



Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, amewaomba mameneja wa masoko nchini kuwasihi wauzaji wa vyakula katika masoko kupunguza bei ya vyakula wakati huu wa Mfungo wa Ramadhani.
Meya Silaa alitoa rai hiyo juzi jioni wakati wa futari ya pamoja iliyoandaliwa na Kamati ya Amani ya viongozi wa dini mkoani Dar es Salaam.
Hafla hiyo ambayo iliandaliwa na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Dar es Salaam na kuwakutanisha viongozi wa serikali na dini, pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi.
Meya Silaa alisema tukio hilo la kuwakutanisha viongozi wa dini na serikali na kula futari ya pamoja, linaonyesha kuwa Watanzania wote ni ndugu na wanaweza kukaa pamoja pasipo kujali udini.
Baadhi ya viongozi wa serikali walioshiriki futari hiyo ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi.
Wengine ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, Sheikh Alhab Salum na Msaidizi wa Askofu la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji George Fupe.
Katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini, Sheikh Alhab Salum, alisema madhumuni ya kuandaa futari hiyo ya pamoja ni kujenga upendo na ushirikiano miongoni mwa viongozi wa dini na Serikali.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mchungaji George Fupe, alisema tukio lililofanyika la kula futari kwa pamoja, linaonyesha nchi ipo kwenye amani na mahusiano mazuri, hivyo nchi nyingine zinapaswa kuiga mfano huo.
“Kula futari hii maana yake sote ni ndugu, tumekuja pamoja, tumekula pamoja na inatakiwa tuishi pamoja,” alisema Mchungaji Fupe.
Alisema kila mtu ana imani yake lakini isiwafanye kutengana na kusababisha nchi kuingia katika chuki na mapigano.