Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Manispaa Kinondoni inawajibika ufisadi huu Soko la Makumbusho

3rd June 2012
Print
Comments

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, kamwe haiwezi kukwepa kashfa hii mpya. Na ni muda muafaka sasa kwa vyombo vya dola, kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) kuchukua hatua.  

Kashfa hiyo inahusisha baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa Ofisi ya Afisa Mtendaji Kata ya Kijitonyama, kujipatia mamilioni ya fedha kwa njia za kifisadi kupitia kodi ya upangishaji wa vibanda vya biashara vilivyoko katika Soko la Makumbusho.

 Upo ushahidi usiokuwa na shaka, kwamba watendaji hao wanawatoza wafanyabiashara wapya Sh. milioni 1.5 badala ya malipo halali ya Sh. 15,000 ya kodi ya upangishaaji wa vibanda hivyo.

 Katika kutekeleza ufisadi huo, baadhi ya wafanyabiashara sokoni hapo, Jumatano wiki hii walivamiwa na askari mgambo wa kata na kuvunjiwa kufuli na kisha kutimuliwa kwenye vibanda walivyokuwa wakivitumia kuendesha biashara zao sokoni hapo muda mrefu.

 Sababu za kufanyiwa dhuluma na unyama huo zinatolewa nyingine. Lakini ukweli ni kwamba ni baada ya kuonekana kodi ya Sh. 15,000 waliyokuwa wakilipa ni ndogo.

 Taarifa sahihi ni kwamba, baadhi ya vibanda ambavyo wafanyabiashara wake wametimuliwa, tayari vimekwishapangishwa wafanyabiashara wengine wapya kwa Sh. milioni 1.5.

 Mimi ni mmoja wa waandishi wa habari niliyepata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wafanyabiashara waliopangishwa kwa Sh. milioni 1.5.  wamethibitisha hilo.

Pia hivi karibuni nilifika sokoni hapo. Nikaigiza kuwa ni mfanyabiashara ninayehitaji kibanda cha kufanyia biashara sokoni hapo.

 Nilihakikishiwa na mmoja wa watendaji hao akishirikiana na baadhi ya viongozi wa soko kuwa vibanda vinapatikana, lakini kwa Sh. milioni 1.5 kwa kimoja.  

Siku chache, kabla ya wafanyabiashara hao kutimuliwa, nilizungumza na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Fortunatus Fwema, kwa njia ya simu kuhusu jambo hilo. Kimsingi, alibariki wafanyabiashara hao kufukuzwa sokoni hapo.

 Na ili kuonyesha kuwa yuko makini na hilo, siku mbili baada ya kuzungumza naye, Fwema alisaini barua za kufukuzwa wafanyabiashara hao sokoni hapo. 

Tukio la kuvunjwa makufuli, lilitanguliwa na vibanda hivyo kufungwa tangu Januari 31, mwaka huu, huku ndani yake kukiwa na bidhaa nyingi, ambazo hadi vibanda vinavunjwa tayari zilikuwa zimekwishahaharibika.

 Baadhi ya wafanyabiashara waliofukuzwa, ni wajane, wengine wanasomesha watoto. Wengine mitaji waliyokuwa nayo imetokana na mikopo waliyochukua kwenye baadhi ya mabenki na kwenye taasisi nyingine za fedha.

 Hatua ya wafanyabiashara hao kuporwa vibanda vyao, kwa mujibu wa uchunguzi, sisiti kusema kuwa ni jambo lililopangwa kwa maslahi binafsi. 

Na ndio maana Fwema alisaini barua hizo baada ya kusikiliza taarifa za watendaji wake na kupuuza madai ya wafanyabiashara hao. Madai ya wafanyabiashara hao yaliwasilishwa ofisini kwa mkurugenzi huyo kwa mdomo na kwa maandishi. 

Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, John Njunde, kwa kushirikiana na afisa mmoja katika Ofisi ya Afisa Masoko wa Manispaa hiyo, walipeleka kwa Fwema taarifa zisizo sahihi dhidi ya wafanyabiashara hao. Bila kujali madai yao, mkurugenzi akazimeza nzima nzima. 

Sikuishia hapo. Niliwasiliana kwa simu pia na Njunde. Alikiri kufunga vibanda hivyo kwa madai kwamba wafanyabiashara hao waligoma kutii maelekezo yaliyowataka walipe madeni yao. 

Njunde alidai wafanyabiashara hao walilipa madeni yao baada ya vibanda vyao kufungwa.  

Kadhalika, alidai Fwema alizuia wasirejeshewe vibanda vyao kwa madai kwamba walikiuka sheria inayotaka walipe madeni ndani ya miezi mitatu baada ya kutangaziwa kufanya hivyo.

 Hata hivyo, upo uthibitisho kwamba wafanyabiashara hao walilipa madeni yao na stakabadhi za malipo zipo. 

Pia upo uthibitisho kwamba walishindwa kulipa kwa wakati kutokana na mkusanyaji wa madeni kutoka manispaa kutokwenda sokoni kukusanya madeni kwa muda mrefu, jambo lililowafanya wakose pa kwenda kulipa madeni yao. 

Njunde alisema madai ya kuwatoza wafanyabiashara wapya Sh. milioni 1.5 badala ya malipo halali ya Sh. 15,000 ya kodi ya upangishaji wa vibanda, yana nia ya kupakana matope.

Hata hivyo, alikiri kuwapo baadhi ya wafanyabiashara waliopangishwa kwa Sh. 100,000 badala ya Sh. 15,000. Lakini akasema wanaofanya hivyo ni wafanyabiashara wenzao na si maofisa wa halmashauri.

Anachokiri hapa Njunde ni nusu ukweli. Ukweli kamili ni kwamba, sokoni Makumbusho kuna dhuluma, kuna uonevu na pia kuna unyanyasaji mkubwa dhidi ya wafanyabiashara. Pia kuna ufisadi wa kutisha. Nimeugusia hapo juu. 

Kwa nchi inayoheshimu na kuongozwa kwa misingi ya utawala bora na sheria, jambo hili kamwe haliwezi kukubalika. Halistahili kuachwa lipite.

Hivyo, uchunguzi wa kina unatakiwa ufanyike ili haki itendeke na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment