Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wizara ya Afya, MSD jipangeni ili muondokane na lawama hizi

5th April 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Asilimia kubwa ya wagonjwa wanakwenda kwenye hospitali za serikali (umma) kupata matibabu aghalab huishia kuwaona madaktari na kisha kuandikiwa dawa, lakini wakifika kwenye dirisha la dawa lugha wanayokutana nayo ni kwamba hakuna dawa. Wenye fedha hununua dawa walizoandikiwa kwenye maduka ya dawa ya watu binafsi, tena yakiwapo ya hao madaktari wenyewe.

Hali hii ya kukosekana kwa dawa katika hospitali za serikali imekuwa ni kawaida, wananchi wamezoe na wengine hawalalamiki tena, hata hivyo, hali hiyo inaendelea wakati dawa za mabilioni ya fedha kila mwaka zinateketezwa baada ya muda wake wa matumizi kumalizika zikiwa zimehifadhiwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Juzi Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ilibaini kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imepata hasara Sh. bilioni 4.7 kutokana na dawa zilizonunuliwa na MDS kukaa bila kutumiwa na mwishowe zikaharibiwa, pia vifaa vyenye thamani ya Sh. bilioni 1.6  vilivyonunuliwa havikupokelewa, kwa maneno mengine ni vifaa hivyo ni hewa na vilivyonunuliwa kwa mwaka wa fedha wa 2010/2011.

Ni vigumu kupata maneno ya kuelezea hali hii, kwamba kodi za wananchi zinatumika kununua dawa, kutoka kokote ndani au nje ya nchi, halafu zinarundikwa stoo wakati hospitali za umma zikizihitaji kwa ajili ya wagonjwa, lakini hazifiki na matokeo yake zinakaa hadi muda wake wa matumizi unafika ukomo hivyo kuharibiwa.

Hakika hali hii haina tofauti yoyote na mtu aliyechukua fedha zake na kuzichoma moto. Ni uharibifu mkubwa wa rasilimali muhimu zinazohitajika kwa ajili ya stawi wa watu wa taifa hili. Lakini pia ni haki na halali kabisa kueleza hali hii kama madudu mengine ya taasisi za serikali katika uendeshaji wa shughuli zake.

Kama alivyosema Mwenyekiti wa PAC, John Cheyo, kuwa wameshtushwa na madudu hayo kwa kuwa zipo hospitali zilizo hoi kutokana na kukosa dawa, lakini vitabu vya wizara vinaonyesha kuwa dawa za mabilioni ya fedha zimeharibiwa kutokana na kwisha muda wake wa matumizi. Wahusika wametakiwa kutoa maelezo ya kina.

Wakati madudu haya yakitokea, MSD wanalalamika kuwa wanakabiliwa na hali ngumu kwani wakati mahitaji ya dawa nchini kwa sasa yanafikia thamani ya Sh. bilioni 150 zikiwa ndizo fedha walizoomba serikalini kwa mwaka wa fedha wa 2011/12, ni kiasi cha Sh. bilioni 78 tu kiliidhinishwa, lakini hata hicho kidogo matumizi yake yamezingirwa na uzembe wa hali ya juu.

Habari zinasema kuwa kwa mwaka wa fedha unaokuja MDS wanatarajia kuwa mahitaji ya dawa na vifaa yatafikia kiasi cha Sh. bilioni 198, hali inayoonyesha kuwa bado suala la upatikanaji wa dawa katika hispitali za umma si wa uhakika kwani mahitaji ni makubwa kuliko kiasi cha fedha kinachotengwa. Ni miujiza tu itawezesha kupatikana kwa Sh. bilioni 198 kama bilioni 150 ilikuwa vigumu kuidhinishwa.

Pamoja na changamoto hii ya ufinyu wa bajeti, kila tunapotafakari hali hii ya kuharibika kwa dawa kwa sababu tu hazikusambazwa kwenye hispitali mbalimbali za umma nchini, tunashindwa kupata majibu ni kwa nini tatizo hili mwaka baada ya mwaka halimaliziki kwani hata mwaka jana kulikuwa na tatizo la kuharibika kwa dawa zenye thamani ya mabilioni kwa kuwa tu hazikusambazwa.

Kumekuwa na kurushiana lawama baina ya watendaji wa MSD na hospitali za umma juu ya hali hii. Wakati hospitali zikilalamika kuwa maombi yao yanapopelekewa MSD kumekuwa na urasimu wa kuyashughulikia, MDS nao wamekuwa wakilalamika kuwa maombi kutoka hospitali hizo yamekuwa yakichelewa mno, kiasi cha kuathiri utoaji na usambazaji wa dawa hizo.

Kwa vyovyote itakavyochukuliwa kuna tatizo la ama kiutendaji au kimfumo katika suala zima la usambazaji wa dawa kutoka MSD kwenda hospitali za umma; Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ndiyo msimamizi mkuu wa sera za afya katika nchi hii, ni aibu na ni jambo lisilokubalika kuona kuwa mwaka baada ya mwaka dawa zenye mabilioni ya thamani zinateketezwa huku wagonjwa wanaopatiwa huduma katika hospitali za umma wakizikosa kwa sababu tu hazijasambazwa. Ni kwa maana hiyo tunasema sasa hali hii ni lazima ifike mwisho.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles