Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mwakosya: Balali aliidhinisha fedha za EPA

31st July 2012
Print
Comments
Aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Daud Balali

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imeambiwa na mshtakiwa Imani Mwakosya (54) kuwa mchakato na malipo ya Sh. Bilioni 3.8 za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa) kupitia kampuni ya Mibale Farm iliyohamishiwa deni Kampuni ya Lakshmi Textile Mills Ltd ya India yalikuwa halali kwa sababu yaliidhinishwa na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Daud Balali.

Kadhalika, Mahakama imeambiwa kuwa malipo hayo yalikuwa halali kwa sababu nyaraka zote za kudai deni hilo yalikuwa sahihi na Gavana aliidhinisha na kuelekeza malipo yafanyike.

Mwakosya aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Madeni ya Nje BoT, alitoa ushahidi wake jana mbele ya jopo la mahakimu watatu wakiongozwa na Mwenyekiti wake Samwel Karua na Beatrice Mutungi Majaji wa Mahakama Kuu Tanzania,  ambao wamepewa kibali cha kuendelea kusikiliza kesi hiyo na Jaji Mkuu na Hakimu Mkazi Mfawidhi Illivin Mgeta.

Akiongozwa na wakili wa utetezi, Majura Magafu, shahidi huyo wa sita wa upande wa utetezi alidai kuwa anaifahamu kampuni ya Mibale Farm kwa sababu alishughulikia mchakato wa malipo ya Sh. bilioni 3.8 baada ya hati za kuonyesha kuwa wamehamishiwa deni na Kampuni ya Lakshmi Textile Mills Ltd ya India.

Alidai kuwa nyaraka zote za malipo ya deni hilo yalianzia kwa Gavana na baadaye kufikishwa kwenye kitengo chao ambapo walihakiki kwenye mtandao wa BoT na kuona kweli deni la kampuni hiyo ya India lipo.

“Baada ya kuhakiki niliandika dokezo kwenda kwa Mwanasheria wa BoT ambaye alikuwa ana wajibu wa kumjulisha Gavana kama nyaraka hizo ziko sahihi kisheria kufanyiwa malipo naye kama bosi wa BoT aliidhinisha malipo hayo yafanyike,” alidai Mwakosya.

Alidai kuwa malipo hayo ni halali Balali alisaini nyaraka za kuidhinisha malipo hayo Oktoba 20, mwaka 2005 ambapo kampuni ya Mibale ililipwa Sh. 3,868,805,737.13.

“Waheshimiwa naomba mahakama hii inifutie mashtaka kwa sababu mashtaka haya yanayonikabili sio kweli na kwamba malipo niliyoshughulikia kupitia wadhifa wangu yalikuwa halali,” alidai Mwakosya.

Upande wa utetezi ulifunga ushahidi wake ambapo Agosti 29, mwaka huu pande zote zitawasilisha hoja za kama washtakiwa wana hatia au la.

Hakimu Karua alisema hukumu ya kesi hiyo itatolewa Oktoba 17, mwaka huu.

Mbali na mwakosya, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Rajabu Maranda, Farijala Hussein, Ajay Soman, Esther Komu na Sophia Lalika,

Katika kesi hiyo, washtakiwa wanadaiwa kula njama na wizi wa Sh. 3,868,805,737.13 mali ya BoT baada ya kudanganya kuwa kampuni ya Kampuni ya Mibale Farm imehamishiwa deni Kampuni ya Lakshmi Textile Mills Ltd ya India.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment