Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mgwima, imulike TRA inatukwaza, inasononesha!

13th May 2012
Print
Comments

Mawaziri wapya walioteuliwa, kisha kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete, wameanza kazi na kuahidi kutekeleza majukumu yao kwa maslahi ya umma.

Ninawapongeza, ingawa katika nadharia ya kawaida, sehemu ya umma wa Watanzania haijajiaminisha kwamba ‘wanaweza’.

Kwa maana hata waliovurunda kabla yao, waliahidi ‘kufanya maajabu ya kiutendaji’ walipoteuliwa, lakini wameondoka kwa aibu!

Changamoto iliyopo ni kwamba, mawaziri wapya na wale waliokuwepo awali ambao hawakuguswa na kashfa zilizowafukuzisha kazi wenzao, watatembea juu ya maneno?

Ama hawatazisoma alama za nyakati kiasi cha kusubiri kufukuzwa, na pengine kufikishwa mahakamani kwa sababu za ubadhirifu wa fedha na mali za umma?

Mmoja wa mawaziri walioteuliwa katika orodha mpya ni Dk William Mgimwa, atakayehudumu katika Wizara ya Fedha na Uchumi. Ninampongeza.

Dk Mgimwa ni miongoni mwa mawaziri waliokabidhiwa dhamana kubwa kuiongoza wizara nyeti katika mustakabali wa uchumi wa nchi. Wizara hiyo ni hazina ya taifa.

Ni wizara yenye ‘wanjanja’ wengi, wale wanaotumia elimu, uzoefu na taaluma zao ‘kupenyeza’ mambo ya hovyo ili yahalalishe uporaji wa fedha za umma, wakajilimbikizie wao, familia zao, ndugu zao na wengine walio katika shirika nao.

Watu wanaocheza mchezo mchafu kwenye wizara hiyo wamekuwepo kwa vipindi vinavyotofautiana kwa utumishi, lakini wakiwa wanachama wa mtandao wa ‘wizi’ na uporaji wa fedha na mali za umma.

Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh imeweka bayana. Inasomeka.

Katikati ya hali hiyo, `wajanja’ hao katika tasnia isiyo rasmi ya nia ovu kwa umma, wamejiwekea mtandao unaogusa matumizi makubwa ya fedha na kuendeleza tafsiri ya ‘penye udhia penyeza rupia’.

Dk Mgimwa asipokuwa makini, atajikuta amekuwa udhia kwa mtandao huo, hivyo njia pekee itakuwa ni kupenyeza rupia, ataweza kuuruka mtego? Namtakia kila la heri.

Kwa upande mwingine, Mgimwa anapaswa kutambua kwamba utoaji taarifa sahihi, tena kwa uwazi na ukweli kuhusu mwenendo na mambo yanayohusiana na uchumi ni jambo muhimu kwa raia.

Halitokani na hisani bali ni moja ya haki za msingi kwa raia, wakiwa wamiliki wa taifa hili.

Moja ya maeneo muhimu katika hitaji la kupatikana kwa taarifa hizo ni Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), iliyopewa jukumu la kukusanya kodi, zikitokana na kazi ama huduma zinazotolewa nchini.

Taifa lolote duniani linategemea kodi, kwanza inayotokana na wananchi wake, ili kufanikisha mipango ya maendeleo na ustawi wa nchi na watu wake.

Lakini kwa muda mrefu sasa, TRA imekuwa mfano wa kikwazo kikuu katika utoaji wa taarifa kwa umma, hasa kupitia vyombo vya habari.

Kwa mamlaka hiyo, taarifa zinazotakiwa na umma kupitia vyombo vya habari zimekuwa siri, tena mithili ya siri iliyo kuu.

Imekuwa desturi kwa mamlaka hiyo ‘kupiga kalenda’ pale vyombo vya habari vinapotekeleza wajibu wake wa kikatiba, kuutumikia umma kwa njia ya upashaji taarifa.

Ikiwa moja ya taasisi za umma zinazohifadhi taarifa nyeti za taifa, vyombo vya habari vinalitambua hilo, lakini haiwezekani hoja hiyo, tena katika zama hizi ambapo wigo wa ‘kuvuja’ kwa taarifa umekuwa mpana zaidi, TRA kuendelea na uhafidhina wa kuficha taarifa.

Wapo waandishi wengi kwa idadi yao, wametoa shuhuda kupitia mijumuiko mbalimbali, jinsi wanavyokwazwa na maofisa wa TRA pindi wanapohitaji taarifa.

Hata taarifa zilizo na maana pana na zinazojenga taswira chanya ya serikali kwa jamii, lakini hawazitoi, wamezikumbatia. Kuna nini?

Kasumba iliyojengeka katika TRA ni kutoa agizo kwa waandishi wa habari, kuwasilisha maswali kwa njia ya maandishi, hitaji ambalo linatekelezwa kwa umakini na haraka.

Lakini hata inapofanyika hivyo, bado waandishi wa habari wamekuwa wakitakiwa kufuatilia majawabu pasipo mafanikio.

Safari ya ‘nenda rudi TRA’ imekuwa jambo linaloibua kero iliyo miongoni mwa kero kuu kwa waandishi wa habari.

Hali hiyo imesababisha miongoni mwa waandishi wamejikuta wanachoka, wanakwazika, wanaishiwa nguvu, wanasononeka, wanakata tamaa na kuamua kuyaacha maswali ya umma ‘yakiozea’ TRA.

Utaratibu wa kutoa taarifa kwa njia ya tangazo maalum ni wa kawaida kama inavyofanyika kwa taasisi yoyote, hivyo TRA haiwezi kukimbilia huko na kujenga msingi wa hoja yenye mashiko kwamba wamekuwa wakifanya hivyo mara kwa mara.

Zipo taarifa nyingine, mathalani zinazohusisha ukwepaji kodi, ulinganifu wa mapato na bidhaa za aina fulani zinazoingizwa kutoka nje, nakdhalika.

Lakini hata pale inapohitajika takwimu ya makusanyo kutoka vyanzo tofauti ndani ya kipindi fulani cha mwaka, kwa TRA imekuwa ‘ngoma nzito’. Kuna nini?

Bila shaka Mgimwa anaingia, akiwa na dhamira ya kukiepuka ‘kikombe cha Mustafa Mkulo’ kisimfike, hivyo kuwa tayari kuvumilia jambo lolote linalomstahili.

Lakini isiwe kuhujumu, kufisadi ama kushiriki ubadhirifu wa mali na fedha za umma.

Wakati akiwa katika njia hiyo iliyo nyembamba kwa watumishi wa umma walio wengi, Mgimwa anatakiwa kukumbuka umuhimu wa upashaji habari kwa umma, kwamba kupitia vyombo vya habari, umma unastahili kujua kinachotokea kwa ‘makaisari’ wanaokusanya kodi.

Kwa kushiriki hilo, ninamsihi asisite, asione haya, asiogope kuishughulikia TRA katika kadhia nzima ya ufichaji na usumbufu wa kutoa taarifa kwa umma.

Hilo litafanikiwa kwa kulegeza masharti ‘mazito’ ya mamlaka hiyo kwa waandishi wa habari wanaoutumikia umma kwa nia iliyo njema.

Kwa pamoja tutashinda.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE.Anapatikana kwenye simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe:[email protected]

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles