Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

NHC yazindua mradi wa kuuza nyumba 48

25th April 2012
Print
Comments

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limezindua mauzo ya nyumba 48 katika mradi wake mpya wa Mchikichini, Ilala, jijini Dar es Salaam ambao ujenzi wake unaogharimu Sh. bilioni 4, unatarajiwa kukamilika Februari, mwakani.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa NHC, David Shambwe, alisema jana kila nyumba itauzwa kwa Sh. 168,239,748.62 bila mnunuzi kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Alisema uzinduzi wa mauzo ya nyumba za mradi huo unalenga kutimiza malengo ya mkakati wa shirika wa miaka mitano ya kujenga nyumba 15,000 ambazo kati ya hizio, nyumba 10, ni za wananchi wa kipato cha kati na cha juu na nyumba 5,000 kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini.

Shambwe alisema mnunuzi wa nyumba hizo atafaidika na huduma zote muhimu za kijamii, zikiwamo za kiafya, shule, maduka, uwanja wa ndege, masoko, ulinzi na usalama pamoja na maegesho ya gari.

Alisema mradi huo una nyumba 48 tu zitakazouzwa, ambapo kila nyumba ina vyumba vitatu vya kulala, sebule kubwa yenye veranda, chumba kimoja cha kulala kinachojitegemea, vyumba viwili vya kulala (vinavyotumia choo cha pamoja), jiko kubwa la kisasa na eneo la kufulia na kuanikia nguo.

Mwombaji wa kununua nyumba hizo, atapata fomu za maombi kutoka ofisi yoyote ya NHC au kwenye tovuti ya shirika hilo kisha atarejesha fomu zilizojazwa kwenye ofisi ya shirika akiambatanisha uthibitisho wa malipo ya asilimia 10 ya thamani ya nyumba kuonyesha dhamira na uwezo wake wa kununua.

Alisema maombi yote yatapitiwa ili kuhakikisha haki inatendeka na taratibu zote za shirika na serikali kuhusiana na ununuzi wa nyumba zinafuatwa.

Waombaji watapewa barua ya toleo, lakini kwa wale tu watakaokuwa wamewahi na wametimiza vigezo vyote vya kuweza kununua nyumba.

Shambwe alisema waombaji waliopewa barua za toleo watatakiwa kumalizia asilimia 90 ya malipo yaliyosalia ndani ya siku 90 toka tarehe ya toleo na kwamba uthibitisho wa malipo unaweza kutolewa  kwa kuonyesha hati ya malipo kwenye akaunti benki husika au hati ya kupewa mkopo toka benki.

Benki hizo alizitaja kuwa ni NMB, NBC, Standard Charterd, Stanbic, CBA na KCB.

Alisema baada ya siku 90 kupita bila mwombaji kuonyesha uthibitisho wa utaratibu wa kulipa, nyumba husika atapewa mtu mwingine kutoka kwenye orodha ya waombaji wanaosubiri.

Alisema asilimia 10 ya malipo ya awali iliyolipwa na waombaji walioshindwa au waombaji wapya inaweza kutumika kuomba kununua kwenye mradi mwingine au inaweza kurejeshwa kwa mhusika.

Alisema mara tu pale wanunuzi watakapokuwa wamekamilisha malipo yao, shirika litatangaza kuwa mauzo kwenye mradi huo yamefungwa na kwamba shirika litatafuta hati za nyumba hizo na kuzikabidhi kwa wanunuzi au kwenye taasisi za fedha zilizowakopesha.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles