


Wabunge wanaotoka mikoa inayolimwa pamba nchini wameitaka Serikali kumfukuza Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba nchini, kwa sababu ni diktekta na mtu hatari katika maendeleo ya sekta ya pamba.
Walikuwa wakichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa mwaka 2012/13 bungeni mjini Dodoma jana.
Mbunge wa Busega (CCM), Dk Titus Kamani, alisema, “Tatizo mheshimiwa Naibu Spika, ni mkurugenzi wa bodi ya pamba ni diktekta ni mtu hatari anaweka masharti ili wanunuzi wengi wasiweze kuingia katika soko la pamba,” alisema.
Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli, alisema mkurugenzi wa bodi ya pamba ameshindwa kutekeleza kazi anazowajibika kufanya.
Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo, alisema wizara imeshindwa kuwakumbuka na kuwasaidia wakulima wa pamba hapa nchini.
Alisema iwapo serikali haitaangalia upya suala hilo, wapo tayari kuongozana na wakulima kwenda mahakamani kuwashtaki wafanyabiashara wote walioingia mkataba na serikali na kufanya pamba kununuliwa kwa bei ya chini.
Akitoa hoja ya wabunge wanaolima zao hilo, Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, alisema wakulima wameamua kuendelea kuishikilia pamba ya Sh 660 kwa kilo.
“Ukikokotoa gharama zote mkulima anajikuta anapata hasara. Inakadiriwa kuwa ekari moja hutoa kilo 300 tu na kuzalisha kilo moja ya pamba kwa sasa ni zaidi ya Sh. 900. Gharama ya kutunza eka moja ya pamba ni Sh. 285,000, wakati mapato yanayotarajiwa kwa bei ya Sh 660, kwa kilo ni Sh 198,800 tu, hivyo kumfanya mkulima apate hasara ya Sh 86,200 kwa kila ekari,” alisema.
Alisema hasara hii ni kubwa na inadidimiza wakulima, inachochea umasikini, wanashindwa kusomesha watoto, wanashindwa kulipa madeni ya pembejeo, wanashindwa kununua chakula na kujipatia mahitaji mengine muhimu.
Mpina alisema jumla ya watu milioni 16 wanategemea zao hili katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Tabora, Simiyu, Mara, Morogoro, Singida,Tanga na Dodoma na kwamba bei ya zao hilo katika soko la dunia imekuwa ikipungua kila wakulima wanapoanza kuuza pamba na kupanda msimu unapoelekea mwishoni.
Pamoja na mapendekezo mengine wabunge hao walipendekeza Serikali ifidie kiasi cha shilingi 340 ili kuifanya bei kufikia shilingi 1000 kwa kilo, ambayo kwa manunuzi ya tani 300,000 itagharimu shilingi bilioni 102.
Akihitimisha hoja hiyo, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, alisema yeye ni mmojawapo wa wakulima wa pamba na anatambua changamoto katika kilimo cha zao hilo.
Aliwataka wabunge kumpa muda ili aweze kushughulikia changamoto hizo kwa kuwa tangu ateuliwe ni miezi miwili tu imepita.
Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa na Bunge jumla ya shilingi 237,624,575,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo kwa mwaka 2012/13.