni kutokuwapo upimaji wa maeneo, kutokutolewa hati za kumiliki ardhi na kukithiri kwa baadhi ya maofisa ardhi.

Jumatano wiki hii, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, aliwasilisha bungeni bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2012/2013 na kupitishwa na Bunge Ijumaa wiki hii.

Siku moja kabla ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk. Faustine Ndungulile, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alimfukuza bungeni na kumtaka kutohudhuria vikao vitatu vya Bunge.

Alifukuzwa kutokana na kugoma kufuta kauli yake ya kuwatuhumu madiwani wanne wa jimboni kwake kuwa walihongwa na Waziri Tibaijuka ili kuunga mkono ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni.

Hata hivyo, kabla ya Dk. Ndugulile hajafukuzwa, Ndugai alimpa dakika tano kujitetea bungeni, ambapo alisisitiza kauli yake kwamba, anaungana na wapigakura wake kupinga ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni kwa kuwa unakiuka sheria ya ardhi inayotamka kuwa ardhi ni mali ya wananchi, ambao hawakushirikishwa. Hivyo, akaeleza bayana kuwa haungi mkono bajeti hiyo kupitishwa na Bunge.

Dk. Ndugulile alikwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba, utendaji wa Waziri Tibaijuka ni ziro. Pamoja na hivyo, bajeti ya wizara yake imepitishwa na Bunge.

Kwa mtazamo wa juu juu, unaweza kuona uamuzi wa Bunge kuiridhia bajeti hiyo kwamba, Waziri Tibaijuka amefanya vizuri na kwamba, Dk. Ndugulile ana chuki binafsi na wivu. Na kwa hiyo, alistahili kufukuzwa bungeni.

Lakini ukweli hauko hivyo. Ukweli ni huu. Kwamba, pamoja na bajeti hiyo kupitishwa na Bunge, bado kuna matatizo katika sekta ya ardhi. Waziri Tibaijuka hajayapatia ufumbuzi. Na kwa hiyo, msimamo wa Dk. Ndugulile kukataa kuunga mkono bajeti hiyo, bado yuko sahihi.

Hapo juu nimegusia kuwa jambo mojawapo linalochangia migogoro ya ardhi, ni kutopima ardhi na kutokutolewa hati ya umiliki wa ardhi. Waziri Tibaijuka aliliambia Bunge kwamba, hadi sasa ni asilimia 10 tu ya ardhi ndiyo iliyokwishapimwa nchini!

Ikiwa ukweli ni huo, hivi kweli kiwanja kinaweza kupimwa ndani ya saa ngapi kwa kutumia teknolojia ya kisasa?

Udhaifu wa kutopima maeneo na kutoa hati, umekuwa ukitumiwa na wajanja wachache, ambao wamekuwa wakitumia vibaya sheria kunyang’anya watu maeneo yao. Wimbi la madhalimu hao limekuwa kubwa sana nchini. Tatizo hilo bado halijalipatiwa ufumbuzi na waziri.

Hali ikiwa hiyo, Waziri Tibaijuka bado anauambia umma kupitia Bunge kwamba, mtu ambaye hamiliki ardhi kisheria aondoke!

Hivi ni watu wangapi nchini, hasa wanaoishi vijijini wanaomiliki ardhi kisheria?

Kama hali ni hiyo, ni wazi kuwa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni unaong’ang’aniwa na serikali, hauwezi kuwa muhimu kama kupima maeneo, ambayo yamekuwa yakihatarisha amani miongoni mwa wananchi kutokana na migogoro ya ardhi.

Kwa nini basi, matrilioni ya shilingi (Sh. trilioni 11) zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa mji huo mpya wa Kigamboni yasielekezwe kwenye kupima maeneo ili kurejesha hali ya amani na utulivu nchini?

Kwanza hilo eneo la mji mpya wa Kigamboni lililotengwa na serikali kwa ajili ya majengo ya kifahari, halizidi umbali wa kilomita 14.

Tofauti na maeneo ya nje, ambayo yamekuwa yakihatarisha amani na watu wengine kudhulumiwa, hayajapimwa, eneo hilo litatumiwa na watu wachache tu. Kama maeneo yatapimwa, hakuna mtu atakayedhulumiwa.

Kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kuwa bajeti ya Waziri Tibaijuka imetoa majibu dhidi ya matatizo madogo. Imeacha makubwa.

Mbunge wa Temeke (CCM), Abbas Mtemvu, akichangia mjadala wa bajeti ya wizara hiyo, alisema ni mwaka wa saba sasa tangu aanze kufuatilia hati ya kiwanja bila mafanikio! Akahoji. Ikiwa ni hivyo kwa mbunge, je, kwa mwananchi wa kawaida hali ikoje?

Tatizo lingine, ambalo halijashughulikiwa na Tibaijuka, ni rushwa iliyokithiri kwa baadhi ya maofisa ardhi. Kwa rushwa hiyo wamekuwa wakichangia migogoro ya ardhi kwa kugawa kiwanja kimoja kwa watu wawili tofauti.

Pia wamekuwa wakiuza na kugawa viwanja vya wazi, huku wakijua kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha maadili ya kazi zao. Hata hivyo, Waziri Tibaijuka hajaeleza ni maofisa wangapi wa ardhi amekwishawachukulia hatua kwa makosa hayo!

Jambo lingine, ambalo halionyeshi kama Waziri Tibaijuka amefanya vizuri, linahusu mradi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wa kujenga nyumba 15,000 hadi ifikapo mwaka 2015. Inaelezwa kuwa nyumba hizo zitauzwa kwa bei nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, mwananchi, ambaye atashindwa kununua nyumba ya Sh. 70,000 ataweza kununua nyumba za bei nafuu, ambazo zitauzwa kwa Sh. milioni 25 hadi milioni 40!

Lakujiuliza ni hili. Hivi mwananchi wa kipato cha chini, ambaye inaelezwa kuwa anaishi kwa dola moja ya Marekani kwa siku, anaweza kweli kumudu kununua nyumba ya Sh. milioni 25?

Majibu ya haraka haraka, ni kwamba, ufumbuzi wa matatizo ya ardhi na makazi nchini bado haujapatikana.

Kumfukuza Dk. Ndugulile bungeni hakujasaidia kitu. Hivi hakuwezi kuwa kulifanywa makusudi baada serikali kuona imekosea, hivyo haikutaka sauti isikike? Au kuuhadaa umma uone kwamba, wanaofukuzwa bungeni si wapinzani tu, bali hata wanaCCM pia.

Muhibu Said ni mwandishi wa habari wa gazeti la NIPASHE: Simu 0717055551 au 0755925656. Baruapepe: muhibu72@yahoo.co.uk

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment