Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Waziri kijana aliyekwama kufungua njia

6th May 2012
Print
Comments
Ezekiel Maige

Kama kuna dhana inayozungumzwa sana katika siasa za sasa ni ushiriki wa vijana katika nafasi za uongozi.

Vijana wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu, kwamba wanazibiwa nafasi na wazee, hivyo kushindwa kupata nafasi ya kuonyesha na kudhihiridha uwezo wao.

Mwaka 2005, Ezekiel Maige  ambaye kumbukumbu za mtandao zinaonyesha alizaliwa Machi 28, 1970, alijitokeza na kutangaza kuwania ubunge wa jimbo la Msalala mkoani Shinyanga, akijaribu kumuondoa Mbunge aliyekuwepo kwa wakati huo, Emmanuel Enock Kipole.

Sina kumbukumbu sahihi kuhusu mahali alipotokea Maige kabla ya kujitosa kwenye siasa, lakini kilichojulikana sana kwa wakati huo, ni ushindani mkali uliokuwepo katika kuwania nafasi ya kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi kuwania kiti hicho.

Ushindani huo ulionekana kuwahusisha wagombea vijana wawili, Maige na Kipole, lakini zaidi Maige alionekana kuungwa mkono na walio wengi ndani ya CCM.

Kwa upande wake, Kipole alionekana kukosolewa kwa kutotekeleza ahadi zake, hivyo katika kujenga hoja za ushawishi ikawa kazi ngumu ikilinganishwa na mshindani wake, Maige.

Hata kura za maoni zilipopigwa, Maige alishinda akiwa mmoja wa vijana waliotajwa kuchochea kasi ya ushiriki wa kada hiyo kwenye uongozi na uwakilishi.

Akiwa katika awamu ya kwanza ya uwakilishi wake, baada ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na kuwa Mbunge wa Msalala, Maige alifanikiwa kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Wakati huo, wizara hiyo ilikuwa inaongozwa na Waziri wake, Shamsa Mwangunga ambaye hata hivyo hakufanikiwa kuchaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Kuteuliwa kwa Maige kuwa Naibu Waziri kulifanyika baada ya Rais Jakaya Kikwete kulivunja Baraza la Mawaziri, kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa Februari, 2008.

Uteuzi wa Maige akiwa katika awamu ya kwanza ya uwakilishi wake bungeni, ilikuwa moja ya mafanikio kwa kada ya vijana, hivyo kilichotakiwa ni kuonyesha namna anavyoweza kudhihirisha ushiriki wake wenye maslahi mapana ya umma.

Hatua ya Maige kuwa Naibu Waziri chini ya Waziri Mwangunga ambaye vyanzo vya taarifa za kielektroniki vinaonyesha alizaliwa Desemba 3, 1953, ilikuwa fursa pana ya kuonyesha tofauti za kiutendaji.

“Maige alikuwa kijana ikilinganishwa na Mwangunga, hivyo tulitarajia aonyeshe njia nzuri itakayochochea kasi ya vijana kuingia kwenye siasa na uongozi,” anasema mwanaharakati wa haki na maendeleo ya vijana, Paschalia James.

Hata hivyo, baada ya kuitumikia nafasi ya Naibu Waziri hadi Uchaguzi Mkuu ulipofanyika mwaka 2010 ambapo alichaguliwa kwa mara ya pili kuwa Mbunge wa Msalala, Maige anatajwa kuwa miongoni mwa viongozi waliokuwa na mvuto mkubwa kwa vijana.

Kwenye mitandao ya kijamii, Maige alitajwa mara kadhaa na wakati mwingine alichangia hoja zikihusiana na masuala mbalimbali ya kijamii.

Rais Jakaya Kikwete alipomteua kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, nyota ya Maige ilizidi kung’ara huku akitolewa kuwa mfano wa viongozi vijana, wanaotekeleza wajibu wao katika sekta inayoongoza kwa kuingiza fedha za kigeni.

“Kitendo cha Rais Kikwete kumuweka Maige katika wizara nyeti ya maliasili na utalii, ilitufariji sana vijana, tukamuona kama mtu anayefungua mlango kwa jamii ili kudhihirisha kwamba vijana wanaweza,” anasema Silvano Isdori, mhamasishaji wa vijana kwenye moja ya vyama vilivyo chini ya Kanisa Katoliki, jimbo kuu la Dar es Salaam.

Isdory anasema kitendo cha Maige kukabiliwa na kashfa za ubadhirifu wa mali za umma, kimerudisha nyuma ari ya vijana na kupunguza imani ya wananchi kwa kada hiyo.

“Tuna vijana wengi katika uongozi na uwakilishi wa wananchi na wanafanya vizuri hadi sasa tunakubalika, isipokuwa hili la Maige aliyekuwa mfano wa kioo bora kwa vijana, halitoi taswira nzuri,” anasema.

Maige amekuwa miongoni mwa mawaziri waliofukuzwa kazi na Rais Kikwete, akiwa mmoja wa walioshambuliwa sana wakati wa mijadala ya Bunge katika mkutano wake wa saba mjini Dodoma.

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, iliibua tuhuma dhidi ya Maige, kiasi cha kuitaka serikali imuwajibishe.

Taarifa ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa shughuli zake katika kipindi cha Aprili, 2011 hadi Aprili 2012, ilisomwa na Mwenyekiti wake, James Lembeli ambapo tuhuma kadhaa zilimuelekea maige.

Mathalani, Lembeli akasema uchunguzi wa kamati hiyo ulibaini mchakato wa ugawaji vitalu ulikuwa na dosari nyingi ikiwamo waziri kutangaza majina ya waliopatiwa vitalu bila kuvionyesha wala kutaja idadi kamili.

Pia kamati hiyo ya Bunge ikaeleza kuwa baadhi ya kampuni ziligawiwa vitalu kinyume na sheria na ushauri wa kamati ya kumshauri waziri kulingana na sifa na vigezo ikiwamo makampuni matatu.

“Maliasili ni eneo nyeti linalotegemewa na taifa lakini zaidi sisi vijana, sasa kama anatokea waziri aliye kijana mwenzetu anaihujumu, tena kwa taarifa zinazotolewa bungeni, inatuvunja moyo,” anasema isdory.

Lembeli akisoma taarifa hiyo akasema kampuni 16 ziligawiwa vitalu vya daraja la kwanza na la pili ambavyo havikuombwa wakati kulikuwa na kampuni za kizalendo zilizokuwa na vigezo. Moja ya mapendekezo ya kamati hiyo yakasomeka, “Kamati ya Bunge inapendekeza kwamba Bunge liitake serikali kumwajibisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, kwa kutengeneza mazingira ya rushwa ikiwa ni pamoja na kuyanyang’anya makampuni 16 vitalu vilivyogawiwa.

Hata hivyo Maige anabaki kuwa Mbunge wa Msalala anayeweza kutumia fursa hiyo kurejesha imani yake kwa vijana akipitia fursa mbalimbali za kisiasa na kijamii.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles