Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mbunge wa CCM anayewaumbua mawaziri wa CCM

29th April 2012
Print
Comments
Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe (kulia) akizungumza na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (kushoto) nje ya Bunge mjini Dodoma hivi karibuni.

Kama kuna majina ya wabunge watakayoingia kwenye kumbukumbu za mabadiliko ya kiutendaji kwa mawaziri wa serikali iliyoundwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Deo Filikunjombe ni mmoja wao.

Filikunjombe akiwa Mbunge wa Ludewa (CCM) mkoani Iringa, alisimama imara akiongoza mashambulizi dhidi ya mawaziri wasiokuwa waadilifu katika utendaji kazi wao, hata kufikia hatua ya kuichafua serikali iliyopo madarakani.

Akitumia ushahidi wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyowasilishwa kwenye Mkutano wa Saba wa Bunge uliofikia ukomo wake hivi karibuni mjini Dodoma, Filikunjombe aliamini na kuusimamia ukweli, kwamba baadhi ya mawaziri hawawajibiki ipasavyo.

Mapema wiki hii, NIPASHE Jumapili ilimhoji Filikunjombe ambapo pamoja na mambo mengine, anasema mawaziri hao na watendaji wengine waliotajwa kwenye ripoti ya CAG, walipewa majukumu walioshindwa kuyatekeleza.

KUINUSURU CCM

Filikunjombe anasema mkakati alioshiriki bungeni kwa mujibu wa kanuni za chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi, ulilenga kuinusuru CCM na serikali yake dhidi ya kupoteza mvuto na kukubalika kwa umma.

“Chama hakina tatizo lolote, lakini sioni kama baadhi ya mawaziri waliokabidhiwa dhamana za uongozi wanatekeleza majukumu na wajibu wao ipasavyo,” anasema.

Filikunjombe anasema kujenga hoja dhidi ya mawaziri wa serikali ya CCM, hakukuwa na maana ya kuibua mapinduzi, bali kuchagiza mabadiliko yatakayosukuma mbele maendeleo ya nchi na watu wake.

Anasema serikali ikisimamiwa vizuri na Bunge, itayafikia matakwa ya umma na hivyo kukifanya chama hicho (CCM) kudumu madarakani kwa muda mrefu.

“Tuhuma zinazowakabili mawaziri husika ni moja ya maeneo yanayoiathiri jamii pana ya Tanzania hivyo hakuna sababu ya kuweka mbele maslahi ya kisiasa, lazima tufike mahali kama hapa tulipo sasa, tupiganie maslahi ya umma,” anasema.

MCHANGO WA WABUNGE WA CCM

Filikunjombe anasema hoja ya kuwataka mawaziri waliotuhumiwa kwa wizi ama kutowajibika kwa mujibu wa nyadhifa zao wajiuzulu, ilipata nguvu sana kutokana na kuzungumzwa na wabunge wa CCM.

Anasema, “hoja hii ingesimamiwa na akina Zitto Kabwe isingekuwa na nguvu, kwa maana watu wangesema ni kawaida ya upinzani, lakini wabunge wa CCM tuliposimama na kuzungumza, imeleta matokeo makubwa.”

Filikunjombe alisema hali ya ustawi wa jamii imedumaa huku baadhi ya viongozi wa serikali wakiwemo mawaziri wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wakijilimbikizia mali kinyume cha sheria.

Anasema hali inawawia ngumu wabunge hasa wa CCM wanapokuwa majimboni, wakihojiwa kuhusu kutofikiwa kwa ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania, huku baadhi ya mawaziri wakizidi kujineemesha.

“Kama kule kwangu Ludewa, wananchi wanahoji kuhusu ukosefu wa huduma bora za afya, elimu, miundombinu na maji safi na salama, kwa hali ilivyo sasa na hulka hii ya mawaziri wasiokuwa waaminifu kuhujumu rasilimali za nchi, si rahisi kuyafikia maisha bora kwa kila Mtanzania.” Anasema.

WIZI KWENYE HALMASHAURI

Filikunjombe anasema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayoashiria wizi wa fedha za umma katika halmashauri ni matokeo ya kuwepo ombwe la uongozi hususani katika ngazi ya serikali kuu.

“Hivi tujiulize ni kwa nini Tanzania iliyo kwenye utajiri inakuwa masikini huku mawaziri wakibainika kuhujumu mali za umma na kujilimbikizia,” anahoji.

Filikunjombe anasema kilichopo sasa ni kuwepo viongozi na watumishi wa umma wanaokiuka maadili ya kazi zao na kuwekeza zaidi katika kufikia maslahi binafsi.

“Kuna viongozi tumewapa dhamana ya kuliongoza taifa, lakini siamini kama wanatekeleza wajibu na majukumu yao ipasavyo,” anasema.

Anasema, kuwa ndani ya CCM katika wadhifa wowote ukiwemo ubunge, haina maana kuweka kando maslahi ya umma na kushabikia uozo kwa kigezo cha kulinda itikadi moja.

KUSAINI WARAKA WA ZITTO

Akiwa mbunge wa kwanza kujitokeza hadharani na kusaini fomu zilizoandaliwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, Filikunjombe anasema miongoni mwa wabunge wa CCM wapo waliokuwa na nidhamu ya woga.

Anasema binafsi saini aliyoiweka kwenye fomu za Zitto haikuwa kwa niaba yake, bali iliwakilisha wananchi wa Ludewa wanaomtaka asaini fomu hizo.

Hata hivyo anasema baada ya kusaini fomu za Zitto akifuatiwa na wabunge wengine wakiwemo Alphaxad Lugora (Mwibara-CCM) na Nimrod Mkono (Musoma Vijijini-CCM), walio wengi hawakuitikia wito huo.

Anasema sababu iliyodhihirika ni kuwa na nidhamu iliyovuka mipaka kufikia kiwango cha kuogopa, hata pale maslahi ya umma yanapoathiriwa.

Lakini Filikunjombe anasema hilo halikuwa tatizo kwa vile baada ya kupita kwa hoja ya Zitto, Bunge lingepiga kura ya siri ambapo idadi kubwa ya wabunge wa CCM wangeonyesha hisia zao.

MAWAZIRI WANAOPASWA KUJIUZULU

Filikunjombe anaamini kuwa sakata hilo halipaswi kuelekezwa katika taswira ya kumnyooshea kidole mtu binafsi, bali wadhifa kwa kuzingatia maeneo makuu matatu.

“Waziri anaweza kujiona mwenyewe hana kosa, mamlaka iliyomteua inaweza ikamuona anafaa, lakini sisi anaotuongoza tukamuona hatufai, kwa hiyo lazima waondoke tu,” anasema.

Lakini Mbunge huyo anaweka wazi kwamba wanaotajwa kutokana na ripoti iliyowasilishwa bungeni ni watu wa awali, lakini kwenye orodha kabili wapo wengi wanaostahili kujiuzulu na kuwajibishwa.

HISIA ZA MAPINDUZI

Filikunjombe anasema kitendo kilichofanywa na wabunge kutaka baadhi ya mawaziri wa serikali kujiuzulu na wachukuliwe hatua, hakimaanishi kuwepo mapinduzi, bali harakati za kuleta mabadiliko yenye maslahi kwa CCM na umma kwa ujumla. Filikunjombe anasema CCM bado ni chama kizuri kwa maana ya muundo, sera, ilani na aina ya wanachama wake, lakini kimeunda serikali isiyokuwa na uwezo wa kufikia matarajio ya umma.

“Tumepata serikali iliyo dhaifu sana kiasi kwamba tunashindwa kutatua kero za jamii, tatizo halipo kwa chama bali watendaji serikalini,” anasema.

Anasema kutokana na hali hiyo, ni dhana potofu kwa wanaozusha hisia hasi kwamba yeye na wabunge walioshiriki kushinikiza mawaziri wasiokuwa waadilifu wajiuzulu, wana mpango wa kuhamia upinzani.

“Kwa mfano mimi ndani ya CCM nilipita bila kupingwa jimboni kwangu, sasa kuna dalili gani za kunifanya nikihame chama changu,” anahoji.

Hata hivyo harakati za wabunge wa CCM zilipelekea kuwepo vikao vilivyohitimishwa na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho ambayo ilitangaza kuridhia kushughulikiwa na kutimuliwa kwa mawaziri na watendaji wahusika.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles