Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Hukumu kesi ya Dk. Makongoro Mahanga leo

2nd May 2012
Print
Comments
Mbunge wa Segerea Dk. Makongoro Mahanga (CCM).

Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, leo inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya kupinga matokeo ya ushindi wa mbunge wa Segerea Dk. Makongoro Mahanga (CCM).

Kesi hiyo ilifunguliwa na  mgombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Fred Mpendazoe, na kuhumu hiyo inatolewa baada ya kusikiliza mashahidi 15 wa mlalamikaji na 16 upande wa walalamikiwa. Hukumu hiyo itasomwa na Jaji Profesa Ibrahim Juma aliyesikiliza kesi hiyo.

Mpendazoe aliwashitaki Mwanasheria Mkuu wa serikali, Dk. Mahanga na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kwa madai ya kukiuka taratibu za uchaguzi wa mwaka 2010.

Katika ushahidi Mpendazoe alidai kura za ubunge katika kata ya Kiwalani, hazikufanyiwa majumuisho na kwamba baada ya upigaji kura kumalizika wasimamizi wasaidizi walianzisha vurugu wakidai posho zao.

Kadhalika, alidai kitendo hicho kilichodumu kwa saa nne, kilisababisha zoezi la kuhesabu kura kutofanyika na askari polisi waliwafukuwa mawakala katika ofisi za kata palipokuwa pamehifadhiwa maboksi ya kura.

Akiongozwa na wakili upande wa mlalamikaji, Peter Kibatala, shahidi huyo alidai kuwa Oktoba 31, 2010, saa 2:00 hadi saa 6:00 usiku wasimamizi wasaidizi walifanya vurugu katika Kata ya Kiwalani kudai posho zao.
Aidha, baada ya tukio hilo askari polisi waliwafukuza mawakala na kuwaamuru warejee kesho yake baada ya kubainika kuwa fomu za vituo 23 za ubunge hazikuwepo.

Alidai kuwa siku ya Novemba Mosi na pili, 2010 zilionekana fomu saba na kubaki 16 ambazo hazikujazwa majumuisho ya kura za wagombea ubunge. Aidha, alidai kuwa aliyenufaika na ukiukwaji huo wa sheria ni Dk. Mahanga.

Naye shahidi wa pili wa upande wa mlalamikaji Gervas Barandaje (29), alidai kuwa Nec ilichochea vurugu na kusababisha ofisi ya Ofisa Mtendaji kuchomwa moto Novemba 2, mwaka 2010 baada ya kuhamisha masanduku na vifaa vya kupigia kura bila kutangaza mshindi wa kiti cha udiwani Kata ya Kiwalani.

Shahidi mwingine wa Mpendazoe ni, Livingstone Rugema (31), alidai kuwa, aliyekuwa Meneja Kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alishirikiana na Mkurugenzi wa Uchaguzi Jimbo la Segerea kuchakachua kura.

Alidai kuwa Novemba 2, 2010 saa 2:00 usiku Kinana alikwenda Arnatouglo ambapo aliingia kwenye ukumbi wa jengo hilo akiambatana na msimamizi wa wa uchaguzi wa jimbo la segerea  wakaingia kwenye gari na kuondoka.

Naye Dk. Mahanga katika ushahidi wake alikirikwamba udaktari wake haujawahi kutambuliwa na Taasisi Maalum  ya Serikali Tanzania, kutokana na kutokuwa na sababu ya kufanya utambuzi huo. Dk. Mahanga alidai  kwamba kama utaratibu wa uchaguzi ulikiukwa unatia dosari uhalali wa ubunge wake.

Shahidi wa sita wa Mpendazoe, Samwel Bubegwa (49), alidai kuwa majumuisho ya kura katika jimbo hilo yalifanyika  bila kutatua kura za migogoro.

Shahidi huyo ambaye alikuwa Msimamizi Msaidizi wa Jimbo la Segerea, alidai kuwa baada ya zoezi la uchaguzi kumalizika Novemba 2, mwaka 2010, walihamishia vifaa vya kura Arnatouglo kwa ajili ya kufanya majumuisho ya kura za urais na ubunge.

Shahidi mwingine wa upande wa walalamikiwa, Omary Mhando, alikiri kuvunja sheria ya uchaguzi wa mwaka 2010 kwa kutosaini fomu za matokeo ya kura za urais, ubunge na udiwani baada ya kuacha kusaini kwa madai kuwa walikuwa na uchovu siku hiyo ya uchaguzi. Mhando alikuwa  Msimamizi Msaidizi wa kituo cha Kombo 4A.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles