Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Papic alijitakia shida Yanga

21st April 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Habari zinazohusu klabu ya Yanga katika siku za karibuni zimetawaliwa zaidi na matukio nje ya uwanja na hususan rufaa za kupinga, kwanza, kufungiwa kwa wachezaji baada ya kupigwa kwa muamuzi na pingamizi la kupokonywa pointi tatu kwa kumpanga mchezaji mwenye kadi nyekundu katika mchezo wa timu yake wa ligi kuu ya Bara.

Lakini mbali na masuala ya rufaa, kuna 'kilio' cha kocha Kostadin Papic ambaye amekuwa akilalamika kutolipwa mshahara kwa miezi mitatu mfululizo ambacho nacho kinatawala habari za Yanga zaidi kuliko kiwango chake cha mchezo uwanjani mwishoni  mwa msimu huu.

Hii si mara ya kwanza kwa Papic kulalamika kwenye vyombo vya habari juu ya ama kucheleweshewa ama kutolipwa stahili zake kwa mujibu wa mkataba baina yake na klabu ya Yanga.

Si mara ya kwanza kwasababu, kama inavyofahamika na wapenzi wa soka nchini, hii si mara ya kwanza kwa Mserbia Papic kuifundisha timu hiyo.

Aliongoza jahazi la Yanga vizuri tu msimu uliopita, lakini palikuwa na malalamiko ya kuchelewa kwa mshahara na hata pale ilipokuwa ni dhahiri kwamba uongozi hautoendelea naye, palikuwa na dalili za kusotea mafao yake kabla ya kurudi nyumbani.

Katika namna ya kushangaza, kocha huyo alirudi nchini katikati ya msimu kuja kuifundisha Yanga. Tena!
Hatufahamu, Nipashe, ni kipi ambacho kilimshawishi Papic kuona kwamba pangekuwa na mabadiliko katika utaratibu wa utekelezaji wa stahiki zake ndani ya Yanga safari hii.

Lakini ambacho tuna uhakika nacho ni kuwa kocha huyo alitakiwa ajiandae na mvutano kama aliokumbana nao katika awamu yake ya kwanza, ya kuwa mwalimu wa Yanga, alipotua nchini kuchukua nafasi ya Mserbia mwenzake Dusan Kondic ambaye naye hatuna hakika kama alikamilishiwa malipo yake wakati akiondoka katika klabu hiyo.

Kama Papic alidhani kuwa Kondic alikamilishiwa malipo yake, katika awamu yake hii ya pili Mserbia huyo ambaye imeshaonekana dhahiri huduma yake haitahitajika tena Jangwani msimu ujao, alipaswa kujiuliza kama Mganda Sam Timbe ambaye alibadilishana naye kazi hiyo mara mbili aliondoka nchini akiwa haidai Yanga.

Na kama ni kweli Timbe aliondoka nchini akiwa haidai Yanga, Papic alitakiwa kufahamu kama katika historia ya Yanga hakuna waalimu marehemu ambao walitangulia mbele za haki wakiacha malalamiko kwenye vyombo vya habari juu ya kutolipwa stahili zao baada ya ama mikataba yao na Yanga kumalizika ama kutemwa na timu hiyo kongwe zaidi nchini.

Na hapa, Nipashe, tunawazungumzia hasa marehemu wawili ambao majina yao yanahusika kwa uzito mkubwa mno na historia ya mafanikio ya klabu hiyo lakini wakatendewa dharau ya ajabu.

Tambwe Leya, kocha Mkongo ambaye aliiongoza timu hiyo kwa vipindi viwili tofauti akianzia na mapema miaka ya 1970 hakupata mafanikio makubwa sana ndani ya uwanja, lakini kama mipango yake ya karibu miaka 40 iliyopita katika ujenzi wa vikosi vya klabu hiyo ingeendelezwa:

Upo uwezekano kwamba Yanga ingekuwa imeacha historia kubwa kwenye michuano ya klabu ya Afrika kwasababu ni mwalimu ambaye alifahamu umuhimu wa kuwa na timu za kuanzia Yanga kids mpaka kikosi cha kwanza.

Tambwe alirudi tena Yanga kwa shangwe kubwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 kabla ya kutimuliwa na uongozi wa Yanga na kufariki dunia akidai malimbikizo ya mishahara yake.

Mwenendo mbovu wa Yanga katika michuano ya kimataifa chini ya makocha wa kigeni wanaolipwa mishahara ya mamilio ya shilingi kwa mwezi siku hizi -- timu hupanda ndege moja kabla ya kuaga Afrika -- unaweza kukufanya usahau kuwa marehemu Tito Mwaluvanda, akiwa kocha wa muda tu, aliiwezesha timu hiyo kucheza robo-fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mara baada ya kuanza kwa nusu ya pili ya miaka ya 1990. Kwa mara ya kwanza na pekee.

Lakini kama ambavyo ilikuwa kwa Tambwe, marehemu Mwaluvanda alifariki akiwa ameacha kwenye vyombo vya habari kilio cha kutolipwa stahili zake nyingi zitokanazo na posho alizotakiwa kulipwa kwa kuwa 'dei waka'.

Bahati mbaya sana, vitendo vya ukiukwaji wa maslahi ya wanamichezo kwa mujibu wa mikataba yao haviishii kwa Yanga tu. Ni utamaduni nchini, sasa, maana pamoja na kwingineko, Moses Basena ameendelea kuvutana na Simba zaidi ya miezi minne tangu atemwe.

Lakini bahati mbaya zaidi ni kuwa mmoja wa waathirika wa ukiukwaji huo wa mikataba ya ajira amerudi kunasa katika mtego ule ule, na kwenye 'mti' ule ule.

Ndipo hapo Nipashe tunapojiuliza kama kilio cha Papic kwenye vyombo vya habari sasa si cha kujitakia.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles