Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Waliotemwa uwaziri wahojiwa Takukuru

22nd May 2012
Print
Comments
  Asilimia 90 wamekwisha kuchukiliwa maelezo
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imeshawahoji asilimia 90 ya Mawaziri wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha  za umma katika wizara zilizotajwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Akizungumza na NIPASHE ofisini kwake jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, alisema baadhi ya mawaziri waliotuhumiwa wamekwisha kuhojiwa na uchunguzi bado unaendelea dhidi yao.

Hata hivyo, Dk. Hoseah, alisema suala la kuwachunguza mawaziri hao siyo la kukurupuka kama baadhi ya watu wanavyofikiri kwani lazima lichukue muda kwa kuwa wanaangalia mambo mbalimbali ikiwemo haki za binadamu.

Alisema mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji utashi wa kisiasa na taasisi yake inafanya kazi bila ya kuingiliwa na jitihada za kuunga mkono mapambano dhidi ya rushwa zimeonekana.

Mawaziri hao ambao waliachwa katika baraza la mawaziri  lililotangazwa na Rais Jakaya Kikwete Mei 4, mwaka huu, jana NIPASHE liliwatafuta kwa simu kuulizwa kama wamehojiwa na Takukuru na kujibu ifuatavyo:

MKULO


Mmoja wa mawaziri aliyetemwa ni Mustafa Mkulo (Fedha): “Mimi sina habari hiyo, si msemaji wa Takukuru, waulize wenyewe Takukuru.”

MAIGE

Waziri mwingine aliyetemwa, ni Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii): “Sizungumzi sasa hivi na vyombo vya habari.”

Alipotakiwa kueleza sababu za kutozungumza na vyombo vya habari, Maige ambaye ni Mbunge wa Msalala (CCM), hakujibu, badala yake alisema hana habari zozote za kueleza iwapo alihojiwa na Takukuru au la.

“Habari hiyo sinayo, lakini sizungumzi na vyombo vya habari, ahsante,” alisema Maige kisha akakata simu.

NUNDU

Aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, alipopigiwa simu yake ya mkononi, alipokea na mwandishi alijitambulisha, lakini kabla hajaulizwa swali, alisema: “Siongei na mtu wa magazeti tafadhali. Kwa heri. Ahsante.” kisha akakata simu.

NGELEJA


Hata hivyo, wakati mawaziri hao walioachwa wakisema hayo, hadi tunakwenda mitamboni, simu ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, mara zote ilipopigwa ilikuwa ikiita bila kujibiwa.

DK. CHAMI

Pia aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, alipopigiwa, mara zote simu yake iliita, lakini haikujibiwa na baadaye ikazimwa kabisa.

DK. NKYA

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya, alisema: Sijawahi kupokea simu wala barua kutoka Takukuru kwenda kuhojiwa.”

DK. MFUTAKAMBA, DK. MPONDA


Aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Athumani Mfutakamba  simu zao jana zilizimwa kabisa.

Ripoti ya CAG na taarifa za  kamati za kudumu za Bunge za Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali (PAC) na Serikali za Mitaa (LAAC) ziliwataja baadhi ya mawaziri kuhusika katika ufujaji wa fedha za umma na wengine kushindwa kusimamia wizara na taasisi zao na kuisababishia serikali hasara.

Pia ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ilimtuhumu Maige katika mchakato wa kugawa vitalu vya uwindaji wa kitalii, akidaiwa kuruhusu kampuni ambazo hazikuomba vitalu kupewa kinyume cha sheria na kanuni na usafirishaji wa wanyama hai nje ya nchi.

Mkulo anadaiwa kuhusika katika ubadhirifu wa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC). Alitajwa kuwa amepoteza uaminifu na uadilifu kiasi cha kusema uongo bungeni ili kuficha maslahi binafsi katika ofisi za umma.

Dk. Chami, alitajwa kuhusika katika kumkingia kifua aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Charles Ekelege, kutokana na kusema uongo katika kazi ya ukaguzi wa magari nje ya nchi.

Ekelege anadaiwa kusema uongo kuwa kuna kampuni zimepewa kazi ya kukagua magari yanayokuja nchini nje ya nchi, ambayo yanalipwa mamilioni ya fedha, lakini kamati ya wabunge iliyokwenda nchi za Singapore na Hong Kong, hawakukuta kampuni hizo.

Mwishoni mwa wiki Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, alitangaza kumsimamisha kazi Ekelege kupisha uchunguzi dhidi yake.

Dk. Mponda anadaiwa kushindwa kusimamia matumizi bora ya fedha za umma kiasi cha kuruhusu nyumba yake kukarabatiwa kwa mamilioni ya fedha.

Ngeleja, anatuhumiwa kwa kushindwa kusimamia sekta ya madini na umeme, kuweko kwa manunuzi makubwa ya mafuta ya kuendesha mitambo ya IPTL ambayo yameongezwa bei.

Nundu, anatuhumiwa kuingilia mchakato wa kumpata mzabuni wa kujenga gati namba 12 na 13 katika Bandari ya Dar es Salaam.

TAKUKURU YAOKOA SH. BILIONI 2

Tatika hatua nyingine, Takukuru imeokoa Sh. bilioni 2.45 kwa wakurugenzi wa majiji na manispaa mbalimbali nchini kwa kuwabana na kuwaamuru kuzirudisha baada ya kubainika kuwa zilitumika vibaya katika mwaka wa fedha 2009/2010.

Dk. Hoseah, alisema jitihada hizo zimefanywa na Takukuru baada ya kuwabana jumla wakurugenzi 87 kati yao 39 ndiwo wamerejesha fedha hizo Hazina.

Alisema wakurugenzi wengine 48 bado hawajarejesha fedha hizo na wataendelea kuwabana na wakishindwa kuzirudisha fedha hizo ifikapo mwishoni mwa mwezi huu watafikishwa mahakamani.

Dk. Hoseah alisema taasisi yake imekuwa ikifanya kazi kubwa katika kuokoa fedha za umma na kupambana na watu wanajihusisha na rushwa, lakini kuna baadhi ya watu wanaiona taasisi hiyo haifanyi kazi yoyote.

“Taasisi yangu inafanya kazi kubwa sana ndio maana tumeokoa kiasi hicho cha fedha na baadhi ya wakurugenzi  ambao hawajarejesha fedha hizo wanahaha wakitafuta pesa hizo kwa kuwa mwisho wa mwezi huu tutawapeleka mahakamani wakishindwa kulipa,” alisema Dk. Hoseah

TAHADHARI DHIDI YA MATAPELI

Wakati huo huo, Takukuru imewatahadharisha wananchi dhidi ya wimbi la matapeli ambao wamekuwa wakijifanya maafisa wa taasisi hiyo na kuwadanganya watu mbalimbali kuwa wanatuhuniwa kwa makosa ya rushwa na kuwadai hongo ili wawaachie.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Uhusiano ya Takukuru jana, watu hao wamekuwa wakiwafuatilia baadhi ya watumishi wa umma waliotajwa katika ripoti ya CAG wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali.

Taarifa hiyo ya Takukuru ilisema mtu yeyote atakayehitajika na Takukuru kwa uchunguzi au ushahidi watamuhita ofisini kwa utaratibu maalum kwa kuandikiwa barua au hati ya wito na siyo kuhojiwa mitaani kama matapeli hao wanavyofanya.

Taarifa hiyo imemtaka mtu mwenye kufahamu watu wa namna hiyo atoe taarifa katika ofisi za taasisi hiyo au polisi kwa kuwa matapeli hao wanaharibu sifa ya chombo hicho.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles