


.jpg)
Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam iliwapa raha mashabiki wake juzi baada ya kushinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Azam katika mechi yao ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) na kutetea taji hilo walilolitwaa pia msimu uliopita.
Huku wakiwa na kocha mpya, Mbelgiji Tom Saintfiet, na pia kikosi kilichojumuisha nyota wao kadhaa wapya, Yanga walionyesha kiwango kizuri na hivyo kukabiliana vyema na Azama ambao pia walionyesha soka safi waliloanza kulionyesha tangu mwanzo wa michuano.
Licha ya kuanza vibaya mashindano hayo baada ya kulala kwa mabao 2-0 katika mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Atletico ya Burundi, Yanga waliocheza fainali juzi walibadilika sana.
Walicheza kwa kasi na kushambulia vyema kwa kustukiza kila mara walipozidiwa katika kumiliki mpira. Ingawa walipoteza mechi hiyo, Azam ambao walikuwa wakishiriki Kombe la Kagame kwa mara ya kwanza ndio waliotawala zaidi mechi hiyo kutokana na pasi zao za uhakika.
Mashambulizi ya timu ya Azam inayoongozwa na raia wa England, Stewart Hall, yalidhibitiwa vyema na mabeki imara wa Yanga.
Ushindi wa Yanga uliwafariji mashabiki wao ambao kama timu yao ingepoteza mechi hiyo, ni wazi kwamba wangeumia zaidi baada ya kushindwa kufurukuta katika Ligi Kuu ya Bara ambayo walishika nafasi ya tatu huku mahasimu wao Simba wakitwaa ubingwa na pia kutolewa mapema katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
Tunazipongeza Yanga na Azam kwani kwa ujumla, zote zilionyesha viwango vya hali ya juu juzi na kuwapa mashabiki burudani iliyoitarajiwa.
Licha ya kutolewa katika hatua za robo fainali, Simba ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Bara na Mafunzo walioshiriki michuano ya Kagame baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar msimu uliopita, wote walionyesha kiwango kizuri, kama ilivyokuwa timu nyingine zilizoshiriki michuano hiyo za URA ya Uganda, Atletico ya Burundi, AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Tusker ya Kenya na APR ya Rwanda.
Timu pekee zilizoonyesha kuwa bado zina kazi kubwa ya kufanya kabla ya kuwazia taji la michuano hiyo ni Ports ya Djibouti na klabu ya Wau Salaam ya Sudan Kusini iliyokuwa ikishiriki michuano ya kimataifa kwa mara ya kwanza.
Ni matarajio yetu kuona kuwa baada ya kumalizika kwa michuano hiyo, Simba, Azam na Mafunzo ambazo zitawakilisha taifa katika michuano ya Afrika zikifanya marekebisho katika maeneo yaliyoonekana kupwaya wakati wakishiriki michuano ya Kagame.
Kwa mfano, safu ya mabeki wa Simba ilionekana kuyumba mara kadhaa wakati wa michuano ya Kagame. Kujichanganya kwao ndiko kulikowagharimu ‘Wana Msimbazi’ katika mechi zao dhidi ya URA ya Uganda wakati walipolala 2-0 na pia katika mechi waliyofungwa 3-1 dhidi ya Azam.
Simba inapaswa kujipanga zaidi pia katika eneo la ushambuliaji kwani michuano ya Kagame imedhihirisha kwamba bado timu hiyo haijapata wachezaji sahihi wa kuziba nafasi ya Mganda Emmanuel Okwi anayesaka nafasi ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya na pia aliyekuwa kiungo mshambuliaji wao, Mrwanda Patrick Mafisango aliyefariki kwa ajali ya gari.
Kikosi cha timu hiyo kinahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa ili kuwahakikishia ‘Wana Msimbazi’ mabao mengi zaidi wakati watakaposhiriki Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
Licha ya kufika fainali, Azam wanapaswa pia kuongeza nguvu katika safu yao ya ushambuliaji kwani takwimu za kufunga mabao sita tu katika michuano yote ya Kagame, huku matano kati ya hayo yakiwekwa wavuni na mchezaji wao mmoja sio nzuri sana. Ni lazima watafute njia bora za kufunga magoli mengi zaidi kabla ya ku anza ushiriki wao katika Kombe la Shirikisho.
Licha ya kucheza soka la kuelewana katika kila mechi, Mafunzo pia walionekana kukosa wamaliziaji wazuri wa nafasi kadhaa za kufunga walizokuwa wakijitengenezea. Ni kwa sababu hiyo, ndipo ‘maafande’ hao wakamaliza michuano ya Kagame bila kuambulia ushindi wowote ule. Ni wazi kuwa, kama benchi la ufundi la Mafunzo halifanyia marekebisho safu yao ya ushambuliaji, kamwe hawatafika mbali katika michuano watakayoshiriki ya Ligi ya Klabu Bingwa.
Hongera Yanga kwa kutetea ubingwa, shukrani kwa waandaaji wa michuano ya Kagame kwa kuzipa nafasi Simba, Azam na Mafunzo kupata nafasi ya kubaini kasoro zao kabla ya kupeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya klabu ya Afrika.