Monday May 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wakenya walima bangi Mara

12th May 2012
Print
Comments
Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa

Baadhi  ya viongozi wa vijiji wa wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara, wanatuhumiwa  kuwakodishia ardhi   Wakenya kwa ajili ya kulima bangi, hatua inayochochea migogoro na vita baina ya koo.

Madai hayo yaliibuliwa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mara,  John Tupa , kwenye mkutano wa  Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara na baadhi ya wananchi wa vijiji viwili vya wilaya hizo  ambapo walisema  wanapata wakati mgumu kupata ardhi kwa ajili ya uzalishaji kwa kuwa viongozi wamewapa wageni kutoka nchi jirani  ili kulima bangi.

Tuhuma hizo zilitolewa katika mkutano wa hadhara ambao uliitishwa na kamati hiyo ya ulinzi na usalama ulioshirikisha  wakazi wa vijiji vya Ikoma wilayani Rorya na Nyamuhunda wilayani Tarime  kuzima mapigano ya koo ambayo yamesababisha nyumba kadhaa kuchomwa moto na mamia ya ekari za mazao mashambani kufyekwa katika kijiji cha Ikoma na kupora mali za wananchi.

“Sisi wenyeji kama tukibahatika kupata ardhi ni lazima utoe mlungula  kiasi kisichopungua  Sh. 200,000 ambapo fedha hizo wanapokea bila kushirikisha mikutano ya vijiji”, alidai msemaji mmoja na kuungwa mkono na wanavijiji wengine.

Mbunge wa jimbo la Rorya  Lameck Airo,  alikiri kuwepo kwa matatizo hayo katika jimbo lake lakini kila alipojitahidi kufuatilia alisema anashindwa kupata ukweli kwa kile alichodai kuwa mchezo huo mchafu ulikuwa unafanywa na baadhi ya viongozi wa vijiji bila kuwashirikisha wananchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mara   John Tupa, akizungumza katika mkutano huo uliofanyika mpakani mwa vijiji hivyo, aliwaonya viongozi hao na kuwataka kuacha mara moja kukaribisha wageni katika ardhi hiyo kinyume cha sheria.

Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Mara,  Jacob Sambai, akizungumza katika hadhara  hiyo alisema kitendo kinachodaiwa kufanywa na viongozi hao wa vijiji kukodisha ardhi kwa watu kutoka nje ya nchi ni uvunjifu mkubwa wa sheria.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment