


.jpg)
Baada ya kutetea taji lake la taifa wa TPBO kwa kumnyuka Msiaha Samson kwa KO, bondia machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Thomas Mashali amesema anataka kuzipigana na Japhet Kaseba au Francis Cheka.
Mashali aliyetetea taji hilo wiki iliyopita kwa kumpiga Samson kwa KO ya raundi ya tano, alisema ni zamu ya kupata mchezo dhidi ya Cheka au Kaseba ambao wanatarajia kupigana Julai 7 jijini Dar.
Bondia huyo anayefahamika kama 'Simba Asiyefugika', alisema yeyote kati ya Cheka na Kaseba atakayeibuka na ushindi atakuwa radhi kupigana nae ili kuendeleza ubabe katika uzani wa Middle anaoushikilia taaji la taifa.
"Nashukuru Mungu nimefanikiwa kumbamiza Samson aliyejiuzulu mwenyewe katika raundi ya tano na sasa ni zamu ya kupata nafasi ya kupigana na mshindi wa pambano la Julai 7 kati ya Francis Cheka ama Japhet Kaseba," alisema.
Mashali alisema anadhani mmojawapo kati ya mabondia hao watasaidia kumpa upinzani wa kweli na kuanza safari yake ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa katika mchezo huo akiota kuja kutwaa ubingwa wa dunia.
Bondia huyo alitwaa taji hilo la TPBO mapema mwaka huu kwa kumchakaza Said Seleman 'Galile' na kulazimika kutetea wiki iliyopita ambapo kabla ya kupanda ulingoni mpinzania wake, alitamba angemtwanga kwa aibu.