


.jpg)
Mabingwa wa soka wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba jana walifanisha kumsajili mshambuliaji wa Azam na timu ya Taifa (Taifa Stars), Mrisho Ngassa kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja.
Simba ilifanikisha mipango hiyo baada ya kuwazidi nguvu mahasimu wao wa jadi, Yanga, ambao pia walipeleka ofa ya kumuhitaji Ngassa lakini wakapigwa kumbo baada ya kuwasilisha dau ‘mbuzi’ la Sh. milioni 20.
Awali, uongozi wa Azam ulishatangaza kuwa uko tayari kumuuza winga huyo kwa klabu yoyote itakayotoa dau la dola 50,000 (sawa na zaidi ya Sh. milioni 80), jambo ambalo limeonekana kuwa gumu kabla ya Simba kumpata mchezaji huyo kwa ofa ya mkopo ya Sh. milioni 25.
Ngassa ambaye alitakiwa sana na kocha wa Simba, Milovan Circkovic, anatarajiwa kuichangamsha safu ya ushambuliaji ya timu yake mpya katika ligi kuu ya Bara na pia katika michuano itakayoanza mapema mwakani ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
Akizungumza na gazeti hili jana, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema jana kuwa wamemsajili Ngassa kwa mkopo na tayari wamefikia makubaliano na Azam, hivyo mchezaji huyo ataichezea timu yao katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambayo inatarajiwa kuanza Septemba Mosi.
Kaburu alisema kuwa wamemsajili mshambuliaji huyo kutokana na maelezo ambayo walipewa na Cirkovic ili kuziba nafasi ya Emmanuel Okwi ambaye sasa anaelekeza nguvu zake katika kusaka timu atakayoichezea soka la kulipwa barani Ulaya.
"Usajili wa Ngassa umeshakamilika, ni mali yetu kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kukamilisha usajili wake wa kuichezea Simba kwa mkopo," alisema Kaburu.
Meneja wa Azam, Patrick Kahemele, alisema kuwa wameamua kumpeleka Ngassa Simba kutokana na maelezo ya Cirkovic kumuhitaji ambapo wanaamini ataendeleza kipaji chake na kuendelea kuisaidia Taifa Stars.
Kahemele alisema kuwa Azam ilifikia maamuzi ya kumuuza mshambuliaji huyo baada ya kuonyesha hadharani mapenzi aliyonayo na mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga.
Mapema wiki hii Azam ilitangaza kwamba iko tayari kumuuza Ngassa kwa gharama ya Dola za Marekani 50,000 baada ya nyoya huyo kuonyesha mapenzi yake kwa Yanga kwa kuvaa na kuibusu nembo ya klabu hiyo wakati akishangilia goli aliloifungia Azam katika mechi yao ya nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ngassa aliyeihama Yanga mwaka juzi aliisaidia Azam kumaliza kwenye nafasi ya pili katika msimu wa ligi uliopita ambapo mwakani itashiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya Kombe la Shirikisho yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).