Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Madaktari wacharuka

10th June 2012
Print
Comments
  Waipa serikali wiki 2 vinginevyo kugoma
Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk. Namala Mkopi,

Madaktari wamecharuka tena ambapo wameipa Serikali siku 14 kutekeleza mapendekezo waliyotoa kwenye kamati maalumu iliyoundwa kushughulikia madai hayo, kinyume chake watatangaza kuingia kwenye mgomo tena nchi nzima.

Hayo yalibainika jana katika kikao chao cha ndani kilichofanyika jijini Dar es Salaam a kujadili ripoti ya kamati ya serikali iliyopewa jukumu la kukaa meza moja ili kujadiliana tatizo la madai yao.

"Wameafikiana kuwa katika kipindi hiki cha wiki mbili wataijibu ripoti hiyo kuwa wameikataa na pia wataisambaza kwa madaktari wote nchini," kilidai chanzo chetu cha habari.

Madaktari hao wamesema hawana imani na Kamati hiyo na kushangazwa na ripoti iliyotoka serikalini ambayo haikuonyesha ongezeko la mshahara waliotaka na kuambiwa kuwa suala hilo halitawezekana bila ya serikali kuonyesha mchanganuo wa kiasi cha fedha walicho nacho.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa madaktari hao walisema wamekaa vikao sita na kamati hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu lakini mpaka sasa hakuna suluhisho kuhusu mshahara wao.

Chanzo chetu cha habari kimedai kuwa kikao hicho cha ndani kimebaini kuwa kamati hiyo imekuwa ikiwazungusha kila mara katika hoja ya madai yao ya nyongeza ya mshahara.

Kimedai kuwa katika kikao cha pili madaktari walijadili hoja za uboreshaji wa huduma za afya kwa kuwa zinazorota na baadaye likaja suala la nyongeza ya mshahara.

Chanzo hicho kimesema pamoja na kukaa vikao vingi na kamati hiyo ya serikali, wamebaini kuwa haina nia ya kutekeleza madai yaliyotolewa na madaktari.

"Tumeikataa ripoti hiyo na pia hatuna imani na kamati kwani haina nia ya kusaidia madai ya madaktari kila wakati ni kujadili suala moja ambalo halimaliziki mpaka sasa na hawajaeleza hayo madai yetu yatatekelezwa kwa kiwango gani.

“Serikali inatakiwa itueleze wao wana shilingi ngapi juu ya nyongeza ya mshahara kama sisi tumetaja kiasi kikubwa ripoti hiyo ilitakiwa itueleze watatekeleza kwa kiasi gani na sio kila wakati kueleza hilo jambo halitekelezeki," alisema.

Katika madai yao madaktari walitaka kiwango cha mshahara kipande kutoka Sh. 860,000 na Sh. 900,000 ya sasa kwa daktari anayeanza kazi hadi kufikia Sh milioni 3.5 kwa mwezi.

Mmoja wa madaktari ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema kamati haijatoa majibu ya kuridhisha na taarifa waliyoipata inaeleza kuwa nyongeza ya mshahara itaathiri bajeti ya serikali.

Alisema jambo jingine lililowashangaza ni ahadi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutotekelezwa ya kulipwa saa za ziada kati ya Sh.20,000 na Sh. 25,000 kwa madaktari wanaoitwa kazini.

Katika ahadi hiyo Pinda aliwaambia katika bajeti ya mwaka huu madaktari bingwa watalipwa Sh 50,000 na daktari wa kawaida atapatiwa sh 40,000 kwa saa za ziada.

Hata hivyo, chanzo chetu kimesema Kamati hiyo katika ripoti yake imeondoa kabisa ahadi hiyo iliyowekwa na Waziri Mkuu.

Alisema katika taarifa hiyo imewajulisha kuwa suala la madai ya bima ya afya linaendelea kujadiliwa na mfuko wa bima ya afya ili madaktari waweze kupatiwa kitambulisho cha kuanza kupatiwa huduma hiyo.

Pia alisema suala la chanjo kwa madaktari ili waweze kujikinga na magonjwa hatarishi wamejulishwa watapatiwa kwa awamu hali ambayo iliibua mzozo mkali na kudai kuwa serikali imekuwa ikichezea taaluma yao kwa kutowajali.

Aidha alisema baadhi ya madai yao wamejulishwa kuwa yatatekelezwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha wa 2013/2014 ambapo wamedai kujibiwa kisiasa.

Alisema kwa sasa wanawaandaa madaktari wote walioko mkoani kuingia katika mgomo wa nchi nzima kama madai yao hayatatekelezwa.

Walisema kuwa mgomo wa awali walisitisha kwa heshima ya Rais Jakaya Kikwete kwa ahadi kamati hiyo itatekeleza madai yao na hatimaye kupata suluhu.

Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk. Namala Mkopi, alipohojiwa kuhusu azma ya mgomo huo alisema hawezi kuzungumzia lolote kwa kuwa kikao hicho kilikuwa ni cha ndani .

Hata hivyo, alisema madaktari watakutana baada ya wiki mbili kwa ajili ya kujadili mrejesho wa taarifa ya kamati ya serikali juu ya madai yao.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment