


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeahirisha kesi inayomkabili Mbunge wa Bahi mkoani Dodoma, Omary Badwel (43), ya kupokea rushwa ya Sh. milioni moja, hadi Septemba 3, mwaka huu.
Mwendesha mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Lizy Kiwia, alieleza mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Faisal Kahamba, kuwa mshitakiwa hakufika mahakamani jana kwa sababu amefiwa na dada yake.
Inadaiwa kuwa kuwa kati ya Mei 30 na Juni 2, mwaka huu katika maeneo tofauti tofauti jijini Dar es Salaam, Badwel akiwa mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), alimshawishi Mkurugenzi wa Wilaya ya Mkuranga, Sipora Liana, kutoa rushwa ya Sh milioni nane ili awashawishi wajumbe wa kamati hiyo kupitisha bajeti ya mwaka 2011/2012 ya halmashauri hiyo kazi ambayo inafanywa na mwajiri wake.
Katika shitaka la pili, inadaiwa kuwa Juni 2, mwaka huu katika Hoteli ya Peacock iliyopo katika Wilaya ya Ilala Dar es Salaam, Badwel alipokea Sh. milioni moja za rushwa.
Inadaiwa kuwa mshtakiwa alipokea fedha hizo kutoka kwa Sipora kwa lengo la kwenda kuwashawishi wajumbe wa LAAC ili wapitishe bajeti ya halmashauri hiyo.