Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Arusha Mjini bado ngome ya Chadema

11th April 2012
Print
Comments
Godbless Lema

Licha ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kulipoteza Jimbo la Arusha Mjini, jimbo hilo bado ni ngome ya chama hicho.

Jimbo hilo ambalo lilishikiliwa na mbunge kupitia Chadema, Godbless Lema, kwa zaidi ya miaka miwili, tangu mwaka 2010, lilipotea mikononi mwa chama hicho, Aprili 5, mwaka huu.

Hiyo ni kufuatia hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha na Jaji Gabriel Rwakibarila wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga.

Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Rwakibarila katika kesi iliyofunguliwa katika mahakama hiyo kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu yaliyompa ushindi Lema katika jimbo hilo.

Kesi hiyo ilifunguliwa na wanachama na makada watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Hao ni Agness Mollel, Mussa Mkanga na Happy Kivuyo.

Katika kesi hiyo, makada hao walidai taratibu za maadili ya uchaguzi zilikiukwa. Walidai mshindi (Lema) alitumia lugha za udhalilishaji, kashfa, matusi na kejeli katika mikutano yake ya kampeni za uchaguzi huo jimboni humo.

Walidai Lema alitumia lugha hizo dhidi ya aliyekuwa mgombea ubunge kupitia CCM, Dk. Batilda Burian, ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania, nchini Kenya.

Tayari Chadema imeshatangaza azma yake ya kukata rufaa kupinga hukumu hiyo ya Mahakama Kuu iliyomvua Lema ubunge jimboni humo.

Azma ya Chadema ya kukata rufaa ilitangazwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya NMC mjini Arusha, wiki iliyopita.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alisema katika mkutano huo kuwa chama hicho kitakwenda mahakamani kupinga hukumu hiyo.

Alisema Chadema itachukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na maamuzi ya Jaji Rwakibarila aliyetoa hukumu hiyo.

Mbowe alisema sasa Chadema itawasilisha rufaa yake Mahakama ya Rufaa ili kesi hiyo sasa iweze kupitiwa na kuamuliwa na jopo la majaji watatu na si mmoja kama ilivyokuwa awali.

“Maamuzi ya Jaji Rwakibarila hayakuwa sahihi na ni maamuzi ya kushangaza na yenye shinikizo. Ndio maana tumeona tukate rufaa ili kutafuta haki zaidi,” alisema Mbowe.

Alitaja sababu nyingine inayoifanya Chadema kukata rufaa ni kutokana na kutaka kuokoa fedha zaidi ya Sh. bilioni 3 na milioni 300 za wananchi walalahoi walipa kodi.

Alisema fedha hizo zingetumika katika uchaguzi mdogo, badala ya kupelekwa kwa wananchi kushughulikia kero za afya, maji na huduma nyingine muhimu.

“Kama CCM wamefurahi kwa kudhani kwamba wanakwenda kwenye uchaguzi mdogo, sisi Chadema tunasema hatuko tayari kwa hilo.Tuna taarifa kwamba serikali ya Rais Jakaya Kikwete imetia shinikizo kutolewa kwa hukumu hii,” alisema Mbowe.

Aliongeza: “Serikali na Rais Kikwete wanapaswa kujua nchi inaongozwa na mihimili mitatu ambayo ni Bunge, Mahakama na Dola. Kama Rais na serikali wanaweza kuingilia uhuru wa mahakama, basi tunasubiri Mahakama ya Rufaa itoe uamuzi wa rufaa.”

Kama nilivyogusia hapo juu, pamoja na Chadema kupoteza jimbo hilo na azma yake ya kutaka kukata rufaa, jimbo hilo bado ni ngome ya chama hicho.

Vipo vigezo vingi vinavyoweza kuthibitisha ukweli huo.  Kwanza ni matokeo halisi ya Uchaguzi Mkuu yaliyompa ushindi Lema jimboni humo.

Matokeo hayo yanaonyesha Lema alimwangusha aliyekuwa mpinzani wake mkubwa katika uchaguzi huo jimboni humo, Dk. Burian kwa kumshinda karibu kura 20,000.

Matokeo hayo yalitangazwa na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Arusha Mjini, Exomii Sanga.

Anasema Lema aliibuka mshindi baada ya kujizoela kura 56,59. Dk. Burian alipata kura 37,460.

Pili, ni mchuano mkali uliopo katika idadi ya madiwani waliovunwa na Chadema dhidi ya madiwani waliovunwa na CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 katika Manispaa ya Arusha.

Katika manispaa hiyo, CCM ina jumla ya madiwani 16, Chadema ina madiwani 15, wakati Chama cha Tanzania Labour (TLP) ina madiwani wawili. 

Mchuano wa idadi ya madiwani umekuwa ukisababisha kuwapo na mvutano na malumbano muda mrefu kati ya Chadema na CCM katika manispaa hiyo.

Hali hiyo inatokana na uchaguzi wa kumpata meya wa kuongoza manispaa hiyo.

Hadi sasa Chadema hawamtambui Meya wa Manispaa hiyo, Gaudence Lyimo, kwa madai kwamba hakuchaguliwa na vikao halali.

Kwa uchache, uchaguzi wa meya wa manispaa hiyo ambao mpaka leo unaonekana kama una mushkeli kwa mujibu wa Chadema ulizua kizaazaa kikubwa katika safu ya Chadema.

Watu kadhaa, wakiwamo madiwani watano wa Chadema walivuliwa uanachama baada ya kutia saini maelewano ya utaratibu wa muafaka kati ya madiwani wa CCM na Chadema.

Matatizo ya umeya yamesababisha kuwapo na kituko katika safu ya madiwani, huku Chadema mara nyingi wakisusia vikao ambavyo ndivyo vinavyofanya shughuli za  kuendesha Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Kikao cha kwanza tu cha Baraza la Madiwani wa Manispaa hiyo, madiwani wote 14 wa Chadema walitoka nje ya ukumbi, kwa madai kwamba hawamtambui Meya wa Manispaa hiyo, Lyimo.

Tatu, ni mwitikio wa watu katika mikutano ya hadhara, maandamano na shughuli nyingine za kisiasa na kijamii zinazoandaliwa na Chadema jimboni humo.

Nne, ni ushindi ambao Chadema iliupata hivi karibuni katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha.

Ni ukweli usiopingika kuwa ushindi huo wa aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kupitia Chadema, Joshua Nassari, katika Jimbo la Arumeru Mashariki, kwa kiasi kikubwa ulichangiwa na mwamko na ushawishi mkubwa wa wananachi kutoka Jimbo la Arusha Mjini.

Tano, ni namna mwitikio wa wananchi ulioonekana mahakamani siku ya hukumu na katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na uongozi wa Chadema mjini Arusha baada ya hukumu hiyo.

Tano, ni imani kubwa ya ushindi waliyonayo viongozi wakuu wa Chadema na Lema mwenyewe.

Hilo linadhihirishwa katika kauli ya Mbowe aliyoitoa katika mkutano wa hadhara baada ya mahakama kutoa hukumu hiyo.

Mbowe alisema: “Tungeweza kukubali kwenda kwenye uchaguzi kwa sababu tuna imani ya kushinda kwa kishindo kwa mara nyingine lakini tukifanya hivyo CCM itapata mwanya wa kuingilia uhuru wa mahakama kwa kesi nyingine za wabunge wa Chadema za Tundu Lissu (Singida Mashariki) na John Mnyika (Ubungo).”

Pia kwa upande wake, Lema aliwasihi wananchi kutokata tamaa na badala yake kuendeleza mapambano ili haki iweze kupatikana.

Alisema Jumanne ijayo (jana) angeandika barua kwenda kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, kumuarifu kwamba bado ni Mbunge wa Arusha Mjini, lakini yupo likizo akisubiri kuamriwa kwa rufaa yake na Mahakama ya Rufaa.

Aliwataka wananchi wa Arusha Mjini na wapenzi wa Chadema kumuomba Mungu kwa kufunga kula chakula kwa muda wa siku saba ili Mungu aweze kuonesha maajabu yake.

Tano, ni imani kubwa waliyonayo wananchi jimboni humo kwa Chadema. Hilo limekuwa likidhihirika kupitia ujumbe wa mabango wanayobeba na nyimbo mbalimbali wanazoimba katika maandamano na mikutano ya hadhara inayofanywa na Chadema jimboni humo. 

Pamoja na Chadema kuazimia kukata rufaa, hukumu ya Mahakama Kuu ya kumvua Lema ubunge, itaendelea kutekelezwa ili kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa inayoweza ama kukazia hukumu ya Mahakama Kuu au kumrejeshea ubunge.

Hata hivyo, bado sijapata hoja ya kuridhisha juu ya sababu za Chadema kutokubali kuingia karika uchaguzi jimboni humo.

Hiyo ni kutokana na imani kubwa waliyonayo viongozi wakuu ngazi ya taifa wa Chadema, Lema na wananchi juu ya uwezo wa kushinda jimboni humo na kulirejesha jimbo hilo mikononi mwao, kama anavyoeleza Mbowe.

Naomba nikatwe kiu yangu. Kama Chadema wanao uwezo wa kulirejesha jimbo hilo mikononi mwao, kwanini wasikubali kuingia moja kwa moja katika uchaguzi badala ya kuamua kukata rufaa kupinga hukumu ya mahakama dhidi ya ushindi wa Lema katika Jimbo la Arusha Mjini?

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles