Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Hoja si udhamini wa mabilioni Stars

12th May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Kampuni ya Bia, TBL, na shirikisho la soka, TFF, wiki hii zimeingia mkataba wa dola za Marekani milioni 10 (sawa na sh. bilioni 15.5) wa kuidhamini timu ya taifa, Taifa Stars, kwa miaka mitatu ijayo.

Mkataba huo, TBL imedai, utagusa maeneo kadhaa kama kuimarisha kambi za mazoezi, kununua vifaa vya kisasa vya michezo na kuhakikisha Taifa Stars inapata mechi nyingi za kirafki.

Aidha, TBL imedai, itaipatia Taifa Stars basi kubwa la kisasa, lenye bodi ya 'Marco Polo' pengine, ili kuachana na kupanda 'Coaster' la sasa na kulaza wachezaji wa timu hiyo katika hoteli ya nyota tatu kila wawapo kambini.

TBL pia imedai kuwa udhamini huo, ambao ni sh. bilioni 3.1 kwa mwaka utatumika katika kutoa mafunzo kwa wafanyakazi (wa TFF, Nipashe tunadhani), uendeshaji wa tovuti (ya TFF, Nipashe tunadhani) na kuwezesha watendaji wa TFF ambayo inapata si chini ya dola 250,000 za Marekani kila mwaka kuhudhuria semina na mikutano ya utawala bora ndani na nje ya nchi.

Udhamini wa TBL pia, kwa mujibu wa TFF, utasaidia kuongeza mara dufu posho za wachezaji wa Taifa Stars wawapo kambini.

Hata kwa mujibu wa TFF, ni mkataba ambao utainua hamasa kwa wachezaji wa Taifa Stars hivyo kupelekea timu kufanya vizuri. Siyo?

Hapana. Hapana kwasababu kwa mtazamo wetu, Nipashe, mafanikio ya Taifa Stars hayatatokana na wingi wa fedha ndani ya mkataba huo baina ya TBL na TFF kama inavyoweza kudhaniwa.

Msingi wa mafanikio ya Taifa Stars, tuna hakika Nipashe, utakuwa katika kiwango cha UWAZI katika matumizi ya vipengele vilivyomo katika mkataba huo, utakaoonyeshwa na pande hizo mbili kwa umma.

Tunafahamu Nipashe kuwa kisheria maudhui ya mkataba huwa ni siri baina ya pande zilizoamua kuingia mkataba husika, kwa gharama yoyote wakati mwingine.

Lakini wakati mkataba baina ya TBL na TFF ukitangazwa, tulitaraji kwamba shirikisho la soka hilo lingekuwa limejifunza gharama zinazotokana usiri ulio katika mkataba wa udhamini wa ligi kuu.

Tumeona katika udhamini huo wa zaidi ya miaka mitano iliyopita kwamba licha ya kiasi kikubwa, kwa ulinganifu, cha fedha kinachotolewa kila msimu bado kuna malalamiko lukuki kutoka kwa timu shiriki.

Lakini ambacho tumejifunza kutokana na malalamiko lukuki kutoka kwa timu shiriki, na ambacho Nipashe tulitaraji TFF ingekuwa imejifunza kutokana na malalamiko hayo luluki ni ubaya wa USIRI huo.

Ni kweli kwamba kuna ahadi ya ongezeko mara dufu la posho za wachezaji wa Taifa Stars kulinganisha na kipindi kilichopita.

Lakini ambacho bado kinaweza kudidimiza morali ya wachezaji wa Taifa Stars na hivyo nchi kuendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu katika michezo ya kimataifa ni, kwa mfano, kutofahamu kwao jumla ya fungu la posho hizo ni asilimia ngapi ya jumla ya udhamini mzima unaotolewa.

Morali inaweza isipande pia kama wachezaji watakuja kufahamu kwamba fungu la posho zao lililopanda ni kiasi kiduchu mno kulinganisha na posho za maofisa wa TFF watakaokwenda kwenye ziara za mafunzo zinazokusudiwa ndani na nje ya nchi.

Hakuna kiasi cha fedha ambacho kinatosha, tunafahamu Nipahe, hivyo malipo ya sasa ya posho za sh.15,000 kwa siku kwa kambi za nyumbani na dola 30 kwa siku kwa safari za nje kinaweza kuwa kikubwa ama kidogo kutegemeana na uzalendo wa wachezaji wa Taifa Stars kwa nchi yao.

Lakini uzalendo huu, Nipashe tunafahamu, hautakuwa rahisi kuonyeshwa kama wachezaji hao watahisi kuna harufu ya kutumika kwa migongo yao kunufaisha wachache wenye kusimamia mkataba huo kwa kisingizio cha udhanini wa Taifa Stars.

Hapa ndipo uwazi katika manunuzi ya vifaa bora vilivyoahidiwa zikiwemo jezi za timu, kwa mfano, utakapohitajika. Ni Adidas? Ni Puma? Ni Nike? Ni vifaa halisi? Ni vya 'kichina'?

Basi la wachezaji, hata liwe la kisasa namna gani, haliingii uwanjani kufunga magoli yatakayoiwezesha Stars kukwea chati za FIFA na kucheza fainali za mashindano makubwa ya Afrika na dunia.

Lakini ununuzi wa basi hilo unaweza kuongeza kiwango cha uchezaji wa timu kama wachezaji watafahamu kuwa lilinuliwa katika mazingira ya uwazi kama ambavyo manunuzi ya jezi za timu yanapaswa kuwa katika mazingira kama hayo.

Ni kiasi gani cha fedha za udhamini kitatumika katika matangazo ya kuipromoti TBL?

Uwazi, tunaonya Nipashe, ndiyo mpango mzima kama kweli TBL na TFF zinataka kuona faida ya udhamini wa mabilioni hayo kwenye soka la Tanzania.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles