Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mkasa wa Yondani 'utie akili' viongozi Simba

21st July 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Klabu ya Simba jana ilipoteza rasmi rufaa yake kwa shirkisho la soka, TFF, ya kupinga mchezaji Kelvin Yondani kuidhinishwa na sekretariati yake kuichezea Yanga katika michuano ya Kombe la Kagame la klabu bingwa ya soka ya Afrika mashari na kati ambalo leo linafunga hatua ya makundi jijini.

Akizungumza na Waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa kamati ya Sheria na hadhi ya wachezaji ya TFF, Alex Mgongolwa alisema wakati wa kujadili rufaa ya Simba kamati yake ilibaini, kwanza, mkataba baina ya mchezaji huyo na timu hiyo ulimalizika Mei 31 hivyo kwa taratibu za usajili Yondani alikuwa huru kuanzia Juni mosi mwaka huu.

Pili, kamati hiyo ilibaini mkataba uliowasilishwa na Simba TFF kuonyesha kuwa Yondani ni mchezaji wake kwa kuwa ni nyongeza ya mkataba uliokuwepo TFF baina ya pande hizo mbili, uliwasilishwa Juni 7 mwaka huu ambapo ni kinyume cha utaratibu wa kuongeza mikataba ya wachezaji unaozitaka klabu kuwasilisha mikataba ya nyongeza ya muda wa mikataba ya wachezaji hao wakati mikataba halisi haijaisha.

Kwasababu ya matatizo hayo mawili mkataba huo mpya wa Simba na Yondani kwa jicho la kisheria haupo, kamati ya Mgongolwa iligundua.

Tatu, hata kama kamati ya Sheria na hadhi ya wachezaji ya TFF ingeuona mkataba huo upo katika jicho la sheria, imeelezwa bado mkataba huo una matatizo kisheria hasa katika tarehe ambazo pande mbili husika ziliingia makubaliano hayo.

Katika hali ya kushangaza, mkataba huo unabainisha kuwa wakati mchezaji Kevin Yondani aliingia makubaliano Desemba 23 mwaka jana, upande wa pili wa kimkataba ambao ni Simba uliingia makubaliano hayo kupitia kwa makamu mwenyekiti Geofrey Nyange Desemba 23 mwaka huu.

Ni makosa ambayo ni ya kizembe, mno, mno kutokea katika klabu kubwa kama Simba lakini tunafahamu, Nipashe, ni kwanini imetokea hivyo.

Ni imani yetu, Nipashe, kuwa mkataba baina ya Simba na Yondani uliandaliwa na mwanasheria lakini tatizo lake ikawa tu taaluma hiyo haikushirikishwa vya kutosha katika mchakato mzima wa kupata sahihi ya beki huyo wa timu ya taifa, Taifa Stars, pia.

Kama usajili wa wachezaji Simba ungekuwa unafanywa na ofisi ya klabu ambayo ina wanataaluma, ni wazi tatizo dogo kama la ufahamu wa tarehe za kuanza na kumalizika kwa mikataba ya wachezaji lisingeiacha ikililia beki ambaye amepotezwa kizembe.

Kama usajili wa wachezaji Simba ungekuwa unafanywa na ofisi ya klabu ambayo ina wanataaluma, ni wazi kosa kama la kukosea tarehe ya mkataba lisingekuwepo katika mkataba ambao ni unaonyesha kuwa ulisainiwa siku mbili tofauti.

Na kama usajili wa wachezaji ungekuwa unafanywa na ofisi ya Simba ambayo ina wanataaluma, ni wazi viongozi wa klabu hiyo wasingepoteza muda kukata rufaa wakipinga maamuzi yaliyopaliliwa na makosa ya kizembe waliyofanya wenyewe.

Simba ni klabu kubwa barani Afrka, ni taasisi, na kwa bahati nzuri si tu ina jengo zuri la klabu bali pia, shukrani kwa maagizo ya FIFA, shirikisho la soka la dunia, inapaswa kuongozwa na sekretariati iliyo chini ya katibu wa kuajiriwa ambaye yupo.

Lakini sekretariati ya Simba ndiyo inayoendesha Simba kweli katika shughuli zake za kila siku, usimamizi wa mauala ya usajili wa wachezaji ukiwemo?
Hapana.

Tena na tena, tumesikia, Nipashe, uongozi wa kuchaguliwa wa Ismail Aden Rage na wenzake ukifanya kazi za waajiriwa wa klabu kutokana na si tu kuwa wasemaji, bali pia waendeshaji wa masulala ya kila siku ya mabingwa hao wa Bara.

Tulitaraji, Nipashe, kwa mfano, Yondani angekuwa ameingia mkataba na wakili wa Simba kwa niaba ya klabu kama taasisi na si kiongozi ambaye muda wake wa kukaa madarakani si tu si wa kudumu, bali pia ni anayeweza kupinduliwa wakati wowote uchaguzi mdogo wa Yanga wa mwishoni mwa wiki ukiwa kielelezo.

Ufike wakati viongozi wa Simba wakajifunza kuacha masuala kama ya usajili, usemaji na uendeshaji wa shughuli za kila siku za klabu kwa waajiriwa; wenye taaluma na masuala husika.
Mkasa wa Yondani uwafundishe. Hivyo.




 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment