



Rais Jakaya Kikwete amesema bila utawala bora maendeleo yatachelewa.
Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), aliyasema hayo wakati akifungua semina ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho juu ya Mpango wa Kujitathimini Kiutawala Bora kwa nchi za Afrika (APRM).
“Hakuna Good Governance (utawala bora), hakuna kuheshimu sheria, hakuna haki za binadamu, maendeleo yatakuwa magumu, yatachelewa,” alisema
Alisema chini ya mpango huo nchi hujitathimini wenyewe, ambapo tume ya mpango huo imeshakuja nchini na kufanya tathimini na inatarajiwa katika kikao cha Umoja wa Nchi za Afrika (AU), ripoti hiyo itatolewa.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa APRM nchini, Rehema Twali, alisema katika ripoti hizo kuna changamoto mbalimbali ambazo zimeanishwa na wananchi.
Alisema katika eneo la siasa na demokrasia, maoni ya wananchi yanelenga katika muundo.
“Bado wananchi wanamaoni kuhusiana na mgawanyo wa rasilimali, lakini wananchi wanaenda mbali zaidi ya ni namna gani ambavyo changamoto hizo zitatuliwe,”alisema.
Alisema maoni mengine yaliyomo katika ripoti hiyo ni eneo la kupambana na rushwa, ambapo wananchi wametaka kuimarishwa kwa taasisi zinazozuia na kupamba na rushwa ziweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Wakati huo huo, Rais Kikwete, alitarajiwa kuondoka jana kwenda nchini Marekani, kwenye mkutano wa kimataifa wa kujadili uchumi wa dunia ikiwemo Mpango wa Kilimo Kwanza.
Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ambapo alieleza kuwa, nchi wafadhili zimekubali kusaidia Mpango wa Kilimo Kwanza baada ya kuridhika na mpango huo.